Mapya yaibuka askari anayedaiwa kumvunja raia miguu kisa mapenzi
- Ni Mohamed Khatibu aliyeshambuliwa kwa madai ya kutembea na mke wa askari mkoani Mwanza.
- Mtuhumiwa aliyemshambuliwa afikishwa mahakani.
- Mke wa mtuhumiwa amkana Mohamed.
Mwanza. Ikiwa zimepita wiki mbili tangu Mohamed Khatibu, mkazi wa jijini Mwanza kushambuliwa kwa kipigo na Mkuu wa Kituo Kidogo cha Polisi Kiseke kwa madai ya kutoka mapenzi mzazi mwenzake, mke wa askari huyo amejitokeza na kukana tuhuma hizo.
Januari 3, mwaka huu askari huyo aliyetambulika kwa jina la Paulo anadaiwa kumkamata Mohamed akiwa nyumbani kwao Mtaa wa Mlimani A eneo la Kirumba wilayani Ilemela akishirikiana na rafiki yake.
Baada ya kumkamata Mohamed na kumpiga pingu mikononi, askari huyo aliyekuwa akitumia gari binafsi alidaiwa kuondoka naye kumpeleka Kituo cha Polisi Kirumba ambako ndugu walipofuatilia hawakumkuta, kwa kuwa alipelekwa Kituo Kidogo cha Kiseke.
Ilidaiwa kuwa alipofikishwa kituoni hapo, Mohamed alishushiwa kipigo kabla ya kuingizwa mahabusu bila taarifa zake kurekodiwa.
Wakati Paulo akiendelea kushikiriwa na polisi kwa ajili ya uchunguzi , Nukta Habari (www.nukta.co.tz) imefanikiwa kumpata mwanamke anayedaiwa kusababisha tukio hilo ambaye anadaiwa kuwa mzazi mwenzake wa aksari huyo.
Mwanamke huyo, Doreen Edward amekana kutoka kimahusiano na Mohamed na kusema yeye ni mke halali wa Paulo kinyume na madai yanayotolewa na watu.
Doreen amesema hajawahi kuwa na mahusiano na Mohamed badala yake alikuwa akilazimishwa ili aweze kulipiza kisasi kwa askari huyo.
Doreen ameiambia Nukta habari kuwa anakumbuka siku ya Disemba 31 mwaka jana, akiwa njiani kuelekea nyumbaniakitokea kwa rafiki yake, Mohamed akiwa na wenzake anaodai kuwa ni vibaka walimkamata kwa nguvu na kumpandisha kwenye bodaboda kisha kumpeleka eneo la Ghana ambapo walifanikiwa kumuibia pochi yake na fedha.
“Kitendo hicho kilinifanya nikaripoti Polisi lakini hakuna hatua zilizochukuliwa hadi pale nilipomweleza mume wangu,” amesema Doreen.
Anaomba msaada wa kisheria na watetezi wa haki za wanawake kwa sababu heshima yake kwenye jamii amechafuliwa kwa kutajwa kuwa anatoka kimapenzi na mwanaume mwingine.
Alipoulizwa iwapo tuhuma za Mohamed kuwa hakuwa ameolewa alikana, na kueleza kuwa hakuwahi kuzungumza naye chochote isipokuwa alikuwa akimlazimisha kutoka naye kwa nguvu.
Mohamed Khatibu akiwa akiwa kindani baada ya kudai kupigwa na polisi na kusababisha kuvunjwa miguu kwa wivu wa mapenzi. Picha | Mariam John.
“Mtuhumiwa abadilishiwa kosa”
Taarifa za ndani ilizopata Nukta Habari zimebainisha kuwa kwa sasa mtuhumiwa huyo, afande Paulo amebadilishiwa kosa kutoka kosa la kushambulia hadi kosa la kutumia silaha za Serikali kwa matumizi binafsi.
Kwa sasa taratibu zinafanyika ili mtuhumiwa afikishwe mahakamani kwa kosa hilo.
“Tunapambana kuhakikisha kesi anayotaka kubadilishiwa nayo isitokee kwani haina mdhamana hivyo leo au kesho atapandishwa mahakamani na huenda akapatiwa mdhamana kwa kesi yake ya awali ambayo ni shambulio,” amesema mmoja wa wanafamilia ya Paulo ambaye ameomba jina lake lifichwe.
“Mapya yaibuka”
Akizungumzia suala hilo, Mama mzazi wa Mohamed, Hidaya Somba amesema kijana wake bado amelazwa Hospitali ya Rufaa Bugando kwa ajili ya uchunguzi wa mifupa.
Amesema taarifa za madaktari zinaonyesha kuwa mguu wa kushoto ndiyo ulioumizwa zaidi na kwamba ndio mguu ambao unapeleka taarifa zote za fahamu.
Amesema mpaka sasa anaendelea kupatiwa matibabu na kwamba watamwingiza kwenye kifaa cha uchunguzi wa mifupa (X-ray) kuona iwapo watamfanyia upasuaji aua la!
Pamoja na taratibu zote za hospitali, Hidaya amesema juzi (Januari 22, 2023) alipiga simu kwa mwanasheria wa Serikali kujua maendeleo ya kesi ya kijana wake ambapo alielezwa kuwa tayari wanakamilisha taarifa muhimu ili mtuhumiwa aweze kufikishwa mahakamani.
Hidaya ameimbia Nukta kuwa alielezwa na mwanasheria huyo ambaye hakumtaja jina kuwa kwenye faili hilo tayari wana fomu namba tatu kwa ajili ya vipimo vya madaktari alivyopimwa hapo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza (Sekou toure)
“Nilichoshangaa ni kwamba fomu hiyo tayari ilikuwa imejazwa na kuwekwa sahihi kuwa mgonjwa hakuumizwa sana na alikuwa na majeraha madogo madogo ambayo alitibiwa hospitali ya Mkoa wa Mwanza Sekouture na kuruhusiwa,” amesema Hidaya.
Amesema maneno hayo yalimvunja moyo kwa kuwa fomu waliyokuwa wakizungumzia na yeye anayo na haijajazwa taarifa yoyote ambapo kwa mujibu wa askari aliyewapa fomu hiyo aliwaambia wasiirudishe hadi pale itakapojazwa na daktari kuona shida aliyopata.
Soma zaidi:
-
Mauaji ya mwanaharakati wa ujangili: 11 wahukumiwa kunyongwa hadi kufa
-
Mauaji ya kutisha yatikisa Mwanza kwa miezi miwili
-
Watatu washikiliwa na polisi mauaji ya mhadhiri SAUT
Mazungumza ya familia baina ya pande zote mbili
Akizungumzia kuhusu mazungumzo yaliyofanyika baina ya pande zote mbili, mama mzazi wa Mohamed amekiri kuwa wazazi wa Paul walifika nyumbani kwao kwa ajili ya kufanya mazungumzo ili kumaliza suala hilo kwa mazungumzo.
Hata hivyo, msimamo wa Hidaya ni kuwa hawataweza kufuta kesi hadi pale atakapojua hatma ya kijana wake kama atatembea tena au atakuwa na ulemavu wa kudumu.
“Sikuweza kukubaliana nao chochote kwani mwanangu bado ni wa kubeba na hawezi kutembea, niliwaomba waache kwanza hadi pale taarifa za madaktari zitakapotolewa,” amesema Hidaya.
Kauli ya polisi
Kamanda wa polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mtafungwa amesema wamekamilisha kufanya uchunguzi na leo mtuhumiwa huyo tayari amepandishwa kizimbani kujibu mashtaka yanayomkabiri.
Leo Paulo amefikishwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza na kusomewa mashtaka ya kushambulia ambapo mtuhumiwa alipata dhamana.
Tangazo

Latest
