Rais Samia kupokea tuzo ya mafanikio Ghana wiki hii

May 23, 2022 8:37 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ataipata akiwa katika ziara ya siku tatu nchini humo.
  • Ptuzo hiyo inamtambua kiongozi wa nchi aliyapata mafanikio katika ujenzi wa miundombinu.
  • Rais pia atashiriki mkutano wa wakuu wa nchi kuhusu mabadiliko ya tabianchi na kupanda kwa bei za bidhaa. 

Dar es salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameondoka nchini leo kuelekea Ghana  kwa ajili ya  ziara ya kikazi ya siku tatu, ambapo pamoja na shuguli nyingine anatarajiwa kupokea tuzo ya mwaka 2022 ya Babacar Ndiaye.

Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Jaffar Haniu katika taarifa yake iliyotolewa leo Mei 23,2022 amesema Rais Samia akiwa Ghana anatarajiwa kupokea tuzo ya mwaka 2022 ya Babacar Ndiaye kwa mafanikio ya serikali ya awamu ya sita katika ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji ambayo hutolewa  kwa mkuu wa nchi iliyofanya vizuri zaidi.

Tuzo hiyo hutolewa katika mkutano wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ambao kwa mwaka 2022 unafanyika Accra, Ghana.

Nchi nyingine zilizowahi kushinda tuzo hizo ni pamoja na nchi ya Nigeria chini ya Rais Muhammadu Buhari mwaka 2021 na Misri chini ya Rais Abdel Fattah Al-Sisi, mwaka 2020.


Soma zaidi:

Tanzania itakavyofaidika ziara ya Rais Samia nchini Ufaransa, Ubelgiji


Ziara hiyo itampa pia kiongozi huyo mkuu wa nchi fursa ya kushiriki mdahalo wa wakuu wa nchi utakaojadili fursa zilizopo na changamoto zinazokabili nchi za Afrika ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabianchi, kupanda kwa bei ya vyakula na nishati endelevu.

Nchi za Afrika ikiwemo Tanzania kwa sasa zinashuhudia kuongezeka kwa bei za bidhaa ikiwemo mafuta ambazo zimechangiwa na athari za vita inayoendelea sasa kati ya Urusi na Ukraine.

Kuitishwa kwa mkutano huo huenda kutasaidia kupatikana kwa suluhu za kuwapunguzia wananchi makali ya maisha kulikosababishwa na kupanda kwa bei ya bidhaa. 

Hii inakuwa ziara ya pili ya Rais Samia katika kipindi cha mwezi mmoja, ambapo ziara yake ya mwisho ya kikazi  ilikuwa nchini Uganda ambapo alifanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Yoweri Museveni.

Pia alishuhudia utiaji saini wa hati ya ushirikiano, kutembelea na kujionea uzalishaji wa kiwanda cha chuma, pamoja na kuhudhuria mkutano wa biashara na watendaji wakuu wa sekta binafsi.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW