Baada ya kodi ya uzalendo, Zungu aitaka Serikali kuangazia mapato ya intaneti
- Asema kwenye huduma hizo kuna pesa nyingi.
- Asema fedha nyingi zinaenda nje ya nchi kwa sababu hakuna udhibiti.
- Ashauri mifumo ya mapato iunganishwe pamoja.
Dar es Salaam. Naibu Spika wa Bunge Mussa Azzan Zungu ameishauri Serikali kuandaa mkakati maalum utakaowezesha huduma za intaneti zinazotolewa nchini kuchangia katika ukuaji wa pato la Taifa kwa sababu huduma hizo zinakua kwa kasi.
Zungu aliyekuwa akihitimisha kipindi cha maswali na majibu Bungeni jijini Dodoma leo Septemba 21, 2022 amesema kwa sasa pesa nyingi ziko kwenye huduma za intaneti zinazotolewa na kampuni za simu.
“Tunakutegemea (Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye) ufanye haya mabadiliko nchini, tupate pesa nyingi kwenye intaneti, sasa hivi mapato mengi ya simu siyo kwenye kupiga simu bali kwenye data, huku ndipo pesa ilipo,” amesema Naibu Spika Zungu.
Ameshauri Nape kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha “gateway (mfumo) ya intaneti inabaki nchini na mapato haya yabaki nchini tusilipe nje ya nchi.”
Kwa sasa Tanzania haipati mapato yatokanayo na matumizi ya intaneti licha ya kuwa na ongezeko kubwa la watu wanaotumia huduma hiyo huku wanaotoa huduma hizo hulazimika kulipia ili kupata intaneti kimataifa.
“Tanzania hatuna GDP (Pato la Taifa) kwenye intaneti, sovereignty ya intaneti gate way (umiliki wa mfumo wa intaneti) iko nje ya nchi, kwa maana hiyo pesa inakwenda nje ya nchi tunapowasiliana kwa intaneti sisi, tunao watoa huduma lakini vilevile wao wanalipa fedha hizi nje ya nchi,” amefafanua Zungu.
Soma zaidi:
Kwa mujibu wa maelezo yake endapo mchakato wa kupata uhuru wa kimtandao ukikamilishwa utatoa fursa kwa vijana kujiajiri kama watoa huduma, sambamba na kuisaidia Serikali kupata fedha kwa njia ya kodi.
“Intaneti inaweza ika-decentralize (kugatua) maeneo mengi nchini vijana wakawa watoa huduma, najua siyo jambo dogo litapigwa vita sababu ni swala la pesa, hapa tunazungumzia maslahi ya Taifa kumsaidia Rais apate mapato na vijana wapate ajira ya kuwa watoa huduma kwenye intaneti,” amesisitiza Zungu.
Unganisheni mifumo ya mapato
Katika hatua nyingine, Zungu ameshauri Serikali kuunganisha mifumo ya ukusanyaji mapato katika vyanzo vyake ili kupunguza upotevu wa mapato kutoka katika rasimali zake.
“Bandari yetu ya Dar es Salaam inakusanya Sh95 bilioni tu kwa mwezi, kuna bandari nchi jirani inakusanya takribani Sh300 bilioni kwa mwezi. Hii inatokana na mifumo kutokuunganishwa inasababisha mapato mengi yanapotea,” amesema Zungu.