Rais Samia atamani maboresho makubwa JKT
- Lengo ni kuwa na jeshi la kisasa, linaloendana na wakati na kutimiza majukumu kwa ufanisi.
- Asisitiza umoja, mshikamano, kufanya kazi kwa moyo na kujitolea.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema ni dhamira ya Serikali kulifanya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) liwe la kisasa, linaloendana na wakati pamoja na kutimiza majukumu yake kwa ufanisi wa hali ya juu.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika maadhimisho ya miaka 60 tangu kuasisiwa kwa JKT leo Julai 10, 2023 jijini Dodoma amesema Serikali itashughulikia changamoto zinazolikabili jeshi hilo ikiwemo kuboresha makambi na vitendea kazi ili mafunzo yanayotolewa yawe na tija.
“Mafunzo yanayotolewa na JKT yawasaidie vijana kuwa wazalendo wa kweli wanaothamini utaifa, umoja na mshikamano wa Watanzania, na wanaopenda kufanya kazi kwa moyo wa kujituma na kujitolea,” amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia ameiagiza Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, kuandaa mpango mkakati wa kuboresha makambi ya JKT hususani katika upande wa malezi ya vijana.
Ili kulisaidia jeshi hilo kujiendesha kiuchumi, Serikali inakusudia kuliwezesha kifedha Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (Suma JKT) kupitia mikopo.
Samia amewataka watakaoajiriwa katika vyombo vya ulinzi na usalama mara baada ya mafunzo kutimiza majukumu yao kwa weledi, uaminifu wa kutumainiwa pamoja na kutetea nchi yao bila hofu.
Kwa upande wake Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Innocent Bashungwa amesema jeshi hilo litaendelea kuwa chombo muhimu kuwaandaa vijana, kuwajengea nidhamu, uzalendo, ukakamavu na kuwafundisha ujuzi ambao unasaidia katika ulinzi wa Taifa na maendeleo ya kiuchumi.
Soma zaidi
-
Rais Samia abadilisha miundo ya wizara, Kitila Mkumbo ateuliwa waziri
-
Mfahamu Paulina, mwanamke msomi anayetengeneza majiko banifu Dodoma
Kwa mujibu wa Bashungwa mwaka 2023 JKT imepokea zaidi ya wahitimu 52,000 wa kidato cha sita ambao watapokea mafunzo maalumu kwa muda wa miezi mitatu kabla ya kuendelea na masomo ya ngazi ya juu.
Historia ya JKT
Jeshi hilo liliasisiwa rasmi Julai 10, 1963 kufuatia utekelezaji wa Azimio la Kikao cha Baraza la Mawaziri. Kikao hicho kilifanyika Aprili 19, 1963 chini ya uongozi wa Rais wa Kwanza wa Tanganyika Mwalimu Julius Nyerere na mwaka 1964 Bunge lilitunga Sheria ya kuanzishwa kwa JKT.
Kwa mujibu wa Sheria ya mwaka 1964 kujiunga na JKT ilikuwa jambo la kujitolea hivyo mwaka 1966 sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho na kuanzisha utaratibu wa kujiunga JKT kuwa lazima kwa mujibu wa Sheria.
Utaratibu huu uliwahusu vijana waliohitimu vyuo vikuu, vyuo vya elimu ya juu, kidato cha sita na waliomaliza kidato cha nne ambao wamepata mafunzo kwenye vyuo vya taaluma mbalimbali kama vile ualimu, uganga, uuguzi na kadhalika.
Hata hivyo, utoaji wa mafunzo hayo ulisitishwa miaka ya tisini kutokana na kudorola kwa uchumi kabla ya kurejeshwa tena na Rais Jakaya Mrisho Kikwete mwaka 2013.
Latest
