Samia ataja vipaumbele siku 100 za kwanza akichaguliwa kuwa Rais
- Ni pamoja na kuboresha sekta ya elimu, afya, kutoa nafasi za ajira na kuanza kwa mchakato wa Katiba mpya.
Dar es Salaam. Mgombea wa Urais wa Tanzania kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Samia Suluhu Hassan ametaja vipaumbele atakavyotekeleza katika siku 100 za kwanza iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Tanzania ikiwemo kutoa nafasi za ajira na kuanza mchakato wa katiba mpya.
Samia aliyekuwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa kampeni za uchaguzi za chama hicho leo Agosti 28, katika viwanja vya Kawe jijini Dar es Salaam amesema iwapo Watanzania watampa ridhaa ya kukalia kiti cha Urais kwa kumpigia kura,ndani ya siku 100 ataboresha huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo huduma za afya, elimu.
Samia ambaye anaomba ridhaa ya kuendelea kuwa Rais wa Tanzania kwa muhula wa pili wa awamu yake ya sita amesema ndani ya siku 100 atatoa kutoa nafasi za ajira hususan kwa walimu wa Masomo ya Sayansi na Hisabati pamoja na wataalamu wa afya.
“Tutaandaa mkakati madhubuti wa kisayansi, kuhakikisha kila mtoto wa darasa la tatu anaweza kusoma, kuhesabu na kuandika bila shida na katika kulitimiza hili tutaajiri walimu 7,000 wa Masomo ya Hisabati na Sayansi,” amesema Samia.
Kuboresha huduma za afya
Aidha, katika kuboresha huduma za afya Samia amesema atazindua Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa wote kwa awamu ya majaribio utakaojumuisha wazee, watoto, mama wajawazito na watu wenye ulemavu ambapo gharama za matibabu za makundi hayo yote zitabebwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Vilevile amesema Serikali atakayoiunda itaanza kugharamia matibabu na vipimo vya kibingwa kwa wananchi wasio na uwezo ambapo matibabu hayo hatahusisha magongwa yasio ya kuambukiza ikiwemo magonjwa ya saratani, figo, moyo, sukari, mifupa na mishipa ya fahamu.
Aidha, ili kuhakikisha sekta hiyo inakuwa imara pamoja na kuajiri wahudumu wa afya 5,000 Serikali yake itapiga marufuku kwa hospitali yeyote kuzuia miili ya waliofariki kwa kushindwa kulipa gharama za matibabu.
Samia amesema atahakikisha unawekwa utaratibu mzuri utaowawezesha ndugu wa marehemu kulipia gharama husika baada ya mwili wa mpendwa wao kupumzishwa.
Katika hatua nyingine, Samia amesema kuwa atatenga kiasi cha Sh200 bilioni ili kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa wafanyabiashara wadogo na wakati pamoja na kuwezesha uendeshaji wa kampuni changa.
“Tutarasimisha sekta isiyo rasmi ikiwemo wakina mama lishe, bodaboda na bajaji na wajasiriamali wadogo ili waingie mfumo rasmi wa Serikali ili waweze kupata huduma zao,” ameahidi Samia.
Aidha, katika kuhakikisha kuwa kuwa kuwa na vyanzo vya uhakika vya maji kwa ajili ya matumizi ya majumbani, kilimo, mifugo na biashara, Serikali itaanzisha Gridi ya Taifa ya maji ambayo itahusisha vyanzo vikubwa kama Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa.
Katiba mpya
Moja kati ya mambo ambayo yamekuwa yakizungumziwa sana hususan na upinzani ni kurejeshwa mchakato wa katiba mpya ambapo Samia amesema endapo atachaguliwa kuwa Rais, ataanzisha Tume ya Maridhiano na Upatanishi pamoja na kuandaa mazingira ya kuanza kwa mchakato wa Katiba mpya.
“Kwa ujumla, tumejipanga kuongeza nguvu si tu kwenye miundombinu bali pia kwenye ubora wa huduma zinazotolewa, kusimamia haki, amani na utulivu wa kisiasa” ameahidi Samia.
Hata hivyo, hoja ya katiba mpya si ngeni kwa wanasiasa wa CCM kipindi cha kampeni, ni miongoni mwa ahadi iliyotolewa na Rais wa awamu ya tano wa Tanzania Hayati John Pombe Magufuli ambaye hakuitekeleza ndani ya siku 100 alipoingia madarakani.
Latest