Miradi ya uwekezaji 537 itakavyoboresha maisha Tanzania

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Aprili 20, 2023 amehudhuria hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo cha Kibiashara cha Afrika Mashariki, katika eneo la Ubungo ambacho kinajengwa na Kampuni ya East Africa Commercial and Logistics Center ya nchini China. Picha | Ofisi ya Waziri Mkuu.
- Kati ya mwaka 2021 hadi Januari, 2023 Serikali imesajili jumla ya miradi ya uwekezaji 537.
- Miradi hiyo inatarajia kutoa ajira takriban 92,770.
- Waziri Mkuu awaita wawekezaji kuwekeza Tanzania.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa katika kipindi cha mwaka 2021 hadi Januari, 2023 Serikali imesajili jumla ya miradi ya uwekezaji 537 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 7,222 sawa na Sh16.9 trilioni, jambo litakalofungua fursa mbalimbali ikiwemo ajira.
Amesema kuwa, hatua hiyo imetokana na kuboreshwa kwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na kuimarisha Kituo cha Huduma za Mahala Pamoja ili kuvutia wawekezaji kwa kupunguza kero na kurahisisha utoaji huduma.
Ongezeko la usajili wa miradi hiyo unatarajia kutoa ajira takriban 92,770
“Kiwango hiki ni kikubwa kuwahi kuandikishwa katika kipindi chochote tangu nchi yetu ilipopata uhuru mwaka 1961,” amesema leo (Aprili 20, 2023) alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa Kituo cha Biashara cha Afrika Mashariki, kinachojengwa na Kampuni ya East Africa Commercial and Logistics Center Ubungo jijini Dar es Salaam.
Pia Serikali kupitia Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Mauzo ya Nje (EPZA) imefanikiwa kusajili Miradi 38 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 139.70 (Sh727.8 bilioni) na mauzo nje yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 191.04 (Sh448.3 bilioni)
“Miradi hiyo ni mahsusi katika sekta zinazozalisha bidhaa zitokanazo na Kilimo, bidhaa za viwandani, bidhaa za mifugo, bidhaa za Kemikali, bidhaa za madini na bidhaa za misitu,” amesema Majaliwa.
Ametoa wito kwa wawekezaji kuja kuwekeza Tanzania kwani ni sehemu sahihi ya uwekezaji, na kuleta mitaji yao.
“Wizara yenye dhamana ya uwekezaji hakikisheni mnaendelea kuratibu vema sekta ya uwekezaji ili nchi yetu iweze kunufaika na uwekezaji nchini,” amesema.

Latest