Mfumuko wa bei za bidhaa, huduma wapaa Tanzania
- Wafikia asilimia 3.1 kutoka asilimia 30.0 Novemba
- Ni kutokana na kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa bidhaa zisizo za chakula.
- Hili ni ongezeko kubwa la kwanza kurekodiwa baada ya miezi miwili.
Arusha. Kasi ya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Desemba 2024 imeongezeka hadi asilimia 3.1 kutoka asilimia 3.0 ilirekodiwa Novemba ikichochewa zaidi na kupanda kwa baadhi ya bei za bidhaa za vyakula na visivyo vya vyakula.
Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.
Taarifa ya mwenendo wa mfumuko wa bei nchini iliyotolewa leo Januari 10, 2025 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inabainisha kuwa hali hiyo inamaanisha kuongezeka kwa kasi ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka unaoishia Disemba ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba, 2024.
Ongezeko hilo ni la kwanza kurekodiwa ndani ya kipindi cha miezi miwili mfululizo kuanzia mwezi Oktoba na Novemba ambapo kiwango kikubwa zaidi kilirekodiwa mwaka ulioishia Novemba 2023 cha asilimia 3.3.
Kwa mujibu wa NBS miongoni mwa bidhaa zilizochangia kupaa kwa mfumuko wa bei kwa mwaka unaoishia Disemba 2024 ni pamoja na ulezi nyama ya ngombe na samaki.
“Ulezi kutoka asilimia 5.9 hadi asilimia 9.8, mikate na bidhaa nyingine za kuoka (kutoka asilimia 11.1 hadi asilimia 15.3), nyama ya ngombe (kutoka asilimia 16.0 hadi asilimia 20.6), samaki (kutoka asilimia 15.1 hadi asilimia 18.0), maharage (kutoka asilimia 4.8 hadi asilimia 7.3), maziwa ya unga (kutoka asilimia 9.1 hadi asilimia 10.3) na karanga kutoka asilimia 9.0 hadi asilimia 10.7,” imefafanua taarifa ya NBS.
Bidhaa nyingine zisizo za chakula zilizochangia kupaa kwa mfumuko huo ni vinywaji vikali na tumbaku kutoka asilimia 1.8 hadi asilimia 2.2, sare za shule (kutoka asilimia 2.2 hadi asilimia 2.4), bidhaa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa majengo kutoka asilimia 0.6 hadi asilimia 1.2.
Nyingine ni mkaa kutoka asilimia 17.3 hadi asilimia 19.0 na huduma ya chakula na vinywaji kwenye migahawa kutoka asilimia 2.7 hadi asilimia 2.9.
Licha ya ongezeko hilo, NBS imeeleza kuwa wastani wa mfumuko wa bei wa Taifa (kutoka mwezi Januari hadi Disemba, 2024) umepungua hadi asilimia 3.1 mwaka 2024 kutoka asilimia 3.8 mwaka 2023 hali inayoashiria ahueni kwa watumiaji wa biidhaa nchini.
Maumivu hadi nchi jirani
NBS imeeeleza kuwa mfumuko wa bei kwa nchi za jirani ikiwemo Kenya na Uganda kwa mwaka unaoishia mwezi Disemba 2024 nao umeongezeka kama ilivyo nchini Tanzania.
Nchini Uganda, mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Disemba, 2024 umeongezeka hadi asilimia 3.3 kutoka asilimia 2.9 kwa mwaka ulioishia Novemba, 2024. Huku nchini Kenya, ukiongezeka hadi asilimia 3.0 kutoka asilimia 2.8 kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba, 2024.