Jeshi la Polisi lamchunguza aliyetamani kuwa IGP
- Ni aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Wankyo Nyigesa.
- Lasema kauli yake ina ukiukwaji wa nidhamu.
- Amerudishwa makuu ya jeshi hilo kwa uchunguzi.
Dar es Salaam. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Wankyo Nyigesa amerudishwa makao makuu ya Jeshi la Polisi Tanzania ili kupisha uchunguzi kutokana na kauli aliyoitoa wiki iliyopita kuwa anatamani siku moja ateuliwe kuwa mkuu wa jeshi hilo.
Kamanda Nyigesa alitoa kauli hiyo Machi 26, 2022 katika sherehe za kumuaga wakati akihamishwa kutoka Mkoa wa Pwani kwenda Kagera.
Siku hiyo, Nyigesa alinukuliwa na vyombo vya habari akisema anatamani siku moja Rais Samia Suluhu Hassan amuote na kumtamka kuwa IGP wa Tanzania ili akafanye kazi kubwa ya kuleta mabadiliko.
Alisema kazi nzuri imefanywa na IGP wa sasa Simon Sirro na yeye akipewa nafsi atafanya vizuri zaidi ili kuboresha utendaji wa jeshi hilo.
Hata kabla ndoto yake haijatimia, Nyigesa amerudishwa makao makuu na nafasi yake imechukuliwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), William Mwampagale.
Soma Zaidi:
- Watano mbaroni mauaji ya ndugu wa familia moja Mwanza
- Polisi yatoa ufafanuzi zaidi askari anayedaiwa kujinyonga mahabusu Mtwara
Msemaji wa jeshi hilo, David Misime katika taarifa yake iliyotolewa leo Machi 29, 2022 amesema kuwa kauli aliyoitoa inaonyesha kuwepo na ukiukwaji wa nidhamu kulingana na miongozo ya jeshi hilo.
“Suala hilo limeanza kufanyiwa kazi na matokeo ya uchunguzi huo yatafikishwa katika mamlaka za kinidhamu kwa hatua zaidi,” imeeleza taarifa hiyo ya Misime.
Aidha, aliyekuwa Afisa Mnadhimu Mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Theopista Mallya anakuwa Kamanda wa Polisi wa mkoa huo anachukua nafasi ya Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Mwampagale ambaye amehamishwa kwenda kuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera.
Misime amesema aliyekuwa Mkuu wa Operesheni mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Mashenene Mayila anakuwa Afisa Mnadhimu wa mkoa wa Rukwa.
Latest
