Namna tani zaidi ya 200,000 za korosho zitakavyonunuliwa na Serikali

November 13, 2018 12:04 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Rais Magufuli amesema Serikali itanunua korosho hizo kwa Sh3,300 kwa kilo ili kuwanufaisha wakulima.
  • Ameagiza usitishwaji wa ushiriki wa kampuni binafsi zilizotakiwa kuwakilisha mipango yao ya manunuzi hadi leo Saa 10 jioni. 
  • Amesema JWTZ litalinda maghala yote na litafanikisha mchakato wa kusafirisha korosho hizo hadi kwenye maghala mengine makubwa nchini.

Dar es salaam. Rais John Magufuli amesema Serikali itanunua korosho zote za mwaka huu kwa Sh3,300 kwa kilo ili kuwaokoa wakulima wa zao hilo na hasara kutokana na uwepo wa bei isiyoridhisha.

Dk Magufuli, aliyekuwa akizungumza baada ya kuwaapisha mawaziri na manaibu mawaziri wapya Ikulu leo (Novemba 12, 2018), amesema Serikali itanunua shehena yote ya korosho inayokadiriwa kufikia tani 220,000 na kuzitafutia soko hapo baadaye.

Uamuzi huo umeenda sambamba na kusitisha ushiriki wa wanunuzi binafsi wa korosho ambao hivi karibuni wamejikuta wakiingia katika mgogoro na Serikali kutokana na kuainisha bei ndogo ya kununua zao hilo linalotegemewa zaidi na wakulima wa mikoa ya Kanda ya Kusini.

“Nimeamua kusitisha mnada na sasa Serikali itanunua yenyewe kwa gharama ya Sh3,300 kwa kilo,” amesema Rais Magufuli  huku akiagiza malipo yote yafanywe na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).

Katika kutekeleza ununuzi huo, Rais Magufuli amemwagiza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuzielekeza kampuni zote zilizojaribu kuleta mapendekezo kwake kwa ajili ya kununua korosho hizo kusitisha zoezi hilo mara moja.

“Waambie waache, watakuja kutuchezea watakwambia wanataka tani 200,000 lakini baadaye wataanza kutuletea masharti na ‘kudelay’ (kuwachelewesha) wakulima wetu, wamesema watanunua kwa bei elekezi Sh3,000 je, ikipanda Desemba?

“Kwa hiyo hawa wanaoendelea kuja wala wasihangaike kuja wanaokuja  sasa ni saa 5:15, nimeshafunga wala wasiangaike korosho tutanunua wenyewe,” amesema Rais Magufuli akionekana kukasirika na mwenendo wa wafanyabiashara hao wa korosho.

Wiki iliyopita (Novemba 10, 2018) Majaliwa aliwapa wanunuzi wote wa korosho waliosajiliwa kuwasilisha taarifa za tarehe na kiwango cha tani za korosho wanazotaka kununua ndani ya siku nne. Leo Saa 10 jioni ilikuwa ni muda wa mwisho kuwasilisha barua hizo. 

Katika hotuba hiyo, Dk Magufuli amasema japo yeye siyo mtaalam wa uchumi bado shehena ya korosho inaweza kabisa kununuliwa na soko la ndani ikizingatiwa kuwa gharama ya kilo moja ya zao hilo iliyobanguliwa ni kati Sh15,000 hadi Sh25,000.

Ameeleza kuwa iwapo ukibangua korosho kilo tatu itatoa kilo moja hivyo tani 210,000 za korosho ghafi zitasaidia kupatikana kwa tani 70,000 zilizochakatwa jambo litakaloleta urahisi wa kuuzika.

“Watanzania tuko milioni 55  tukachukulia Watanzania milioni 35 wanakula korosho  kila moja akala korosho kilo mbili tu hizi tani 70,000 zinaisha zote,” amesema Rais Magufuli na kufanya wageni waalikwa kuangua kicheko.


 Zinazohusiana: 


Kwa mujibu wa Rais, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) litakuwa na jukumu la kusimamia na kuhakikisha ulinzi kwenye maghala ya korosho na upimaji kwenda sawa na wakulima wanalipwa stahiki zao kikamilifu.

“Jeshi likishapokea korosho ambazo tayari zimeshalipiwa itapeleka kwenye maghala makubwa na nimeshaambiwa wanajeshi wapo tayari ,” amesema. 

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amekabidhi Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kiwanda cha Buko kilichopo mkoani Lindi chenye uwezo wa kuzalisha tani 20,000 kwa mwaka. Kiwanda  kilirudishwa serikalini hivi karibuni baada ya mwekezaji kushindwa kukiendesha.

Zitto Kabwe ataka uwajibikaji katika ununuzi

Kiongozi wa Chama cha ACT -Wazalendo, Zitto Kabwe licha ya kupongeza  Serikali kwa hatua hiyo, amesema itafanya nchi ikose mapato ya fedha za kigeni ambayo ni muhimu katika kutunza thamani ya Shilingi. 

“Pia wapo Watanzania wengi watakaoathirika kutokana na kutokuwepo kwa mnyororo wa korosho (Value Chain) kuanzia wenye magari ya usafirishaji, wamiliki wa nyumba za wageni, wenye mikahawa, makuli, mawakala wa meli pamoja na wamiliki wa maghala. 

“Watu wote hawa ni walipa kodi, hivyo Serikali itakosa mapato. Pia, Serikali itakosa mapato ya kodi ya Export Levy pamoja na mapato ya kodi ya halmashauri za miji inayolima korosho,” amesema Zitto katika taarifa yake kwa wanahabari. 

Amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba ndiyo itakayoathirika zaidi kwa kuwa ilitarajiwa kupata Sh5 bilioni mwaka huu.

Zitto ambaye ni mchumi, amedai kuwa TADB haina fedha za kumudu ununuzi wa korosho zote nchini kutokana na hali ya ukwasi wa taasisi hiyo.

“Maagizo ya kuwa TADB ndioy wanapaswa kununua korosho yameleta mashaka kidogo kwetu. Uwezo wa mtaji wa kifedha wa TADB ni Sh200 bilioni tu, zinazoweza kununua 30% tu ya korosho zinazotarajiwa kuvunwa, ili kununua Korosho zote, tani 200,000 wanahitaji Sh660 bilioni. Serikali inataka kuwakopa wakulima wa Korosho? Tunatoa tahadhari kuwa iwapo Serikali itawapa fedha TADB kwa shughuli hii lazima ifuate Sheria,” amesema na kuongeza,

“Tuna mashaka kuwa Benki Kuu itatoa Fedha za Mashirika ya Umma zilizopo kwenye akaunti zake na kuwapa TADB. Jambo hili likifanyika bila kufuata sheria itakuwa ni wizi kama wizi mwengine wowote. Tutaendelea kufuatilia kwa kina suala hili ili kuhakikisha Serikali haitumii fedha za umma hovyo ili kufunika makosa yake yenyewe.”

Enable Notifications OK No thanks