Rais asema wapinzani siyo maadui akiwatambua bodaboda
- Asema wanatofautiana kwa mawazo tu lakini siyo maadui.
- Ataja alivyorahisisha Lema kurudi Tanzania.
- Asisitiza kuwatambua madereva wa bodaboda.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema kwa sasa hali ya kisiasa Tanzania imeimarika na hawachukulii wapinzani kama maadui bali hutumia mawazo yao kuboresha changamoto wanazoibua huku akisema anawatambua madereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda.
Rais Samia aliyekuwa akiwasalimia wakazi wa mji wa Usa River mkoani Arusha leo Machi 5, 2023 amesema kitendo cha mwanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Godbless Lema aliyekuwa uhamishoni nchini Canada kurejea nchini kinadhihirisha kuwa siasa za Tanzania kwa sasa ni imara.
“Kwenye siasa na kwenyewe tuko vizuri. Nadhani lile tendo la juzi kwa mtu wao wa kanda hii (Lema) kurudi nchini na hakuna kilichotokea inaonyesha siasa zetu ziko imara sana,” amesema Rais Samia.
Amesema kilichobaki sasa hata baada ya Lema kurudi nchini ni kuimarisha siasa za ushindani.
“Kwa hiyo mdogo wangu amerudi ameniambia mama nataka kurudi nikamwambia rudi. Kasema mama nina kesi nikasema nazifuta. Amerudi tunaimarisha siasa si ndiyo? Mwanaume ni yule anayejiamini, mwanamke ni yule anayejiamini,” amesema Rais.
Kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema kutokana na hali hiyo Watanzania wote ni wamoja licha ya kuwa wana mawazo tofauti, hivyo anawachukulia wapinzani kama watu wanaompa changamoto ya kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) anachokiongoza.
“Mtanzania yoyote awe wa chama chochote cha siasa tunachotofautiana ni mawazo na fikra lakini pia lakini siwachukulii wapinzani kama maadui nawachukulia kama watu watakaonionyesha changamoto zilipo nizitekeleze ili CCM iimarike,” amesema Rais Samia huku akishangiliwa na wananchi waliojitokeza kumsikiliza.
Lema aliyekimbilia Canada baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 aliibua mjadala mpana kwenye jamii na mitandao ya kijamii baada ya kusema kazi wanayofanya madereva wa bodaboda ni kama ya “laana” kwa sababu inawaweka katika hatari kupata magonjwa, majeraha, ulemavu na vifo kutokana na ajali za barabarani.
Kauli hiyo ya Lema ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Arusha Mjini alitoa kauli hiyo Machi 1, 2023 muda mfupi baada ya kuwasili nchini, iliwaibua watu mbalimbali wakiwemo wanasiasa huku baadhi yao wakisema imejaa dharau kwa kundi hilo muhimu kwenye jamii kwa sababu imetoa ajira kwa maelfu ya vijana nchini.
Baadhi ya watu wameunga mkono kauli hiyo na kusema bodaboda isichukuliwe kama ajira rasmi kwa vijana bali wawekewe mazingira wezeshi ya kujiajiri hasa katika sekta ya kilimo ili kuwaepusha na athari za kutumia vyombo hivyo vya moto.
Wakati mjadala huo ukiendelea, naye Rais Samia amegusia kwa sehemu suala hilo huku akisema anawatambua bodaboda kwa kazi wanayofanya.
“Nawashukuru watoto wangu wa bodaboda, wamenisindikiza kutoka mjini mpaka hapa (Usa River) mwendo ni ule ule mpaka 2025 wanangu, nawatambua,” amesema Rais Samia wakati akiwaaga wakazi wa Usar River.
Maafisa Usafirishaji (Bodaboda) wakiwa wameshika Mabango wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Usa River Mkoani Arusha tarehe 05 Machi, 2023. pic.twitter.com/tXydClhsmM
— ikulu_Tanzania (@ikulumawasliano) March 5, 2023
Latest
