Necta yafuta matokeo ya wanafunzi 61 darasa la saba 2024 kwa kuandika matusi na udanganyifu
- Idadi ya waliofutiwa matokeo imeongezeka kutoka wanafunzi 31 waliofutiwa matokeo kwa udanganyifu mwaka 2023.
Arusha. Wakati wanafunzi 974,229 wakifurahia matokeo yao ya darasa la saba kwa mwaka 2024 huenda hali ikawa tofauti kwa wanafunzi 61 waliofutiwa matokeo na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kwa udanganyifu na kuandika matusi.
Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Said Mohamed aliyekuwa akitangaza matokeo hayo leo Oktoba 29, 2024 jijini Dar es Salaam amesema matokeo hayo yamefutwa kwa mujibu wa sheria za baraza hilo.
“Matokeo hayo yamefutwa kwa mujibu wa kifungu cha 5(2)(i) na (j) cha Sheria ya Baraza la Mitihani, Sura ya 107, ikisomwa pamoja na kifungu cha 30(2)(b) cha Kanuni za Mitihani za mwaka 2016,” amesema Dk Mohamed.
Kati ya waliofutiwa matokeo watahiniwa 45, sawa na asilimia 0.03 ya waliofanya mtihani huo waliobainika kufanya udanganyifu huku wengine 16 wakiandika matusi katika karatasi za kujibia mtihani.
Hata hivyo, idadi hiyo imeongezeka kutoka wanafunzi 31 waliofutiwa matokeo kwa udanganyifu mwaka 2023.
Pamoja na kufuta matokeo ya watahiniwa waliofanya udanganyifu Necta imezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 148 ambao walipatwa na magonjwa au matatizo mbalimbali yaliyowafanya kushindwa kufanya mtihani kwa idadi kubwa ya masomo au masomo yote.
Watahiniwa hao wamepewa fursa ya kurudia kufanya mtihani mwaka 2025 kwa mujibu wa kifungu cha 30(1) cha Kanuni za Mitihani.
Aidha, Necta imezipongeza kamati za usimamizi wa mitihani nchini, wakuu wa shule, wasimamizi, na wasahihishaji kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya pamoja na watahiniwa wote waliofanya mtihani kwa utulivu na kuzingatia taratibu zilizowekwa.