Namna wakulima, wafanyabiashara walivyoukwaa kupanda bei ya mahindi
Bei ya jumla ya gunia la kilo 100 la mahindi kwa mwezi Machi 2020 ilikuwa Sh64,452 ikiwa imepanda kutoka Sh50,634 iliyorekodiwa Machi 2019.
- Akiba ya chakula katika ghala la Taifa nayo yapungua.
- Walaji ni moja ya walioumia na kupaa huko kwa bei
Dar es Salaam. Wakulima na wafanyabiashara huenda ni miongoni mwa watu walionufaika zaidi na zao la mahindi baada ya ripoti mpya kuonyesha kuwa bei ya jumla ya zao hilo ilipanda kwa asilimia 21.5 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Ripoti ya Mapitio ya Uchumi kwa mwezi Aprili 2020 (Maonthly Economic Review) iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaeleza kuwa bei ya jumla ya gunia la kilo 100 la mahindi kwa mwaka ulioishia Machi 2020 ilikuwa Sh64,452 ikiwa imepanda kutoka Sh50,634 iliyorekodiwa Machi 2019.
Bei hiyo ya Machi ni sawa ongezeko la asilimia 21.5 katika kipindi cha mwaka mmoja.
Kupanda kwa bei ya mahindi huenda kuliwafaidisha zaidi wakulima ambao wamewekeza kulima zao hilo au wafanyabiashara wa mazao wanaojipatia kipato cha kuendesha maisha na familia kupitia kilimo.
Mahindi ni miongoni mwa mazao makuu ya chakula yanayojumuisha mchele, maharage, viazi mviringo, mahindi, mtama, uwele, ulezi na ngano ambayo hutumiwa zaidi na Watanzania.
Hata hivyo, katika miezi miwili ya Februari na Machi bei ya mahindi imekuwa ikishuka mfululizo.
Januari bei ya jumla ilikuwa Sh92,795.8 lakini ikashuka hadi Sh85,038 mwezi uliofuata kabla ya kushuka zaidi hadi Sh64,452 mwezi Machi.
Mazao mengine ambayo bei yake imepanda katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ni mchele kwa asilimia 5.7, maharage (asimilia 10.5), mtama (asilimia 33.9) na viazi mviringo kwa asilimia 6.6.
Wakati bei ya mazao hayo ikipanda, bei ya uwele imeshuka hadi Sh126,955 mwezi Machi 2020 kutoka Sh134,727 iliyorekidiwa Machi mwaka jana.
Hata hivyo, bei za mazao makuu ya chakula zimekuwa za kupanda na kushuka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya uzalishaji, hali ya hewa na gharama za usafirishaji.
“Kulingana na mwenendo wa msimu, bei za jumla za mazao makuu ya biashara isipokuwa mtama zilishuka Machi 2020 ikilinganishwa na bei zilizorekodiwa mwezi uliotangulia (Februari),” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo ya BoT.
Akiba ya chakula nayo yashuka
Wakati bei za mazao makuu ya chakula zikipanda na kushuka, akiba ya chakula katika ghala la Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) nayo imepungua.
Ripoti hiyo ya BoT inaeleza kuwa Machi 2020 ghala hilo lilikuwa na tani 39,597 ikilinganishwa na tani 78,336 zilizokuwepo Machi 2019.
Mwenendo wa uhifadhi wa chakula katika ghala hilo ambalo huifadhi chakula kwa ajili ya dharura ikiwemo njaa nao umekuwa wa kupanda na kushuka katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Mathalan, tangu Septemba mwaka jana, akiba hiyo imekuwa ikishuka mfululizo kwa viwango tofauti kila mwezi.
Ripoti ya BoT imeeleza kuwa kupungua kwa akiba ya chakula mwezi Machi 2020 kulisababishwa na NFRA kuuza tani 1,634 za mahindi kwa wafanyabiashara binafsi, Mpango wa Chakula wa Dunia (WFP) na Idara ya Magereza.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya hivi karibuni akiwa mkoani Shinyanga aliitaka NFRA kubuni njia muafaka ya kuongeza mapato kwa kuhifadhi nafaka zaidi na kufanya biashara ya mazao ya kilimo.
“Tafuteni mbinu itakayoifanya NFRA mhifadhi nafaka nyingi zaidi kama mahindi, choroko, maharage, mpunga na ziada muweze kuuza na kupata fedha za kujiendesha kibiashara ikiwemo kutumia fursa ya mahitaji makubwa ya nafaka hususan chakula kwenye nchi za jirani na Tanzania” alisisitiza Kusaya.
Latest
