Magufuli aagiza watuhumiwa uhujumu uchumi walio tayari kutubu waachiwe

Mwandishi Wetu 0922Hrs   Septemba 22, 2019 Habari
  • Amemwagiza DPP kuwasikiliza watuhumiwa ili ambao wako tayari kutubu na kulipa fedha waachiwe huru. 
  • Amesema anawaonea huruma kama anavyoonea wafungwa wengine nchini.
  • Makosa ya uhujumu hayana dhamana nchini Tanzania.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amemuagiza Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP), Biswalo Mganga kwenda kuwasikiliza watuhumiwa wa makosa ya uhujumu uchumi waliopo rumande ili ambao wako tayari kutubu na kulipa fedha waweze kuachiwa huru.

Rais Magufuli aliyekuwa akizungumza leo (Septemba 22, 2019) Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali wa aliowateua, amesema wapo watu wamekaa ndani kwa kesi za uhujumu uchumi kwa muda mrefu wengine wana miaka mitatu na  anawahurumia sana kama ambavyo anawahurumia wengine.

Amesema iwapo watu hao wako tayari kulipa fedha wakiwemo waliotakatisha fedha, kukwepa kodi na kukiri kutorudia makosa wasamehewe waliyotenda na kuachiliwa huru ili waendelee na shughuli zao. 

“Kuanzia Jumatatu (Septemba 23, 2019) hadi siku ya Jumamosi ya wiki inayokuja, kama wako watu wa namna hiyo ambao wako mahabusu kwa sababu ya kesi za uhujumu uchumi ambazo zitawafanya wasitoke mapema kwa mujibu wa sheria yetu lakini wako radhi kurudisha zile fedha na kutubu kwamba hawatarudia, mimi ningeshauri watu wa namna hiyo kama sheria inaruhusu, DPP wakatoke humo ndani,” amesema Rais Magufuli.


Soma zaidi: Magufuli aagiza zoezi la kuwaachia mahabusi wanaoshikiliwa kimakosa lifanyike nchi nzima


Amemtaka DPP kutengeneza mazingira ya watu hao kurudisha fedha hizo za umma kwa kupanga utaratibu mzuri utakaofanikisha kupatikana hizo fedha.

Hata hivyo, amesema kwa wale watakaokaidi agizo hilo, wataendelea kukaa mahabusu mpaka kesi zao zikamilike hata kama itachukua muda mrefu.

 “Lakini wasipofanya hivyo ndani ya siku saba, nyinyi muendelee kuwabana kisawa sawa hata kama kesi itachukua miaka 20. Lakini nilifikiri kama kiongozi nina wajibu wa kusamehe ili tulijenge Taifa letu kwa pamoja,” amesema Dk Magufuli. 

Rais Magufuli amefikia hatua hiyo, baada ya kusema kuwa Mkuu wa Magereza nchini, Kamishana Jenerali Phaustine Kasike, alimuomba aajiri askari magereza 800 lakini alikataa kwa sababu hataki wafungwa waongezeke magerezani.

Hii ni mara ya pili kwa Rais Magufuli kumuagiza DPP kuwasikiliza na kuwaachia huru watuhumiwa waliopo mahabusu ambao hawakutendewa haki. 

Julai 18, 2019 akiwa mkoani Mwanza, Rais John Magufuli aliiagiza Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP) kutembelea mahabusi na magereza katika mikoa yote ya Tanzania ili kubaini na kuwaachilia huru watuhumiwa wa makosa mbalimbali ambao hawajatendewa haki.

Agizo hilo la Rais alilitoa baada ya watuhumiwa zaidi ya 70 wakiwemo askari polisi wanane walioshitakiwa kwa usafirishaji wa shehena ya dhahabu kuachiwa huru kutoka katika Gereza Kuu la Butimba jijini Mwanza.

Related Post