Dk Mpango: Polisi, Takukuru shirikianeni kudhibiti rushwa Uchaguzi Mkuu 2025

August 11, 2025 6:40 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • |Watakaovuruga amani wakati wa uchaguzi kukiona

Arusha. Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Philip Mpango, amelitaka Jeshi la Polisi kuimarisha usalama na kudhibiti vitendo vya rushwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025. 

Kwa mujibu wa Dk Mpango wananchi wanapaswa kuchagua viongozi kwa kuzingatia ilani za vyama na uwezo wa wagombea na si kwa ushawishi wa rushwa unaoathiri maendeleo ya taifa.

Dk Mpango aliyekuwa akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa mwaka wa maafisa waandamizi wa Jeshi la Polisi ameziagiza taasisi za usalama kushirikiana na wadau muhimu, ikiwemo Takukuru kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki. 

“Jeshi la Polisi lishirikiane na wadau wengine muhimu ikiwemo Tume ya Kudhibitii na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili kudhibiti rushwa katika kipindi cha uchaguzi…

…wananchi wanatakiwa kuchagua viongozi kwa kuzingatia ilani za vyama vya siasa pamoja na uwezo halisi wa wagombea, viongozi yanayopatikana kwa vitendo vya rushwa huathiri maendeleo ya wananchi na taifa letu kwa ujumla,” amesema Dk Mpango.

Aidha Dk Mpango ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuliwezesha Jeshi la Polisi ili liwe na weledi na uwezo mkubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki katika kukabiliana na uhalifu.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi Tanzania, limesema limepajipanga vyema kulinda usalama wa nchi kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camillus Wambura amesema hali ya usalama nchini Tanzania ni shwari na wapo tayari kuendelea kulinda amani kuelekea uchaguzi mkuu. 

“Nchi yetu ipo salama, hali ya utulivu ni mkubwa na tuna uhakika kwa jinsi tulivyojipanga na mikakati yetu nchi hii itaendelea kuwa salama…

…Jeshi la polisi limejipanga vyema na kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu ujao  utafanyika kwa amani,” amesema IGP Wambura.

Makamu wa Rais wa Dk. Philip Mpango (kushoto) akipokea tuzo Maalumu kutoka kwa IGP Camillus Wambura.

kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan.Picha|TanPol.

Kauli ya IGP inakuja ikiwa imesalia siku 79 hadi Oktoba 29 inayotarajiwa kuwa siku ya uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani nchini Tanzania, ambapo tayari baadhi ya hatua za kikatiba zimeanza kuteekelezwa kuelekea siku hiyo ikiwemo uchukuaji fomu kwa wagombea wa urais.

Aidha, Wambura amesema kuwa Jeshi hilo halitasita kuwachukulia hatua watu wote watakaotishia kuvunja amani wakati wa uchaguzi kwa mwamvuli wa wa siasa, demokrasia na uwanaharakati hatua inayotajwa kulinda ustawi wa jamii.

“Jeshi la Polisi lipo imara na litahakikishwa kuwa nchi yetu ipo Shwari wakati wote na halitamvumilia mtu au kikundi cha watu watakaojaribu amani kwa namna yoyote kwa kufanya hvyo wananchi watanedelea kufanya shughuli zao za kijamii, kisiasa na kiuchumi katika kuimarisha ustawi wa maisha yao ya kila siku,” IGP amesema Wambura

Pamoja na hayo amesema tayari Jeshi hilo lilishajipatia uzoefu wa kutosha wa kulinda amani kupitia uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwaka 2024 hivyo wamefanyia kazi changamoto zilizojitokeza na kuahidi kuwa hazitojirudia.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW