Air Tanzania yasema ndege ilipata ‘hitilafu ya kawaida’

Esau Ng'umbi 0756Hrs   Februari 29, 2024 Habari
  • Yasema ndege hiyo haikuungua bali ili ilipata hitilafu ilitokana na injini kupata joto jingi na kusababisha moshi.
  • Wabainisha tukio hilo ni la kawaida kwa vyombo vya usafiri ndio maana hawakutoa taarifa.

Dar es Salaam. Shirika la ndege Tanzania (ATCL) limeeleza kuwa ndege yake aina ya Airbus A220-300 iliyokuwa ikisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya Februali 24, 2024 ilipata hitilafu kwenye moja ya injini zake na kusababisha moshi ndani ya chombo hicho huku likieleza kuwa tukio hilo ni la “kawaida” kwenye sekta usafiri wa anga. 

Maelezo hayo ya shirika hilo ambalo hujulikana zaidi kama Air Tanzania yanakuja baada ya kuwepo mjadala mkali mtandaoni kufuatia kuchapishwa kwa habari na gazeti la Mwananchi kuwa injini moja ya ndege hiyo ilishika moto na kusababisha “hekaheka” kwa abiria. 

Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL Ladislaus Matindi amewaambia wanahabari leo Februali 29, 2024 jijini Dar es Salaam kuwa kilichotokea ni hitilafu ya kawaida iliyosababishwa na kuongezeka kwa joto katika moja ya injini.


Kwa mujibu wa Matindi harufu ya moshi na moshi ulio onekana kwa abiria waliopanda ndege hiyo iliyoanza safari majira ya saa 12 asubuhi ulitokana na tatizo la injini moja ya hiyo ndege.

“Kulikuwa na injini moja iliyopata joto sana na kutokana na jinsi inavyofanya kazi kunakuwa na mafuta mengi sana, yale mafuta ndio yaliyoanza kutoa moshi na sio kuungua, ule moshi ukaingia kwenye mfumo wa kurekebisha hewa na ukaonekana sehemu ya kukaa abiria,” amesema Matindi.

Hata hivyo, ndege hiyo ililazimika kurejea Dar es Salaam na baada ya saa chache baadhi ya abiria waliendelea na safari huku wengine wakibadili tarehe ya safari.

Matindi amesema hali ndani ya ndege hiyo haikuwa ya kutisha na marubani na wahudumu wengine walichukua hatua za kiusalama kwa kuwapa taarifa abiria na kuwasihi kuwa watulivu na wasiwe na wasiwasi.

"Hali ya moshi ndani ya ndege ilidumu kwa dakika tano tu na ilichukua dakika 25 ndege kurudi Dar es Salaam na abiria walibadilishiwa ndege na 104 kati ya 122 waliendelea na safari huku 18 wakiomba kubadilishiwa siku ya safari," amesema Matindi.

Taarifa za tukio hilo zilianza kusambaa Februari 27 mwaka huu lakini Air Tanzania haikuwa imetoa taarifa yeyote licha ya kuwa tukio hilo liliibua hofu miongoni mwa wasafiri. 

Alipoulizwa na wanahabari kwa nini walikaa kimya, Matindi amesema hawakutoa taarifa kuhusiana na tukio hilo kutokana na taratibu za usafiri wa anga kutaka kuripoti tatizo kubwa na ajali.




Katika taratibu hizo, bosi huyo amesema katika usafiri wa anga huwa kuna matatizo madogo, matatizo makubwa na ajali. 

“Hatuwezi kutoa taarifa ya kila kitu hata tairi likiishiwa upepo," amesema Matindi.

Hata hivyo, sehemu kubwa ya mjadala mitandaoni ilikuwa ikihoji juu ya usalama wa ndege hiyo, jambo ambalo Air Tanzania imesema halipaswi kuzua hofu.

Injini imetoka matengenezo 

Kwa mujibu wa Matindi, injini iliyopata changamoto hiyo ilikuwa imetoka kufanyiwa matengenezo kupitia kampuni ya Pratt & Whitney (PW) ya nchini Ujerumani na tangu kurejea imeshafanya safari kwa saa 200 tu, hivyo kwa mujibu wa makubaliano itarejeshwa tena kwa matengenezo.

Kwa upande wake Mkuu wa usalama wa ndege za ATCL, Emmanuel Tivai amesema jambo lililotokea ni la kawaida kwa vyombo vya usafiri na kwamba hatua zinazochukuliwa baada ya tukio ndio muhimu zaidi.

"Inapotokea tatizo kama hilo hatua kadhaa huchukuliwa ikiwa ni pamoja na kurudisha ndege uwanjani ili iangaliwe na wahandisi wake na hicho ndicho kilichofanyika," amesema Tivai.

Related Post