Rais Samia abadilisha miundo ya wizara, Kitila Mkumbo ateuliwa waziri

July 6, 2023 8:12 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Aunda wizara mpya ya Mipango na Uwekezaji.
  • Amemteua Profesa Kitila Mkumbo kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango.
  • Baadhi wasema ni mabadiliko muhimu.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko ya miundo ya Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Viwanda, Biashara na Uwekezaji na kuunda wizara nyingine mpya ambapo amemteua Profesa Kitila Mkumbo kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu jana Julai 5, 2023 mabadiliko hayo yametokana uwepo wa Sheria ya Mipango ya Taifa ya Mwaka 2023 pamoja na uamuzi wa kuhamishia masuala ya uwekezaji Ofisi ya Rais.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa sasa Rais Samia ameunda Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji ambapo amemteua Kitila Mkumbo kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango.

Mkumbo ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo amewahi kuhudumu nafasi ya uwaziri katika Wizara ya Viwanda na Biashara kabla ya kuenguliwa kufuatia mabadiliko madogo yaliyofanywa na Rais Samia mapema mwaka 2022.

Hata hivyo, hii ni wizara ya pili mpya kuundwa tangu Rais Samia aingie madarakani Machi 19, mwaka 2021.

Januari 8, 2022 Rais Samia aliunda Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalumu ambapo aliyekuwa Waziri wa Afya wakati huo Dorothy Gwajima aliteuliwa kuwa waziri wa wizara hiyo.

Itakumbukwa Februari 27 mwaka huu, Rais Samia alipokuwa akiwaapisha viongozi aliowateua Ikulu ya Chamwino Dodoma, aliwambia Watanzania kuwa ofisi ya Msajili wa Hazina, Tume ya Mipango na Uwekezaji zitakuwa chini ya Rais.

“Tutakuwa na waziri wake na naibu waziri wake, tukimaliza mchakato wa sheria itakuwa wizara kamili. Kwa sasa tumetanguliza katibu mkuu atusaidie kupanga, tunafanyaje wanakaaje, mambo ya uchumi, uchumi mkubwa na mdogo tunafanyaje atusaidie kupanga.” alisema Rais Samia.

Juni 8, 2023 Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene aliwasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Tume ya Mipango wa mwaka 2023 ambao  ulipitishwa siku hiyo hiyo.

Pamoja na mambo mengine, tume hiyo itakuwa na jukumu la kubuni, kupanga, kuratibu na kusimamia mipango ya maendeleo ili kuwa na mfumo jumuishi wa ufuatiliaji na tathimini ya utekelzaji wa vipaumbele vya maendeleo ya Taifa.

Prof.Kitila Mkumbo  alipokuwa akizungumza bungeni Mei 22,2021 wakati akiwasilisha hotuba ya Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa Mwaka 2021/2022. Pichal Viwanda na Biashara

Mabadiliko mengine

Kufuatia mabadiliko hayo sasa Mwigulu Nchemba atakuwa Waziri wa Fedha pekee, na Ashatu Kijaji atakuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, mara baada ya sehemu ya wizara zao kupelekwa katika Wizara ya Mipango.

Aidha Rais Samia amemteua Lawrence Nyasebwa Mafuru  kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango ya Taifa kutoka kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango (Usimamizi wa Uchumi) huku Elijah Mwandumbya akiteuliwa  kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha (Usimamizi wa Uchumi).

Kabla ya uteuzi huo Mwandumbya alikuwa Kamishna, Idara ya Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha na Mipango.


Soma zaidi


Wasemavyo wadau

Kufuatia mabadiliko hayo, wananchi wametoa maoni yao. Baadhi wamepongeza na kuunga mkono kilichofanyika huku wengine wakisema mabadiliko hayo yanaiongezea Serikali mzigo wa kifedha kwa ajili ya kuendesha wizara mpya.

Chande Kasita ameandika katika ukurasa wa mtandao wa Instagram kuwa jambo hilo limekaa vizuri kutokana na unyeti na shughuli za Wizara ya Fedha hivyo kulikuwa kuna haja ya kufanya mabadiliko.

“Hii imekaa vizuri. Kutokana na unyeti na activities (shughuli) za Wizara ya Fedha na Mipango kulikuwa na haja ya kufanya restructuring (kuunda upya). Pia uwekezaji na mipango zina uwiano wa karibu sana…,” yanasomeka maoni hayo.

Muda mchache baada ya mabadiliko hayo kutangazwa Zitto Kabwe ambaye ni  Kiongozi Mkuu wa Chama Cha ACT-Wazalendo alichapisha katika ukurasa wake wa Twitter  maneno yanayosomeka ‘A super Minister’ yanayoweza kutafsirika kama kongole kwa Prof Mkumbo kuteuliwa kushika wadhifa huo.

Enable Notifications OK No thanks