Ongezeni ubunifu, thamani ya habari-Meena
- Hatua hiyo itasaidia kujikita katika habari za uchunguzi ili kutatua changamoto za upatikanaji wa nishati vijijini.
- Wataalam wasisitiza matumizi endelevu ya nishati ili kuwasaidia wananchi kupunguza gharama za umeme.
Dar es Salaam. Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena amewataka Wanahabari wanaobobea kuripoti habari za nishati kuongeza ubunifu na thamani ya habari zao ili kuhamasisha utatua wa changamoto za nishati kwenye jamii.
Nishati jadidifu siyo jambo geni lakini halijapata msukumo mkubwa wa vyombo vya habari kuwafikia watu wengi ambao wanahitaji nishati ya umeme.
Akitoa mada ya jinsi ya kuandika habari za uchunguzi jana (Januari 17, 2019) katika mafunzo maalum ya wanahabari ya nishati yanayofanyika jijini Dar es Salaam, amesema ubunifu wa kuziboresha habari za nishati ambazo zimezoeleka utasaidia jamii kuongeza na kunufaika na matumizi ya nishati yenye uhakika.
“Kuna dhana kwamba taarifa inayofahamika, watu wanaona siyo habari lakini sio kwamba kila taarifa inayofahamika basi kila mmoja inaifahamu, hapana! Taarifa inayofahamika katika sehemu A inaweza kuwa na thamani kubwa katika eneo B,” amesema Meena.
Katika kuhakikisha wanahabari wanatoa mchango wa kukua kwa sekta jadidifu, Meena amewataka kufanya marejeo ya tafiti na kuangalia namna ya kufanya habari za uchunguzi ambazo zinaweza kuleta matokeo chanya ikiwemo kuongeza uwajibikaji kwa mamlaka husika.
Mwandishi Mwandamizi kutoka kampuni ya Mwananchi Communication, Allan Lawa amesema Wanahabari wanapaswa kongeza kasi ya kuripoti habari za nishati wakibobea katika kuelimisha jamii umuhimu wake kwa uchumi na maendeleo ya Taifa.
“Kazi ya Nukta ya kusisimua uandishi huu wa habari za nishati ni jambo la kuliunga mkono sana kwasababu ndiko ambako dunia inakokwenda, nishati ile nyingine ya mafuta na makaa ya mawe inakwisha tunabaki wapi?” amehoji Lawi.
Lawi amebainisha kuwa habari hizo zikiripotiwa vizuri zitawasaidia watunga sera na wananchi kufahamu nishati mbadala inayoweza kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa ikiwemo ukame, ongezeko la joto na kina cha bahari.
Zinazohusiana:
- Wanahabari wahimizwa kuripoti habari za nishati jadidifu.
- Washiriki tamasha la nishati 2018 waondoka na matumaini kibao
- Weledi, takwimu sekta ya takwimu kuwatoa Wanahabari Tanzania
Hata hivyo, wadau wa nishati wamebainisha kuwa nguvu kubwa ielekezwe katika kutoa hamasa kwa wananchi kuwa na matumizi endelevu ya nishati jadidifu yanaweza kusaidia kuboresha huduma za kijamii, kiuchumi na kuongeza uzalishaji bishaa.
Mtaalam wa Matumizi Endelevu ya Nishati (PUE), Fredrick Mushi amesema hamasa hiyo ikifanikiwa itasaidia kutengeneza ajira za miradi midogo ya uzalishaji kama mashine za kusaga nafaka, pampu za maji zinazoendeshwa na umemejua au upepo.
“Uhamasishaji huu una uwezo mkubwa sana kuongeza ajira na kipato kwa familia ambazo zinatumia nishati,” amesema Mushi.
Pia itakuwa ni fursa kuisaidia Serikali kuharakisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya 2030 yanakusudia kuwawezesha wananchi kutumia nishati mbadala inayoweza kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Mushi ambaye amekuwa akifanya kazi na kituo cha kijamii cha Energy Change Lab, amesema kukamilisha matumizi endelevu ya nishati ni muhimu kufanyika tathmini na mchanganuo wa mnyororo wa thamani kati ya shughuli za uzalishaji na nishati inayotumika kulingana na mazingira au hali ya kiuchumi ya eneo husika.
Mafunzo Maalum ya Wanahabri ya Nishati yalipofunguliwa Januari 15, 2018 na yanafikia kilele chake leo ili kuwapa fursa Wanahabari kwenda katika maeneo yao kuzalisha habari za nishati jadidifu zinazokusudiwa kufungua fursa za uzalishaji na maendeleo kwa watanzania.