Rais Magufuli kuwaachia huru wafungwa 1,415 wa Ethiopia
- Asema wameanza mazungumzo kuwarejesha katika nchi yao.
- Watakaorejeshwa ni pamoja na wale wenye matatizo ya uraia.
- Asema hatua hiyo itasaidia kupunguza idadi ya wafungwa magerezani.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema Serikali inafanya mazungumzo na nchi mbalimbali ili kuwarejesha katika mataifa yao wafungwa wa kigeni wakiwemo Waethiopia 1,415 ili kupunguza idadi ya wafungwa waliopo katika magereza ya Tanzania.
Dk Magufuli aliyekuwa akizungumza leo (Februari 6, 2020) katika maadhimisho ya Siku Ya Sheria jijini Dar es Salaam, amesema wafungwa hao watakaorejeshwa katika nchi zao ni pamoja na wale wenye matatizo ya uraia.
“Aidha, tunaendelea na majadiliano ya kuwarejesha makwao raia wa kigeni wakiwepo Waethiopia 1,415 ambao wamefungwa katika magereza yetu kutokana na matatizo ya immigration (uhamiaji).
“Na tunafanya mazungumzo na nafikiri hati zenyewe nitazisaini mapema ndani ya siku mbili tatu ili hawa wafungwa kutoka nchi ya Ethiopia waweze kurudishwa kwao,” amesema Rais Magufuli.
Soma zaidi:
- Magufuli aagiza zoezi la kuwaachia mahabusi wanaoshikiliwa kimakosa lifanyike nchi nzima
- Magufuli aagiza watuhumiwa uhujumu uchumi walio tayari kutubu waachiwe.
- DPP aanza kuwaachia huru watuhumiwa wa uhujumu uchumi
Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza idadi ya mahabusu ambao wanashinda mahakamani kutokana na kuchelewa kwa mashauri na upelelezi wa kesi zao.
“Na hii itatusaidia Serikali kutupunguzia idadi ya wafungwa wanaokaa mahakamani, kwa sababu kwa taarifa tulizonazo wafungwa ni wachache kuliko walioko mahabusu,” amesema Rais.
Amesema tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, imeendelea na juhudi za kuboresha magereza na kupunguza idadi ya wafungwa na mahabusu ili kuharakisha mchakato wa upatikanaji wa haki.
Amebainisha kuwa jumla ya washtakiwa 335 waliokiri makosa yaani “pre bargain” kwa Mwendesha Mashtaka (DDP) wamepata msamaha na kutoka magerezani.
“Magereza yetu hivi sasa yanahudumia watu wapatao 32,208 ambapo wafungwa ni 13,455 na mahabusu ni 17,632. Hii inadhihirisha kuwa tatizo la ucheleweshaji kesi bado lipo na hili linawahusu zaidi wapelelezaji,” amesisitiza Rais.
Latest