Rais Samia akutana na Kagame, wakubaliana haya
- Wakubaliana kukuza biashara baina ya Tanzania na Rwanda.
- Kuimarisha mawasiliano na kudumisha amani Afrika Mashariki.
- Kuendeleza miradi ya kimkakati
Dar es Salaam. Tanzania na Rwanda zimefungua ukurasa mpya wa kidiplomasia na biashara baada ya marais wa nchi hizo mbili kukutana leo na kukubaliana baadhi ya mambo ikiwemo kuweka miundombinu itakayochochea ukuaji wa uchumi.
Makubaliano hayo yamefikiwa leo Aprili 27, 2023 baada ya Rais Samia Suluhu Hassan na Paul Kagame, Rais wa Rwanda kukutana Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais Samia akiongea na vyombo vya habari mara baada ya mazungumzo hayo amesema ziara hiyo siku mbili ya Rais Kagame imewezesha nchi hizo kuzungumza masuala mbalimbali ikiwemo biashara.
“Tumeona haja ya kukuza biashara na kuweka miundombinu ya kuweka biashara kwa sababu kiwango cha biashara tulichonacho hakiendani na rasilimali tulizonazo kwa nchi mbili (Tanzania na Rwanda) lakini na uhusiano mzuri uliopo,” amesema Rais Samia.
Katika kukuza biashara, Rais Samia amesema Tanzania ipo kwenye mchakato wa kuimarisha bandari hususani bandari za Dar es Salaam na Tanga ambazo ndizo zinatumiwa zaidi na nchi ya Rwanda.
Rwanda ni moja kati ya nchi za Afrika Mashariki zisizokuwa na bandari, hivyo kulazimika kutoa na kuingiza bidhaa kupitia bandari mbalimbali za nchi jirani zikiwemo bandari za Dar es Salaam na Tanga.
Soma zaidi
-
Fursa zilizojificha utalii wa milimani
-
Bajeti Wizara ya Madini yaongezeka, miradi ya maendeleo ikisuasua
Kuimarishwa kwa bandari zilizopo nchini kutaiwezesha nchi hiyo inayoongoza kwa kusafirisha madini ya Tungsten mwaka 2021 kukuza uchumi wake.
Sambamba na mambo hayo maraisi hao pia walijadili maendeleo ya mradi wa umeme wa maji wa Rusumo utakaozalisha megawati 80 unaojengwa wilayani Ngara, mkoani Kagera.
Mradi huo unaojengwa kwa ushirikiano wa nchi tatu za Rwanda, Tanzania na Burundi ambapo kila nchi itapata megawati 27.
Pia wamegusia masuala ya ulinzi na usalama huku wakiagiza vyombo vya usalama vya nchi hizo mbili kufanya kazi kwa pamoja kuleta amani katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa upande wake Rais Paul Kagame amesema wamekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kihistoria kati ya Tanzania na Rwanda.
“Ushirikiano huu utaziwezesha nchi zetu kushindana kwenye soko la dunia,” amesema Kagame.
Ameongeza kuwa makubaliano hayo yatawawezesha kutengeneza mazingira mazuri kwa ajili ya vijana wajasiriamali waliopo kwenye nchi zote.
Pamoja na hayo kiongozi huyo wa Rwanda ameishukuru nchi ya Tanzania kwa kuendelea kutunza amani na kusuluhisha migogoro ndani ya nchi za Afrika Mashariki.
“Mwisho kabisa nikushukuru (Rais Samia) kwa kutafuta suluhu ya kudumu ndani ya nchi zetu hususani Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo kwa kushirikiana na nchi nyingine za Afrika Mashariki,”
Latest