Bajeti Wizara ya Madini yaongezeka, miradi ya maendeleo ikisuasua

April 27, 2023 12:05 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Imeongezeka kwa asilimia 7.08 hadi Sh89.3 bilioni kwa mwaka 2023/24.
  • Utekelezaji wa bajeti ya miradi ya maendeleo kwa mwaka 2022/23 umekuwa chini ya malengo.
  • Wizara imepokea asilimia 20.9 ya fedha za maendeleo zilizoidhinishwa hadi Machi mwaka huu. 

Dar es Salaam. Licha ya bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka 2023/24 kutarajiwa kuongezeka kwa asilimia 7.08, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeeleza kuwa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika wizara hiyo hazitolewi kwa wakati jambo linalosababisha miradi iliyopangwa kutokamilika kikamilifu.  

Waziri wa wizara hiyo, Dk Doto Biteko aliyekuwa akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka ujao wa 2023/24 leo Aprili 27 bungeni jijini Dodoma amewaomba Wabunge waidhinishe Sh89.3 bilioni kwa ajili matumizi ya kawaida na maendeleo.

Kati ya fedha hizo, Sh23.2 bilioni ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo, Sh20.3 bilioni (mishahara ya watumishi wizara) na Sh45.8 ni kwa ajili ya matumizi ya mengineyo. 

Waziri Biteko amesema katika mwaka ujao wizara yake itakuwa na vipaumbele sita muhimu vya kutekeleza ikiwemo uendelezaji madini muhimu na kimkakati kwenda sambamba na mahitaji ya sasa ya dunia yatakapokuwa yanahitajika kwa kiasi kikubwa katika vifaa vya kielektroniki.

Pia uanzishwaji wa maonyesho ya madini ya vito kwa lengo la kuinua biashara ya madini ya vito hapa nchini na kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli na kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa.

Waziri huyo amesema watawaendeleza wachimbaji wadogo na kuwawezesha wananchi kushiriki katika uchumi wa madini, kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini, kuhamasisha biashara na uwekezaji katika sekta ya madini.

Kusimamia mfumo wa ukaguzi wa shughuli za migodi, kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya wizara ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi na kuendeleza rasilimali watu na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi, ni miongoni mwa kazi muhimu za wizara.


Soma zaidi:  


Bajeti yaongezeka lakini…

Bajeti ya Wizara ya Madini kwa mwaka 2023/24 imeongezeka kwa asilimia 7.08 kutoka Sh83.4 bilioni ya mwaka 2022/23. 

Licha ya kuongezeka kwa bajeti hiyo, hadi kufikia Machi 2023, Wizara imepokea jumla ya Sh47.8 bilioni sawa na asilimia 57.3 ya bajeti yote iliyoidhinishwa ikiwa imebaki miezi miwili mwaka wa bajeti uishe.

Kati ya fedha hizo zilizopokelewa, Sh4.6 bilioni ndiyo zilipelekwa kushughulikia miradi ya maendeleo. 

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Judith Kapinga akitoa maoni ya kamati yake amesema utekelezaji wa bajeti ya miradi ya maendeleo kwa mwaka 2022/23 umekuwa chini ya malengo hususan mradi wa ujenzi wa jengo la Kituo cha Jiomolojia Tanzania (TGC).

“Ni vyema tathmini ya uhakika ikafanyika kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi hii ili kuwezesha kukamilika kwa wakati bila kuchelewa,” amesema Kapinga.

Uchambuzi wa kamati hiyo unaonyesha miradi ya maendeleo imepokea asilimia 20.9 tu ya fedha zilizoidhinishwa.

“Kamati inatoa raia kwa wakandarasi kutekeleza kazi kwa wakati na kuwasilisha hati za madai mapema ili kulipwa. Mapungufu yote yaliyojitokeza katika miradi ya maendeleo yafanyiwe kazi ili kuwezesha utekelezaji bora wa miradi kwa maendeleo ya sekta ya madini na kwa uchumi wa Taifa,” amesisitiza. 

Pamoja na bajeti ya Serikali kwa mwaka 2023/24 kuongezeka kwa asilimia 7 ikilinganishwa na mwaka huu, asilimia ya bajeti ya Wizara ya Madini dhidi ya bajeti ya Taifa imebaki kuwa ni ileile ya mwaka uliopita ambayo ni asilimia 0.20

“Kamati imeona umuhimu wa kuongeza bajeti ya wizara ambayo ina mchango mkubwa kwa Taifa ambayo pia inakabiliwa na changamoto nyingi katika taasisi zake ambazo zinazochangia katika pato la Taifa,” amesema Kapinga. 

Enable Notifications OK No thanks