PSPTB yatakiwa kudhibiti rushwa sekta ya manunuzi, ugavi

Baadhi ya Washiriki wa Kongamano la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPSTB), wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi, Kaimu Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Richard Mkumbo wakati akifunga Kongamano la Tisa la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), katika ukumbi wa DCC, Jijini Dodoma.
- Pia imetakiwa kuhakikisha inadhibiti maadili ya wafanyakazi wa sekta ya ununuzi na ugavi ili fedha za serikali zinazotumika kwenye ununuzi ziwe na tija kwa wananchi.
- Yabainika kuwa asilimia 75 ya fedha za umma zinazotumika kupitia mchakato wa manunuzi zina viashiria vya rushwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya wananchi.
Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Susana Mkapa ameiagiza Bodi ya wataalam wa ununuzi na ugavi nchini (PSPTB), kuhakikisha inadhibiti maadili ya wafanyakazi wa sekta ya ununuzi na ugavi ili fedha za serikali zinazotumika kwenye ununuzi ziwe na tija kwa wananchi.
Ametoa maagizo hayo Jijini Dodoma, katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Kaimu Naibu Katibu Mkuu ambaye pia ni Mkurugenzi wa mipango wa Wizara ya Fedha na Mipango, Richard Mkumbo, wakati akifunga kongamano la tisa la wataalam wa ununuzi na ugavi kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kitengo cha mawasiliano wizarani hapo, Mkumbo amebainisha kuwa licha ya vitendo vya matumizi mabaya ya fedha za umma kupitia sekta ya ununuzi na ugavi, ikiwemo rushwa kuendelea kupungua, Bodi inatakiwa kuhakikisha kuwa vitendo vya rushwa vinadhibitiwa ipasavyo.
Amesema asilimia 75 ya fedha za umma zinatumika kupitia mchakato wa manunuzi ambao taarifa ya mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za serikali (CAG) na Mamlaka ya Ununuzi nchini PPRA zimebaini kuwepo kwa viashiria vya rushwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya wananchi.
Zinazohusiana:
- Sekta ya manunuzi kuboresha mfumo wa utoaji taarifa kwa umma
- Nsekela ateuliwa kurithi mikoba ya Dk Kimei
- BOT yashusha riba tena kwa benki za biashara Tanzania
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa PSPTB, Dk Hellen Bandiho, amesema kuwa Bodi yake itahakikisha inasimamia kikamilifu maadili ya watumishi wa sekta ya ununuzi ili iweze kushiriki katika kukuza uchumi wa viwanda.
Kongamano hilo limewashirikisha wataalam wa ununuzi na ugavi wapatao 650 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara.