Mvutano mkali: Mlima wa kijiji ukiuzwa kwa mwekezaji

March 24, 2023 8:11 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link

Wananchi wa kijiji cha Mwasonge kata ya Identemya wilayani Misungwi wakiwa kwenye mkutano wa hadhara kujadili maendeleo ya kijiji hicho ambapo ajenda kubwa ilikuwa ni kuuzwa kwa mlima wa kijiji ambapo baadhi yao wanapinga kwa sababu ni kitega uchumi chao. Picha | Mariam John. 


  • Mlima wa kijiji cha Mwasongwe mkoani Mwanza wauzwa kupata pesa za kujengea madarasa.
  • Baadhi ya wananchi wapinga wasema wanautimia kupata kipato.
  • Serikali yaingilia kati yataka wananchi waridhiane. 

Mwanza. Mvutano umeibuka baina ya wananchi katika Kijiji cha Mwasonge wilayani Misungwi mkoani Mwanza juu ya uuzwaji wa mlima wa kijiji hicho ili kupatikana kwa fedha za kujengea shule ya sekondari.

Wapo wananchi wanaokubaliana na suala hilo wakieleza kuwa yalikuwa makubaliano yao huku wengine wakipinga kwa kueleza kuwa mlima huo unawasaidia katika kujiingiza kipato.

Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji hicho hivi karibuni, baadhi ya wananchi wamesema suala la kuuzwa kwa mlima huo lilizungumziwa kwenye mkutano wa Kijiji uliopita ingawa kuna baadhi hawakuwa wamehudhuria.

Luchwenula Pauline ni mkazi wa Kijiji cha Mwasonge pamoja na kujishughulisha na kilimo lakini pia shughuli zake nyingine hufanyia katika mlima huo za kuponda kokoto.

Pauline amesema ni siku ya tatu sasa shughuli hizo zimesitishwa kwenye mlima huo kwa maelezo kuwa tayari mwekezaji amekabidhiwa eneo hilo.

“Shughuli zetu kuu za kipato tunazifanyia kwenye mlima huu, lakini leo ni siku ya tatu tumezuiwa kuendelea tukielezwa mlima umeuzwa kwa mwekezaji jambo ambalo wananchi hatukushirikishwa,” amesema Pauline

Mkazi mwingine, Machunda Ngemela amesema kuna mashamba yapo chini ya mlima huo ambayo pia yanadaiwa kuuzwa kwa mwekezaji huyo bila wamiliki kushirikishwa.

“Suala hili hatukushirikishwa kama tunakubaliana kuyauza (mashamba) na kwamba hii nchi ni ya demkrasia kwanini wasipate maoni yetu juu ya hili suala?,” amehoji Ngemela.

Hat hivyo, wapo baadhi ya wananchi ambao wamesema suala la kuuza mlima walikubaliana katika mkutano wa kijiji kilichoitishwa na Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Masumbuko Ruben.

Akizungumzia suala hilo, mjumbe wa kamati ya upimaji shirikishi wa Kijiji hicho, Fidelis Kanali amesema makubaliano ilikuwa mlima huo uuzwe ili pesa itakayopatikana ambayo ni Sh10 milioni ziwasaidie katika ujenzi wa maboma mawili ya shule ya sekondari Mwasonge.

Amesema maamuzi hayo yalifikiwa baada ya kusuasua kwa michango ya wananchi kwa ajili ya ujenzi wa maboma ya shule mbili za msingi na sekondari.

“Ajenda kuu kwenye mkutano huo ilikuwa mlima huo uuzwe ili kupata fedha kwa ajili ya kukamilisha maboma mawili ya vyumba vya madarasa lakini kinachoonekana kwa sasa ni vitu viwili tofauti,” amesema Kanali.

Amesema hata baada ya makubaliano hayo, wapimaji walianza kazi ya kupima na watu walio karibu na mlima huo walishirikishwa na kuwa wanaacha sentimita ambazo wao wanataka zibaki.

“Leo tunashangaa kuibuka baadhi ya watu wakidai kuwa suala hili halikuwa shirikishi,” amesema Kanali.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Masumbuko Rubeni ambaye ameshiriki katika zoezi la uuzaji wa mlima huo amesema kuwa zoezi hilo sio maamuzi yake bali aliitisha mkutano na wananchi wakakubaliana wasichange pesa ya maendeleo ya ujenzi wa shule na badala yake baadhi ya maeneo yauzwe katika mlima huo ili pesa ipelekwe katika ujenzi wa shule.

Diwani wa Kata ya Idetemya, Edward Dauson akizungumza na wananchi hao ametoa maagizo la kusitishwa kuuzwa kwa mlima huo kutokana na wananchi kutoridhiana kwa pamoja mpaka pale suala hilo litakapopata ufumbuzi.

Dauson amemwagiza mtendaji wa Kijiji hicho kupitia upya muhtasari wa kikao hicho kisha ashirikishe ofisi ya ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kwa ajili ya kuja na mipango thabiti.

“Kwa sasa shughuli zozote zisitishwe kwanza hadi pale timu ya wataalam wa ardhi kutoka halmashauri itakapopitia upya masuala haya,” amesema Dauson.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW