Mambo ya kuzingatia kuwa na afya bora 2025

January 1, 2025 8:00 am · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  •  Kula mlo kamili pamoja na kuepuka matumizi mabaya ya pombe na sigara.
  • Fanya mazoezi na pima afya yako mara kwa mara.  

Dar es Salaam. Mwaka 2024, wataalamu wa afya wameendelea kusisitiza umuhimu wa kutunza afya ili tuweze kuisha maisha mazuri yaliyo mbali na magonjwa. 

Kanuni ambazo wamekuwa wakisisitiza ni pamoja na kula lishe bora, kufanya mazoezi mara kwa mara, kuepuka tabia hatarishi kama unywaji wa pombe kupita kiasi na uvutaji sigara na kulinda afya ya akili.

Licha ya kuwa unaweza kupata mabadiliko ya kiafya katika mwili wako ikiwemo uchovu na homa lakini hakikisha mwaka 2025 unaboresha afya yako kwa kuzingatia kanuni ambazo ndio msingi wa afya bora.

Afya bora ni mtaji. Hautaweza kufanya jambo lolote la maendeleo kama afya yako haijakaa sawa. Hakikisha afya iwe uwekezaji namba moja katika maisha yako. 

1. Kula mlo wenye afya
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mwonekano wa mlo wenye afya unaweza kutofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine, kulingana na tamaduni, mahali anapoishi na vyakula vinavyopatikana katika eneo husika.

Hata hivyo, kanuni ni zile zile kufanya maamuzi yenye ufahamu kunaweza kuboresha jinsi unavyokula, kupunguza vyakula vyenye chumvi nyingi, sukari isiyo ya asili, mafuta inaweza kuonekana kama changamoto mwanzoni, lakini hatua ndogo zinaweza kuleta tofauti kama kunywa maji badala ya soda. 

Kula hovyo ni kujiweka katika hatari ya magonjwa sugu, hakikisha unakula lishe yenye virutubisho ili kuulinda afya. Picha /Canva.

Kula angalau sehemu tano za aina tofauti za matunda na mboga kila siku ikiwa ni pamoja na kufikiria kuhusu mlo ulio na uwiano mzuri na uliotofautishwa. Zingatia kula matunda, mboga, nafaka isiyokobolewa, kunde na karanga unapopanga milo yako ya kila siku bila kusahau mapendekezo yaliyowekwa na wataalamu juu ya mlo wenye afya.

2. Fanya mazoezi
Kuwa na shughuli kila siku kunaweza kuwa changamoto, lakini je, unajua kuwa kila harakati huhesabika? Kuongeza matembezi baada ya mlo, kufagia sakafu au kupanda ngazi kunaweza kusaidia afya ya moyo.

Tenga angalau dakika 150 za kufanya mazoezi kwa wiki ikiwa wewe ni mtu mzima. 

Kukosa mazoezi ni sawa na kuufanya mwili wako ushindwe kupambana na magonjwa. Jitunze kwa kufanya mazoezi mara kwa mara. Picha/ Canva.

Kwa faida za ziada za kiafya, watu wazima wanapaswa kuongeza mazoezi ya wastani hadi dakika 300 kwa wiki au sawa na hayo. Ikiwa una watoto au vijana, fanyeni mazoezi pamoja na kuwasaidia kufikia dakika 60 za mazoezi kila siku.

3. Epuka matumizi mabaya ya pombe
Matumizi ya pombe huchangia zaidi ya magonjwa, majeraha na hali nyingine za kiafya takribani 200.

Pombe huongeza hatari ya majeraha na madhara ya muda mrefu kama uharibifu wa ini, saratani, magonjwa ya moyo na magonjwa ya akili. 

Matumizi mabaya ya pombe huharibu afya yako kimwili na kiakili. Picha/ Canva.

Kiwango chochote cha unywaji pombe kina hatari, ikiwa unakunywa pombe, fikiria kujadiliana na mtoa huduma wa afya kuhusu matumizi yako. Punguza pombe na ikiwezekana acha kabisa. 

4. Usitumie tumbaku /sigara

Matumizi yoyote ya tumbaku na kuvuta moshi wa tumbaku ni hatari, hivyo kuacha tumbaku hupunguza hatari ya magonjwa ya moyo, saratani, ugonjwa sugu wa kupumua (COPD) na magonjwa mengine.

Faida za kuacha tumbaku huanza haraka kama dakika 20 baada ya sigara ya mwisho.

Uvutaji wa sigara unakaribisha kifo polepole ingawa vijana wengi wanaovuta sigara wanadai kuwa zinawachangamsha akili. Picha / Canva.

Kuacha matumizi ya sigara za kielektroniki pia ni hatua ya kuelekea kuwa na afya bora. Sigara ni hatari kwa afya yako na zina athari za muda mrefu, hasa kwa vijana, kwa sababu watumiaji hukutana na nikotini na kemikali zingine hatari.

Jiwekee lengo la kuacha na ukishindwa ni vyema ukaenda kuwaona wataalamu wa afya wakupe msaada.

5. Lind afya ya akili
Matatizo ya afya ya akili ni matokeo ya mwingiliano wa sababu tofauti kulingana na mazingira anayoishi mtu. 

Huenda sababu hizo zikawa za kibailojia, kisaikolojia, kijamii ama kimalezi. 

Hata hivyo, Dk Araby amethibitisha kuwa kujitengea utaratibu wa kupumzika pamoja na kula vizuri husaidia kuondoa msongo wa mawazo unaotokana na changamoto za maisha.

Msongo wa mawazo na hofu vinaweza kudhoofisha maisha yako. Tafuta msaada unapohisi mambo hayaendi sawa. Picha /Canva.

‘’Siku hizi hatuangalii afya ya mwili tu tunaangalia na afya ya akili pia. ‘Stress’ (msongo wa mawazo) na ‘depression’ (mfadhaiko) vinapunguza uwezo wa uzalishaji mali pamoja na ufanisi kwenye kazi” anaeleza Dk Araby.

Kubali kuwa changamoto za maisha zipo. Weka kipaumbele katika kutafuta suluhu ya hali ngumu unayopitia. Usikae peke yako, washirikishe watu wa karibu matatizo unayopitia. Omba msaada ukiwa na uhitaji, usikubali kufa na tai shingoni. 

Njia nyingine ya kulinda afya ya akili ni kuweka malengo yanayotekelezeka na kujipatia shughuli ya kufanya ili kuepuka ubongo wako kuwa sehemu mawazo hasi. Fanya jambo unafurahia maishani mwako lakini lisilo la madhara hasi.

6. Ongeza umakini katika matumizi ya barabara

Ajali za barabarani zimebainika kuwa chanzo kikuu cha vifo vinavyoweza kuzuilika.

Kwa mujibu wa Dk Frank Araby, daktari wa magonjwa ya binadamu kutoka hospitali ya Comprehensive Community Based Rehabilitation in Tanzania (CCBRT) iliyopo jijini Dar es Salaam ameiambia Nukta Habari kuwa watu wanaongeze umakini wawapo barabarani ili kuepuka ajali.

Kutokuwa makini barabarani kunaweza kugharimu maisha yako na ya wengine. Tumia barabara kwa tahadhari kubwa. Picha /Canva.

“Ajali za barabarani ni vitu vinavyoongoza sana kuua watu, hivyo ni vyema kuongeza umakini tuwapo barabarani,” anasema Dk Araby.

7. Epuka ngono zembe
Hakikisha mwaka 2025, unaepuka kufanya mapenzi na watu usiowaamini ili kuepuka magonjwa ya ngono.

Dk Araby anabainisha kuwa ni muhimu kuwa na mahusiano na mpenzi mmoja mnaoaminiana ili kuepuka kuwa na magonjwa ambayo huambukizwa kwa njia ya kujamiana.

Ngono zembe ni chanzo cha maambukizi na majuto, chukua hatua salama kila wakati. Picha / canva.

Hata hivyo, kuwa salama wakati wa ngono ni muhimu,kuwa na mpenzi mmoja au kuacha kabisa kujihusisha na mahusiano mpaka uingiapo kwenye ndoa, matumizi ya kondomu, kuwa na tabia ya kupima afya yako mara kwa mara,  vinaweza kukusaidia kuijua afya yako na kuzuia maambukizi ya magonjwa ya zinaa (STIs), mimba zisizotarajiwa na Virusi vya Ukimwi (VVU).

8. Usafi wa mikono

WHO inasisitiza umuhimu wa usafi wa mikono kwa kuzuia maambukizi. Mikono safi huchangia kuokoa mamilioni ya maisha kila mwaka.

“Kuosha mikono kwa sabuni na maji katika nyakati muhimu ni hatua rahisi lakini yenye matokeo makubwa,” WHO inasema.

Kushindwa kunawa mikono kunaweza kusababisha maambukizi hatari, safisha mikono yako kwa sabuni na maji mara kwa mara. Picha /Canva.

Mikono safi husaidia kuzuia kusambaa kwa maambukizi ya magonjwa. Hakikisha unaosha mikono yako sabuni na maji tiririka kabla na baada ya kula. Pia osha mikono mara kwa mara kila unapomaliza kufanya shughuli zako zinazohusisha mikono.

9. Pima afya mara kwa mara

Jenga utamaduni wa kupima afya yako mara kwa mara, angalau mara mbili kwa mwaka ili kujua hali yako ya kimwili na kiakili. Vipimo kama vile vya shinikizo la damu, viwango vya sukari, na magonjwa ya zinaa vinaweza kusaidia kugundua changamoto mapema na kudhibiti maambukizi yoyote kwenye mwili wako. 

Kutojua hali ya afya yako ni hatari kubwa. Pima afya mara kwa mara ili kuishi kwa amani. Picha /Canva.

Kwa kuzingatia vidokezo hivi, mwaka 2025 unaweza kuwa mwaka wa afya bora kwa kila mtu. Kila mmoja anashauriwa kuchukua hatua leo kwa mustakabali bora wa kesho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks