Dangote afungua milango umiliki kiwanda cha mafuta, hisa kuanzia Sh10,508
- Mwekezaji anaweza kuanza kununua hisa 10 kwa gharama ya naira 5,250 ambayo ni karibu Sh10,508, uuzaji wa hisa hizo ukitarajiwa kuanza Septemba 14 na kufungwa Oktoba 13, 2026 katika Soko la Hisa la Nigeria (NGX).
Dar es Salaam. Mfanyabiashara wa Nigeria, Aliko Dangote, amefungua rasmi fursa kwa wawekezaji kumiliki sehemu ya kiwanda chake cha kusafisha mafuta kupitia uuzaji wa hisa kwa umma, hatua inayolenga kukusanya zaidi ya Dola za Marekani bilioni 1.6 kwa ajili ya upanuzi wa biashara hiyo.
Dangote Petroleum Refinery, iliyopo katika mji wa Lekki nchini Nigeria, imetangaza kuuza hisa bilioni 4.1 kwa bei ya naira 525 kwa hisa moja, sawa na takribani Dola za Marekani 0.40 au takriban Sh1,060.
Kwa bei hiyo, mwekezaji anaweza kuanza kununua hisa 10 kwa gharama ya naira 5,250 ambayo ni karibu Sh10,508, huku uuzaji wa hisa hizo ukitarajiwa kuanza Septemba 14 na kufungwa Oktoba 13, 2026 katika Soko la Hisa la Nigeria (NGX).
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na kampuni hiyo, mpango huo ni sehemu ya uuzaji wa hisa za kampuni kwa umma kwa mara ya kwanza (IPO), unaotarajiwa kuwa miongoni mwa mauzo makubwa zaidi ya hisa kuwahi kufanyika barani Afrika.
Shirika la habari la kimataifa Reuters limeeleza kuwa IPO hiyo imelenga kukusanya takribani naira trilioni 2.15, sawa na karibu Dola za Marekani bilioni 1.6 (zaidi ya Sh4.24 trilioni).
Fedha zitakazopatikana zinatarajiwa kusaidia mipango ya Dangote kuongeza uwezo wa kiwanda hicho kutoka takribani mapipa 650,000 kwa siku hadi mapipa milioni 1.4 kwa siku ifikapo mwaka 2029.
Kiwanda hicho kilichogharimu zaidi ya Dola za Marekani bilioni 20 kilianza uzalishaji mwaka 2024 na sasa ni miongoni mwa miradi mikubwa zaidi ya nishati barani Afrika.
Kwa mujibu wa Dangote mpango huo unalenga kuwapa Waafrika nafasi ya kumiliki sehemu ya biashara kubwa ya nishati barani humo ukiwalenga zaidi wawekezaji wadogo wakiwemo wafanyakazi wa kawaida kuwa wanahisa wa kiwanda hicho.
Kutoka Tanga hadi Kenya
Hatua hii ya Dangote inakuja wakati ambapo mfanyabiashara huyo pia anaendelea kupanua uwekezaji wake katika sekta ya mafuta nje ya Nigeria, ikiwemo mpango wa kujenga kiwanda kingine kikubwa cha kusafisha mafuta Afrika Mashariki.
Hata hivyo, safari ya mradi huo imepitia mabadiliko ya eneo.
Awali, Tanzania ilikuwa miongoni mwa maeneo yaliyotajwa kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho, huku Tanga ikitajwa kama eneo ambalo lingetumika kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta kwa ajili ya kuhudumia Tanzania na nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Mnamo Aprili 2026, Rais wa Kenya William Ruto alisema nchi za Afrika Mashariki zilikuwa zikijadili uwezekano wa kujenga kiwanda cha pamoja cha kusafisha mafuta huko Tanga, ambacho kingetumia mafuta ghafi kutoka Uganda, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na nchi nyingine za ukanda huo.
Lakini baadaye Dangote alielekeza zaidi uwekezaji huo nchini Kenya, akitaja Mombasa kama eneo lenye faida zaidi kutokana na ukubwa na kina cha bandari yake pamoja na ukubwa wa soko la mafuta nchini Kenya.
Taarifa za baadaye kutoka kampuni ya Dangote zilithibitisha kuwa mradi huo sasa unaelekea kujengwa katika pwani ya Kenya, huku eneo la Lamu likitajwa kama eneo la mradi huo wa kiwanda chenye uwezo wa kuchakata takribani mapipa 700,000 ya mafuta kwa siku.
Mradi huo unakadiriwa kugharimu kati ya Dola za Marekani bilioni 15 na 17 na unalenga kupunguza utegemezi wa Afrika Mashariki kwa mafuta yaliyosafishwa kutoka nje ya bara hilo.