Sare za shule, nguo za watoto zapaisha mfumuko wa bei Februari
- Wafikia asilimia 3.2 kutoka 3.1.
- Bidhaa zisizo za chakula ikiwemo nguo za watoto, sare za shule zapaisha mfumuko kwa mwezi Februari 2025.
Arusha. Kasi ya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Februari 2025 imeongezeka kwa asilimia 0.1 ikichangiwa na kuongezeka kwa bei ya bidhaa zisizo za chakula ikiwemo nguo za watoto na sare za shule.
Taarifa ya mwenendo wa mfumuko wa bei nchini iliyotolewa leo Machi 10, 2025 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inabainisha kuwa mfumuko huo kwa mwaka unaoisha Februari 2025 umeogezeka hadi asilimia 3.2 kutoka asilimia 3.1 iliyorekodiwa katika mwaka unaoishia Januari 2025.
Ongezeko hilo ni la kwanza kurekodiwa katika mwaka 2025 baada ya kiwango hicho kung’ang’ania asilimai 3.1 kwa mwezi mmoja tangu Disemba 2024 huku kiwango kikubwa zaidi kikirekodiwa mwaka ulioishia Novemba 2023 cha asilimia 3.3.
Kwa mujibu wa NBS, hali hii inamaanisha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Februari, 2025 imeongezeka ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Januari, 2025 ikichangiwa na kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula.
“Baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizoonesha kuongezeka kwa Mfumuko wa bei ni pamoja na: vitambaa vya kushona nguo kutoka asilimia 0.8 hadi asilimia 1.2, nguo za wanawake (kutoka asilimia 1.9 hadi asilimia 2.0), nguo za watoto kutoka asilimia 1.3 hadi asilimia 1.4,” imesema taarifa ya Nbs.

Huenda mfumuko wa bei wa nguo za watoto ulioongezeka kutoka asilimia 1.3 hadi asilimia 1.4 ulichangiwa na sikuu za mwisho wa mwaka ikwemo Krisimasi na mwaka mpya,Picha|FreePik.
Bidhaa nyingine ni pamoja na sare za shule kutoka asilimia 3.7 hadi asilimia 3.9, nishati ya kuni (kutoka asilimia 11.9 hadi asilimia 20.7), magodoro (kutoka asilimia 4.5 hadi asilimia 4.8), huduma ya chakula na vinywaji kwenye migahawa (kutoka asilimia 1.6 hadi 1.7), huduma ya malazi kwenye mahoteli na nyumba za kulala wageni (kutoka asilimia 2.6 hadi asilimia 3.1), bidhaa na huduma kwa ajili ya usafi binafsi kutoka asilimia 4.6 hadi asilimia 4.9.
Aidha, NBS imebainisha kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Februari, 2025 umepungua hadi asilimia 5.0 kutoka asilimia 5.3 kwa mwaka ulioishia mwezi Januari, 2025.
Mfumuko wa bei usiojumuisha bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Februari, 2025 umeongezeka hadi asilimia 2.4 kutoka asilimia 2.1 kwa mwaka ulioishia mwezi Januari, 2025.
Maumivu hadi Kenya na Uganda
NBS imeeeleza kuwa mfumuko wa bei kwa nchi za jirani ikiwemo Kenya na Uganda kwa mwaka unaoishia mwezi Februari 2025 nao umeongezeka kama ilivyo nchini Tanzania.
Nchini Uganda, mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Februari 2025 umeongezeka hadi asilimia 3.7 kutoka asilimia 3.6 kwa mwaka ulioishia Januari 2025 huku nchini Kenya, ukiongezeka hadi asilimia 3.5kutoka asilimia 3.3 kwa mwaka ulioishia mwezi Januari 2025.
Latest



