Rais Samia ateua Mwenyekiti mpya wa Tume ya Uchaguzi
- Ni Jaji Jacob Casthom Mwambegele.
- Ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mjumbe wa NEC.
- Anachukua nafasi ya Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Semistocles Kaijage.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Jaji Jacob Casthom Mwambegele kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Jaji Mwambegele ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mjumbe wa NEC anachukua nafasi ya Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Semistocles Kaijage ambaye amemaliza muda wake.
Jaji Kaijage aliteuliwa kuongoza tume hiyo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Desemba 20, 2016 akichukua nafasi ya Jaji Mstaafu Damiani Lubuva.
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Jaffar Haniu katika taarifa yake iliyotolewa leo Desemba 27, 2021 amesema pia Rais amefanya uteuzi wa viongozi wengine akiwemo Jaji Mwanaisha Athuman Kwariko kuwa mjumbe wa Tume hiyo.
Jaji Kwariko anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Jacob Casthom Mwambegele.
Aidha, Rais Samia amemteua Jaji Sam Mpaya Rumanyika, kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.
Profesa Khamis Dihenga ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).
Kabla ya uteuzi huo Profesa Dihenga alikuwa anahudumu kwa mkataba katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) mkoani Morogoro.
Profesa Dihenga anachukua nafasi ya Profesa William Anangisye aliyemaliza muda wake.
Soma zaidi:
-
Tanzania yashauriwa kutafakari upya kurejea mahakama ya Afrika
-
Mahakama Tanzania ni mwendo wa kidijitali utoaji wa huduma
Rais Samia pia amemteua Mhadhiri Mwandamizi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Mussa Muhidin Kissaka kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).
“Uteuzi huo umeanza 23 Desemba, 2021,” imeeleza taarifa ya Haniu.
Rais Samia awasamehe wafungwa 5,704
Rais wa Tanzania, Samia ametoa msamaha kwa wafungwa 5,704 katika kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene amesema Rais Samia ametoa msamaha huo kwa masharti ikiwa ni pamoja na wafungwa hao wawe wametumikia robo ya adhabu zao gerezani na wawe wameingia kabla ya Oktoba 9, 2021.
Latest
