Daraja la Kigongo-Busisi: Alama isiyofutika ya Magufuli jijini Mwanza

March 17, 2022 5:02 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Litakuwa daraja refu kuliko yote Afrika Mashariki
  • Linatarajiwa kukamilika mwaka 2023 na alama ya Hayati Magufuli Mwanza.
  • Wananchi wasema litakuza biashara na kuokoa maisha. 

Mwanza. Ingawa amefariki dunia lakini bado ataishi katika mioyo ya watu kutokana alivyogusa maisha ya watu mbalimbali siku za uhai wake wakiwemo wakazi wa kanda ya Ziwa nchini Tanzania. 

Huyo ni Hayati John Magufuli, aliyekuwa Rais wa awamu ya tano ya Tanzania ambaye alifariki dunia Machi 17 mwaka huu jijini Dar es Salaam kutokana na maradhi ya moyo.

Kifo chake kiliacha simanzi na majonzi kwa wananchi wa Tanzania lakini ataendelea kukumbukwa daima huku moja ya kumbukumbu hizi ni kuasisi ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi lilipo Ziwa Victoria ambalo ujenzi wake unaendelea.

Daraja hilo ambalo limepewa jina la John Magufuli linalounganisha mikoa ya Mwanza na Geita na nchi za maziwa makuu likikamilika  litakuwa na urefu wa kilomita 2.3 na upana mita 28.45 na ujenzi wake utagharimu Sh699 bilioni. 

Daraja hilo linalotajwa kuwa refu kuliko yote Afrika Mashariki, na la sita kwa urefu barani Afrika litakuwa mbadala wa vivuko vya MV Misungwi, MV Sengerema na MV Mwanza. 

Maono ya Hayati Magufuli yalikua ni kuhakikisha Mkoa wa Mwanza unakuwa kivutio kikuu cha utalii kwa nchi za maziwa makuu na ujenzi wa miundombinu ni kichocheo kikuu cha shughuli hizo. 

Huenda alitamani ashuhudie uzinduzi wa daraja hilo muhimu kwa wakazi wa kanda hiyo ukiwemo mkoa aliozaliwa wa Geita. 

Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli akiangalia picha ya mfano wa daraja la Kigongo (Misungwi) hadi Busisi (Sengerema) mkoani Mwanza kabla ya kifo chake. Daraja hilo litakalopita ziwani litakuwa na urefu wa kilomita 3.2 na kufanya kuwa daraja refu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki. Picha| Ikulu Tanzania.

Maono ya Magufuli kwenye daraja hilo

Akihutubia mamia ya wakazi wa Wilaya za Sengerema (Geita) na Misungwi (Mwanza) eneo ambalo daraja hilo linajengwa, kabla ya kifo chake, Hayati Magufuli alisema ujenzi wa daraja hilo unaojengwa na fedha za ndani  ni kielelezo kingine kwamba Tanzania ina uwezo wa kutekeleza miradi yake yenyewe  kwa kutumia fedha zake za ndani bila kutegemea wafadhili  kutoka nje ya nchi.

Alisema manufaa ya kiuchumi ya utekelezaji wa mradi huo hayatanufaisha Watanzania pekee bali na nchi jirani za Rwanda, Uganda, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC)  na Burundi.

Ukamilishwaji wa mradi huo utakuwa umetoa fursa za ajira 1,600 kwa wakazi wa maeneo jirani na utapunguza changamoto ya usafirishaji kwa  wananchi wa kanda ya ziwa. 

Daraja hilo litatatua kero ya miaka mingi iliyosababisha vifo kutokana na ajali za majini na wagonjwa kucheleweshwa hospitali, kuchelewa kwa biashara na safari za wananchi.


Soma zaidi: 


Litaokoa maisha, biashara za watu

Baadhi ya wakazi katika maeneo mbalimbali jijini Mwanza wameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa daraja hilo litasaidia kupunguza upotevu wa muda na gharama kubwa ya kuendesha biashara zao. 

Pius Kamala, mkazi wa Usagara wilayani Misungwi, anasema ujenzi wa daraja hilo utaboresha usafirishaji na kupunguza muda wa kuvuka kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Kamala anasema pia daraja hilo litakuwa moja ya kivutio cha utalii na kwa kiasi fulani litaongeza mapato ya Taifa na kwamba “maono ya kiongozi Magufuli ilikuwa ni kurahisisha usafirishaji.”

Daraja hilo, linalojengwa na wakandarasi wa China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) na China Railway 15 Group Corporation, kwa mujibu wa mkazi wa Sengerema, Petro Pendo litaokoa maisha ya wagonjwa, akina mama wajawazito na wengine ambao maisha yao yalipotea kwa kusubiri kivuko.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mhandisi Patrick Mfugale alisema ujenzi wa daraja hilo pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 1.66 umepangwa kukamilika  Julai 2023. 

Picha ya namna daraja la Kigongo –Busisi litakavyokuwa mara baada ya kukamilika. Picha| Ikulu.

Tanroads itamuenzi Hayati Magufuli

Meneja wa Tanroads Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Vedastus Maribe amesema kifo cha Magufuli kimewagusa kwa kuwa walitamani baada ya daraja hilo kukamilika ndiye angekuja kulizindua. 

Mhandisi Maribe anaeleza kuwa hadi sasa kazi ya ujenzi wa daraja la muda umekamilika kwa asilimia 90 na kwamba daraja lenyewe limeanza kujengwa na sasa limefikia asilimia 20.

“Tuna maumivu makubwa kama kiongozi aliyekuwa na ndoto za kujenga daraja hilo lirahisishe usafiri  kwa Watanzania ndoto hizo tulitamani zitimie kwa yeye kuja kulizindua baada ya kukamilika, “anasema Maribe.  

Anasema bado wanatumaini kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ndiye atatimiza ndoto za kiongozi huyo kwa kuja  kulizindua mara tu litakapokamilika. 

Kazi ya ujenzi wa daraja hilo, Maribe anasema inatia matumaini makubwa na mpaka sasa zaidi ya Sh89 bilioni zimeshatolewa kumlipa mkandarasi.

Enable Notifications OK No thanks