Air Tanzania kuajiri wahudumu wa ndege 88 kuimarisha uendeshaji

Mwandishi Wetu 0329Hrs   Januari 13, 2018 Biashara
  • Kiwango cha ajira mpya zilizotangazwa na ATCL ni kikubwa tangu mwaka 2018 uanze.
  • Wahudumu hawatakiwi kuwa na urefu wa chini ya futi tano na nchi mbili.
  • Ajira hizo ni moja ya hatua za kuendelea kuifufua kampuni hiyo.


Dar es Salaam. Katika jitihada za kuongeza ufanisi wa biashara, Kampuni ya ndege ya Air Tanzania (ATCL) imetangaza ajira mpya za wahudumu wa ndege 88, ikiwa ni moja ya fursa kubwa ya ajira kutangazwa nchini ndani ya siku 10 za mwanzo za mwaka 2018.

Katika tangazo la nafasi za kazi lililochapishwa kwenye tovuti (Kiingereza) ya ATCL Januari 9 na gazeti la Daily News, kampuni hiyo inatafuta wahudumu Watanzania wenye elimu isiyopungua kidato cha nne na cheti cha uhudumu ndege (Cabin crew) kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCCA).

Mbali na taaluma, ATCL inataka wahudumu hao wawe na umri wa miaka kati ya 18 na 27 kwa wasio na uzoefu na wazoefu wasiwe na zaidi ya miaka 40.

“Wanaoweza kuzungumza na kuandika Kiingereza na Kiswahili. Uelewa wa lugha nyingine za kimataifa kama Kifaransa, Kiarabu, Kichina na Kihindi itakuwa ni sifa ya ziada,” inasomeka sehemu ya tangazo hilo na kuongeza;

“Urefu wa futi tano na nchi mbili na zaidi na uzito unaoendana na mwili.”

Nafasi hizo za ajira ni moja ya hatua kubwa ya maboresho ambayo ATCL inayafanya baada ya kuongezewa ndege mbili na Serikali mwishoni mwa mwaka 2016 aina ya Bombardier Q400 Next Gen.

Hadi sasa ATCL inayomilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 ina ndege tatu ikiwemo ya awali iitwayo Dash8-Q300 iliyokuwa ikitumika tangu mwaka 2011.

Moja ya ndege zilizokuwa zikitumika na Air Tanzania miaka ya nyuma. Serikali imeanza kuifufua kampuni hiyo kwa kuinunulia ndege nyingine nne.

Katika kuendelea kuifufua kampuni hiyo, Serikali imepanga kuiongezea ndege nyingine ATCL ikiwemo Bombardier Q400, Boeing 787 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba abiria 262 na mbili Bombardier CS300 zenye uwezo wa kubeba abiria kati ya 137 na 150.

Ndege ya Bombardier Q400 iliyotakiwa kufika katikati ya jana, inashikiliwa nchini Canada baada ya kampuni ya ujenzi ya Stirling Civil Engineering kutokana na deni inalolidai Serikali la Dola za Marekani milioni 38 wastani wa Sh84.7 bilioni (Kwa viwango vya sasa vya kubadilishia fedha). Serikali ilisema kuwa inaendelea kuchukua hatua ya kumaliza mgogoro huo ili kuirejesha.

“ATCL ipo kwenye mchakato wa kuboresha uendeshaji wake na imeongeza ndege mpya katika safari zake,” linasomeka tangazo hilo linaloeleza kuwa mwisho wa kuomba nafasi hizo za kazi ni Januari 23, 2018.

Kampuni hiyo ya umma sasa inafanya safari zake kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, Kilimanjaro, Mwanza, Kagera, Mbeya, Kigoma, Arusha Tabora, Ruvuma, na Mtwara na Hahaya nchini Commoros.


Related Post