Rais Samia asamehe wafungwa 1,548 kuadhimisha miaka 63 ya uhuru

December 9, 2024 3:03 pm · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link
  • 22 kuachiwa huru leo wengine wakitumikia sehemu ya msamaha gerezani.
  • Walioachiwa watakiwa kushirikiana na jamii kwenye ujenzi wa taifa huku wakijiepusha na makosa yatayowarejesha gerezani.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa msamaha kwa wafungwa 1,548 waliopo katika magereza mbalimbali nchini kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 63 ya uhuru wa Tanzania ambayo huadhimishwa kila ifikapo Desemba 9 kila mwaka.

Taarifa iliyotolewa na Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Daniel Sillo leo Desemba 9, 2024 imebainisha kuwa kati ya wafungwa waliopewa msamaha 22 wanaachiwa huru leo na 1,526 wanabaki gerezani kumalizia sehemu ya kifungo kilichobaki baada ya kupewa msamaha.

Masharti ya msamaha

Uamuzi huo umetokana na mamlaka aliyopewa Rais wa Tanzania chini ya Ibara ya 45(1)(a) (d) ya Katiba ya Tanzania kutoa msamaha kwa wafungwa kwa masharti mbalimbali ambapo wafungwa wenye sifa mbalimbali wamepunguziwa robo ya adhabu zao wanazozitumikia hivi sasa baada ya kutoa punguzo la kawaida la moja ya tatu (1/3) linalotolewa chini ya Kifungu cha 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58. 

Wafungwa hao ni wale waliohukumiwa adhabu ya kifungo cha kuanzia miaka miwili (2) na kuendelea ambao wametumikia robo ¼ ya adhabu zao gerezani na walioingia gerezani kabla ya tarehe 19 Oktoba, 2024

Taarifa hiyo imebainisha kuwa wafungwa wengine walionufaika ni wagonjwa wenye magonjwa ya kudumu au sugu ambao wapo kwenye hatua ya mwisho “terminal stage” ambao ugonjwa na hatua hiyo vimethibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

Aidha, wafungwa wote waliotumikia kifungo cha maisha gerezani bila kujali kosa ambao wametumikia adhabu zao kwa miaka kumi na tano (15) na kuendelea wamebadilishiwa adhabu zao kuwa kifungo cha miaka thelathini (30) kuanzia tarehe ya hukumu.

“Wafungwa waliobadilishiwa adhabu kwa msamaha wa Rais wa Tanzania kutoka adhabu ya kifo na kuwa kifungo cha maisha ambao wametimiza miaka 10 na kuendelea tangu kupata msamaha huo, wamebadilishiwa kifungo cha maisha kuwa kifungo cha miaka 30 gerezani.

Wanufaika wengine wa msamaha ni wafungwa wazee wenye umri wa miaka 70 au zaidi, ambao umri huo umethibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa mganga mkuu wa mkoa/mganga mkuu wa wilaya,” inasomeka sehemu ya taarifa ya Sillo.

Wafungwa hao kipengele cha kutumikia robo ya adhabu zao hakitawahusu na makosa yao yawe ni yenye sifa ya kunufaika;

Wengine ni wafungwa wa kike walioingia na ujauzito gerezani au wenye watoto wanaonyonya, wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili wasio na uwezo wa kufanya kazi ambao ulemavu huo umethibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa mganga mkuu wa mkoa/mganga mkuu wa wilaya pamoja na wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kuwekwa kizuizini (under presidential pleasure) ambao wamekaa gerezani kuanzia miaka kumi au zaidi.

Wafuatao kutonufaika na msamaha

Hata hivyo, msamaha huo hautawahusu wafungwa wanaotumikia vifungo vya nje na wale waliowahi kukiuka masharti chini ya Sheria ya Bodi za Parole Sura ya 400 (R.E 2002), na kurudishwa gerezani kutumikia adhabu zao, Sheria ya Huduma kwa Jamii Sura ya 291 (R.E 2002) na Kanuni za kifungo cha Nje [The Prisons (Extra Mural Penal Employment) Regulations, 1968.

Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo gerezani ambacho siyo cha maisha kwa makosa ya uhujumu uchumi, matumizi mabaya ya madaraka, utakatishaji wa fedha, rushwa na usafirishaji au kujihusisha kwa namna yoyote ile na madawa ya kulevya ikiwemo bangi.

Wengine ni wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo gerezani ambacho siyo cha maisha kwa makosa ya kujamiiana, utekaji au wizi wa watoto, kupoka, kuwapa mimba wanafunzi au makosa yoyote yale yanayohusiana na ukatili dhidi ya watoto na kujihusisha kwa namna yoyote ile na biashara haramu ya binadamu;

Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo gerezani ambacho siyo cha maisha kwa makosa ya kukutwa na viungo vya binadamu, unyang’anyi, unyang’anyi wa kutumia nguvu, unyang’anyi wa kutumia silaha, kumiliki silaha, risasi, milipuko au kujaribu kutenda makosa hayo

“Wafungwa wanaotumikia kifungo gerezani ambacho siyo cha maisha kwa makosa ya kujihusisha kwa namna yoyote ile na nyara za Serikali au ujangili, wafungwa wanaotumikia kifungo gerezani ambacho siyo cha maisha kwa makosa ya wizi au ubadhilifu wa fedha za Serikali, waliohukumiwa adhabu ya kifo, wanaotumikia vifungo gerezani kwa makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi halali au kusaidia kutendeka kwa makosa hayo,” imebainisha taarifa hiyo.

Vilevile, wafungwa wenye makosa ya kujaribu kuua, kujaribu kujiua au kuua watoto wachanga, ugaidi, uharamia na makosa ya kimtandao (Attempt to Murder, Attempt Suicide, Infanticide, Terrorism, Piracy and Cyber Crimes nao hawatanufaika na msamaha wa Rais.

Hata hivyo, Sillo amesisitiza wafungwa wanufaika wa msamaha huo kurejea tena katika jamii kushirikiana na wananchi wenzao katika ujenzi wa Taifa  na kujiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani.

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
15 Jun, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
15 Jun, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
15 Jun, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Mwenendo wa deni la serikali

Mwenendo wa deni la serikali

Nukta TV

Rais Samia: Uchumi wa nchi unapanda , lakini ukifika kwa watu hali si nzuri

Rais Samia: Uchumi wa nchi unapanda , lakini ukifika kwa watu hali si nzuri

Nukta TV

Gavana Tutuba afichua kiasi cha dhahabu kilichopo BoT thamani yake

Gavana Tutuba afichua kiasi cha dhahabu kilichopo BoT thamani yake

Nukta TV