Mambo 12 yaliyotafutwa zaidi Google 2024, Tanzania
- Ni pamoja na michezo ya kubahatisha, kikoa (.tz), muziki, video, na lugha ya kiswahili.
Dar es Salaam. Watumiaji wengi wa intaneti hutumia injini ya utafutaji ya Google kama njia muhimu kupata maarifa, kujifunza mambo mapya, na kupata majibu ya maswali ya kila siku.
Wakati uhitaji wa maarifa mapya na matumizi ya intaneti yakiendelea kuongezeka kampuni ya Google kupitia nyenzo yake ya ‘Google Trend’, imeanisha mambo 12 yaliyotafutwa zaidi kwa mwaka 2024 nchini Tanzania.
Zikiwa zimesalia siku kadhaa kuuaga mwaka 2025 ni vyema ukatumia muda wako kupitia mambo hayo ili kama uliachwa nyuma uweze kujisasisha na maarifa mapya ili mwaka mpya uwe wa tofauti kwa upande wako.
Michezo ya kubahatisha ‘betting’
Kwenye pitapita za mjini imekuwa kawaida kukutana na ofisi za kampuni mbalimbali za michezo ya kubahatisha. Sio mtaani pekee, bali pia mtandaoni utafutaji wa michezo hiyo umeshika namba moja mwaka huu.
Wabashiri wengi wamekuwa wakitafuta, kufungua tovuti, kuingia kwenye akaunti zao, kupakua programu tumizi za kubashiri na kubashiri mbashara.
Michezo hii imeendelea kuvutia idadi kubwa ya watu, hasa vijana ambao Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 inawataja kuwa ni asilimia 77 ya watu wote chini ya umri wa miaka 35 huku asilimia 34.7 wakiwa na umri kati ya miaka 15 hadi 35.
Mikoa 10 inayoongoza kwa utafutaji wa mada hii ni Shinyanga, Rukwa, Kigoma, Mbeya, Ruvuma, Mara, Tabora, Kagera, Kaskazini Pemba na Mtwara.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha (GBT), James Mbalwe, hadi kufikia Machi 6 mwaka huu kampuni 91 za michezo ya kubahatisha zimesajiliwa kutoka kampuni 9 zilizokuwepo mwaka 2003.
Miongoni mwa kampuni maarufu ni SportPesa, Premier Bet, BetPawa, M-Bet, Meridian Bet, Parimatch, Betway, Gal Sport Betting, MkekaBet, WinPrincess, Bongo Bet, Tanzania Sports Betting, Worldstar Betting na Play Master.

Michezo ya kubahatisha ni miongoni mwa shughuli inayopendwa sana siku za hivi karibuni ikivutia zaidi vijana ambao baadhi ya tafiti zinawataja kutokuwa na ajira. Picha|Africa Press Arabic.
Tanzania
Jina Tanzania ni miongoni mwa mambo yaliyotafutwa zaidi katika mtandao wa Google na kufanya kushika nafasi ya pili.
Hii inaashiria umuhimu wa Taifa hili kwa Watanzania wenye kiu ya kulifahamu kiundani hususani katika masuala kama vivutio vya utalii kama Mlima Kilimanjaro, hifadhi ya Serengeti na fukwe za Zanzibar.
Sambamba na matukio kama chaguzi, makongamano ya kimataifa, au maendeleo ya kiuchumi na kijamii pamoja na utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu kama reli ya SGR.
Mikoa iliyotafutwa zaidi ni Kigoma, Mtwara, Mara, Shinyanga, Rukwa, Arusha, Manyara, Lindi, Ruvuma na Kagera.
‘Download’(pakua)
Upakuzi kwa mujibu wa kamusi ya kiswahili ni kitendo cha kutoa data au taarifa iliyotumwa kutoka kwenye kompyuta moja kwenda nyingine kwa njia ya mtandao.
Watumiaji wengi wametafuta kupakua nyimbo, filamu, programu tumishi na kampuni. Maneno mahususi yaliyotafutwa kwenye kipengele hichi ni MP3, muziki, apk, mp4, mdundo, Rainlex investments limited, kautaka na Facebook video downloader.
Mikoa iliyoongoza kwa upakuaji ni Lindi, Ruvuma, Mtwara, Tanga, Singida, Iringa, Pwani, Mbeya, Rukwa na Tabora.
Video
Watanzania wengi wameonekana kupendelea picha mjongeo (video) kukidhi mahitaji yao tofauti kuanzia kwenye elimu hadi burudani.
Video zilizotafutwa ni za nyimbo maarufu za wasanii wa ndani na kimataifa, filamu na vipindi vya televisheni vya ndani na nje, mafunzo (tutorials) zikilenga kujifunza stadi mpya kama vile kupika, ufundi, au teknolojia sambamba na mafunzo ya kitaaluma kama kozi za mtandaoni zinazotumia video kama njia ya kufundishia.
Huenda imechangiwa pia na kuongezeka kwa umaarufu wa video za kwenye mitandao ya kijamii kama TikTok, YouTube, na Instagram reels na ‘challenges’.
Video zimetafutwa zaidi Pemba, Unguja, Mbeya, Tanga, Pwani, Mwanza, Rukwa, Singida, Lindi, Kigoma, Ruvuma, Mtwara na Dodoma.
Mp3
Kwa mujibu wa kampuni ya muziki ya Sony, Mp3 ni muundo wa sauti wa kidijitali unaotumika kuchakata na kuhifadhi faili za sauti kwa njia inayopunguza ukubwa wake huku ubora ukibaki wa kiwango cha juu.
Nyimbo zinazowekwa kwenye mfumo huu huweza kutunzwa kwenye vifaa vya kielektroniki sambamba na vifaa vingine vya sauti za kidijitali.
Hali hii inaweza kusababishwa na watu kutafuta nyimbo mpya, huduma za muziki mtandaoni, au njia mbadala za kupakua na kusikiliza muziki. Aidha, tafsiri nyingine inaweza kuwa ni matumizi ya huduma za utiririshaji wa muziki kwenye majukwaa kama vile Spotify, Audiomack na YouTube Music.
Nyimbo zilizotafutwa zaidi ni Tshwala bam, Kautaka, Ndoa, Egwu, Nikurejeshee na Komasava, Huu mwaka, Hakuna matata, Disconnect, Kunguru na kibango.
Swahili
Kiswahili kinaendelea kutumika zaidi hasa kwenye vyombo vya habari, elimu, biashara, na sehemu muhimu ya muktadha wa utamaduni.
Watafutaji wengi wameonekana kutumia neno hili kama sehemu ya kufanya tafsiri ya maneno ya lugha tofauti kwenda kwenye Kiswahili.
Neno hili limetafutwa zaidi Zanzibar, Pemba, Arusha, Pwani, Dodoma, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Singida, Iringa, Tabora, Mtwara, Kigoma na Rukwa.
‘Livescore’
Katika dunia ya sasa ambapo mashabiki wa michezo wanapenda kufuatilia matukio ya michezo kwa wakati halisi, huduma ya Livescore imekuwa mkombozi kwao.
Huu ni mfumo wa mtandaoni unaotoa matokeo ya michezo ya soka, mpira wa vikapu, tenisi na michezo mingine punde yanapotokea bila kuhitaji kutazama mechi moja kwa moja.
Huduma hii hupatikana kupitia tovuti maalum na programu za simu, ikitoa habari kuhusu mashindano ya ligi za kimataifa na kitaifa, wachezaji na timu kwa watumiaji wake popote walipo iwe ni ofisini, nyumbani au kwenye daladala.
Kwa neno hili kutafutwa zaidi kuonyesha jinsi watu wanavyotumia zaidi teknolojia ya mtandao ili kufuatilia matukio na kupata taarifa kwa wakati halisi wakati yakiendelea.
Lugha ya kingereza
Lugha ya kingereza au jina lingine kimombo, ni lugha inayozungumzwa zaidi duniani, watu wengi huvutiwa kujifunza lugha hii kwa sababu ya umuhimu wake katika masuala ya elimu, kazi, na biashara.
Watumiaji wengi wametumia neno hili kufanya tafsiri kutoka kwenye Kiswahili, kama kamusi, kutafuta ‘subtitle’ za filamu.
Neno hili limetafutwa zaidi Zanzibar, Pemba, Arusha, Pwani, Kilimanjaro, Tanga, Dodoma, Morogoro, Tanga, Mara, Singida, Tabora, Iringa, Shinyanga, Mwanza, Kigoma, Manyara na Kigoma.
‘Song’
Unaweza kuita muziki kwa Kiswahili, yaani mpangilio wa kisanaa wa sauti ya mtu au watu ambao huambatana na mdundo wa ala ukilenga kutoa ujumbe au kuchochea hisia kwa msikiaji.
Neno hili kuchukua nafasi ya nane katika orodha ya maneno yaliyotafutwa sana, linatafsiri umuhimu wa muziki kama burudani kubwa kwenye maisha ya Watanzania na huenda hamu yao kubwa ya kupata habari za muziki na wasanii wao wapendwa.
Watu wengi wametafuta nyimbo mpya za audio na video kwa kutumia neno ‘new song’ likiambata na jina la msanii wanaemtaka.
Mikoa iliyotafuta zaidi ni Lindi, Tanga, Mbeya, Ruvuma, Iringa, Mwanza, Mtwara, Pwani, Morogoro, Manyara, Tabora, Sinyanga na Rukwa.

Baraza la Kiswahili Tanzania ni miongoni mwa taasisi zinazochangia kukuza matumizi ya kiswahili, ambapo pia watumiaji hutumia tovuti ya Google kutafuta maana ya baadhi ya maneno.Picha|Bakita.
‘Meaning’
Hili ni neno la Kiingereza lenye linalotafsiriwa kama ‘maana’ kwenye Kiswahili, kuingia kwake ndani ya orodha hii ni ishara kuwa Watanzania wengi wametumia Google kutafuta maana ya maneno, dhana au majina mbalimbali.
Baadi ya maana zilizotafutwa zaidi ni majina ya watu, maneno kama ‘aura, gen z, nonchalant, adhd, ololufemi na introvert’.
Mikoa limetumiwa zaidi neno hili ni Arusha, Kilimanjaro, Dodoma, Pwani, Morogoro, Iringa, Tanga, Zanzibar, Mwanza, Manyara, Shinyanga, Kagera, Tabora na Singida.
Kikoa (.tz)
Kikoa ni jina linalotumika kutambua tovuti na huduma mbalimbali zinazotolewa kwenye nchi husika kupitia matumizi ya intaneti. Kwa mfano, unapokutana na tovuti yenye anwani ‘https://nukta.co.tz/,’ sehemu ya mwisho (.tz) ni kikoa kinachofanya tovuti kuwa rahisi kupatikana na kutambulika.
Vikoa pia hutumika kwenye anwani za barua pepe, kama vile ‘barua@tcra.go.tz,’ kusaidia kutuma na kupokea ujumbe wa kielektroniki.
Kuonekana kwake kwenye orodha hii ya vitu vilivyotafutwa kupitia Google kumedhihirisha kuwa watu wanatafuta taarifa zinazohusiana na huduma na tovuti zinazotolewa ndani ya Tanzania.
Kimetumika zaidi maeneo ya Kagera, Rukwa, Manyara, Mtwara, Ruvuma, Mara, Lindi, Kigoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Iringa, Dodoma, Pemba na Mbeya.
‘Lyrics’
Neno hili linamaanisha maandishi au mashairi ya wimbo ambayo yanaelezea ujumbe au hisia zinazotolewa kupitia wimbo.
Wasikilizaji hutafuta maneno ya nyimbo za wasanii wa kimataifa wanazozipenda ili wao pia waimbe au waelewe maana yake.
Mashairi ya maandishi waliyotafuta watumiaji wengi wa Google ni kendrick lamar not like us, Chris Brown, American singer-songwriter. Kaa nami Israel mbonyi, over the horizon samsung, olodumare, tshwala bam, joel Iwaga olodumare, qing madi american love na commas ayra starr.
Mikoa iliyoongoza kutafuta ni Mbeya, Zanzibar, Mwanza, Pwani, Arusha, Dodoma, Zanzibar, Pemba, Kilimanjaro, Ruvuma, Mara, Lindi, Mtwara, Morogoro na Rukwa.
Latest



