Mzee wa miaka 72 alivyoachana na mila inayochochea maambukizi ya Uviko-19

October 27, 2021 12:08 pm · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni mkazi wa jijini Mbeya, Sekela Mwaijulu.
  • Ni tabia ya kusalimiana kwa kushikana mikono na kukumbatiana.
  • Watalaam wapendekeza njia mbadala ya kusaliamiana kwa kupunga mikono.

Mbeya. Moja ya mila na desturi ya kabila la Wanyakyusa si rahisi kumkuta mtu wa kabila hilo akimsalimia mtu mwingine hasa aliyemzidi umri bila kumshika mkono, kumkumbatia, kupiga magoti au kuchuchumaa.

Mtu anayesalimia bila kufanya vitendo hivyo anatafsiriwa kuwa hana adabu na aliyekosa heshima katika jamii.

Lakini tofauti na ilivyo kwa sasa, mlipuko wa ugonjwa wa Corona (Uviko-19) umebadilisha mwenendo wa tamaduni za kabila hilo ambapo miongozo ya wataalamu wa afya inashauri watu wasishikane mikono au kukumbatiana.

Hatua hiyo inasaidia kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. 

Badala yake watu wanahimizwa kunawa mikono kwa maji tiririka mara kwa mara, kutumia vitakasa mikono, kuvaa barakoa, kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima na kupata chanjo.

Kwa kiwango kubwa desturi hizo za Wanyakyusa hushikiliwa na watu wenye umri mkubwa kama Sekela Mwaijulu ambaye kwa sasa ameamua kuachana na utaratibu huo baada ya kupata elimu kutoka kwa wataalamu wa afya.

Sekela Mwaijulu (72) anasema ameamua kuachana na desturi hiyo baada ya kuona athari za Uviko-19 ikiwemo vifo hivyo anapokwenda misibani au kwenye mikusanyiko lazima anawe mikono au kuvaa barakoa.

“Mimi ni lazima ninawe mikono siwezi kufika sehemu bila kunawa mikono,” anasema Sekela, mkazi wa Mafiati jijini Mbeya ambaye sasa kushikana mikono na kukumbatiana siyo kipaumbele chake.

Kutoshikana mikono au kutokukumbatiana siyo tu kumesaidia kupunguza maambukizi ya Uviko-19 bali kumesaidia kupunguza magonjwa mengine hasa ya mlipuko ikiwemo kuhara ambayo husababishwa na uchafu.

Licha ya kuwa kushikana mikono na kukumbatiani hakupendekezwi kwa sasa, wataalam wa saikolojia wanaeleza kuwa kugusana kimwili kunaongeza kingamwili, kunapunguza msongo wa mawazo na kuwaunganisha wapendanao. 

Sekela Mwaijulu (72) pichani anasema kwa sasa ameamua kuweka kando mila aliyoizoea kwa muda mrefu ya kusalimiana kwa kushikana mikono ili kujikinga na Uviko-19. Picha| Isakwisa Mbyale.

Haikuwa rahisi kwa Sekela

Valentina Mwaijulu, mjuu wa Sekela anasema ilimchukua muda mrefu bibi yake kuelewa umuhimu wa kuacha kushikana mikono wakati wa kusalimiani kutokana na utamaduni huo kuishi nao kwa muda mrefu.

“Hapa bibi amebadilika sana mwanzoni alikuwa haelewi kabisa ukimueleza kusalimiana bila kushikana mikono” anasema Valentino.

Siyo Sekela peke yake, hata wazee wa kabila hilo mkoani hapa imewachukua muda kukubali kuacha kwa muda utaratibu wa kusalimiana kwa mikono. 

Mkazi wa Majengo jiji Mbeya, Jackson Mwaipopo anasema ingawa hapo awali ilikuwa ikimfanya aeleweke vibaya kwa wazee wake kutokana na kuwasalimia bila kuwashika mikono na kuwakumbatia lakini kwa sasa haina ugumu tena kutokana na kuongezeka kwa elimu.

“Sasa hivi kila siku utasikia wataalamu wanasema msishikane mikono msishikane mikono hii imesaidia wazee kuelewa kuwa ukiwasalimia kwa umbali bado ina maana wala haipunguzi heshima yake” anasema Mwaipopo.

Huenda utamatuduni huo wa kusalimiana kwa mikono ukarejea tena baada ya Serikali na wadau wa afya kuimarisha mapambano ya Uviko-19 kwa kuwekeza nguvu kubwa katika utoaji wa chanjo.

Chanjo hiyo inasaidia kupunguza maambukizi kwa kiasi kikubwa na idadi ya watu wanaolazwa hospitalini. 

Hadi kufikia Oktoba 26 mwaka huu, Tanzania ilikuwa imeripoti wagonjwa wa Corona 26,115 na vifo 725, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Afisa Afya wa jiji la Mbeya, Baraka Kipesa anasema matokeo hayo ni kutokana na nguvu kubwa waliyowekeza katika kutoa elimu kwa umma.

“Tangu wimbi la kwanza hata hili la sasa suala la elimu limekuwa ni kipaumbele kikubwa na hayo ndiyo matokeo yake na sisi tunafahamu kwamba mapambano haya yako katika hatua nzuri” alisema Kipesha.

Kipesha anahimiza watu kuendelea kuzingatia tahadhari zote zinazopendekezwa na wataalam wa afya za kujikinga na maradhi ya Uviko-19 ikiwemo kuzingatia umbali kati ya mtu mmoja na mwingine.


Mbadala wa kushikana mikono

Wataalam wa afya likiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO) wanashauri watu kusalimiana kwa njia mbalimbali wakati huu ikiwemo kwa kupunga mikono wakiwa mbalimbali.

Pia kusalimiana kwa kugonganisha viwiko vya mikono au miguu, jambo linalosaidia kutokahusana moja kwa moja mwilini kama ilivyo desturi ya watu wengi. 

Makala hii imefadhiliwa na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV

Sakata bei ya mafuta kupanda latua BoT, Naibu Gavana atoa ufafanuzi

Sakata bei ya mafuta kupanda latua BoT, Naibu Gavana atoa ufafanuzi

Nukta TV

BoT yabakiza Riba ya Benki Kuu 5.75% kudhibiti mfumuko wa bei

BoT yabakiza Riba ya Benki Kuu 5.75% kudhibiti mfumuko wa bei

Nukta TV