Wavunja makaburi kupata vyuma chakavu
Mwonekano wa makaburi ya Serikali wilayani Magu yakiwa yamebomolewa kisha wezi kuiba misalaba ya chuma na nondo na kwenda kuviuza kama vyuma chakavu. Picha| Mariam John.
- Ni baadhi ya watu wilayani Magu, Mkoa wa Mwanza.
- Wanavunja ili kupata nondo za kuuza.
- Pia wanaida kukata viungo vya marehemu waliozikwa.
Dar es Salaam. Katika hali ya ushangaza na kuhuzunisha, kumeibuka tabia ya baadhi ya watu katika Wilaya ya Magu mkoani Mwanza kuvamia makaburi na kung’oa misalaba ya nondo na chuma na kuviuza ili kupata kipato.
Licha ya kufanya uharifu huo usio na utu, watu hao wanadaiwa kukata viungo vya marehemu na kutokomea navyo kusikojulikana.
Baada ya kusambaa kwa taarifa hizo wilayani humo, Serikali imeanza kuchukua hatua za kuwakamata.
Mkuu wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, Salum Kali amesema polisi wilayani humo wamefanikiwa kuwakamata watu waliokuwa wanabomoa makaburi na kuchukua misalaba ya nondo na chuma na kwenda kuuza.
Amesema alipokea taarifa kutoka kwa wananchi wakilalamika kuwa makaburi ya ndugu zao yamekuwa yakivunjwa na kuachwa yakiwa wazi.
“Nimeskitishwa na tabia hiyo isiyokuwa na utu ndani yake, tayari watuhumiwa wameanza kukamatwa na jeshi la polisi linaendelea kuwabaini wengine ili waweze kuunganishwa kwenye mashtaka hayo,” amesema Kali wakati akizungumza na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) Februari 28, 2022.
Amesema uchunguzi wa awali umebaini kwamba waliofanya tukio hilo la kinyama ni watu wanaotafuta nondo na misalaba kwa lengo la kwenda kuviuza kama vyuma chakavu.
Pia wanadaiwa wanabomoa zege la juu la kaburi na kisha kuchomoa nondo zote.
Amesema watu wamekuwa wakivamia makaburi ya Serikali wilayani Magu mkoani Mwanza na kuvunja majeneza huku wakikata baadhi ya viungo vya maiti na kuondoka navyo.
Kali amesema msako wa kuwasaka watu hao umeanza na kuwa ameagiza vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi hiyo usiku na mchana ili kuendelea kuwabaini watuhumiwa hao.
Serikali wilayani humo imelaani, kukemea vitendo hivyo ambavyo imeviita vya kikatili na visivyokuwa vya kawaida katika tamaduni za kitanzania.
Kutokana na hali hiyo, kwa sasa umeimarishwa ulinzi wa mgambo ambao wameagizwa kulinda makaburi hayo wakati ndugu wa marehemu waliozikwa hapo wakifanya utaratibu wa kuyajengea upya.
Latest