Mpango aanika vikwazo kufikia malengo Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025

April 3, 2023 3:46 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na Umaskini wa kipato na lishe duni.
  • Aahidi ushirikishwaji wa watu wote.

Dar es Salaam. Ikiwa imesalia miaka miwili kuhitimisha miaka 25 ya Dira ya Taifa ya Maendeleo, Serikali imeeleza kuwa kuna changamoto kubwa zikiwemo umaskini wa kipato na lishe duni vilivyokwamisha usitekelezeke kikamilifu. 

Makamu wa Rais Dk.Philip Mpango ameeleza leo Machi 3, 2023 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa mchakato wa kuanza kuandaa Dira ya Taifa ya mwaka 2050 takribani asilimia 26.4 ya Watanzania bado  wanaishi chini ya kipato na wananchi masikini zaidi wanaishi vijijini.

Kwa takwimu hizo zilizotajwa na Dk Mpango ni sawa na kusema zaidi ya robo ya Watanzania bado wanaishi katika lindi la umaskini huku asilimia takriban theluthi moja au asilimia 31.3 ya watu hao wakiishi vijijini.

Makamu huyo wa Rais amesema  baadhi ya mikoa inayokabiliwa na kiwango kikubwa cha umaskini kuwa ni Kagera, Kigoma, Singida, Tabora na Dodoma.

Makamu wa Rais Dk Philip Mpango (Kushoto) akizindua mchakato wa kuanza kuandaa Dira ya Taifa ya mwaka 2050, kulia ni Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba.Picha|Wizara ya Fedha.

Lishe bado tatizo Tanzania

Mbali na Umaskini Dk Mpango amesema lishe duni imechangia kwa kiwango kikubwa kuzorotesha mafanikio ya Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025 inayowakabili asilimia 30 ya watoto waliopo nchini. 

Hii ina maana kuwa watoto watatu kati ya 10 Tanzania wanakabiliwa na lishe duni jambo linalozorotesha afya na kudumaza akili zao.  

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alieleza hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa ripoti ya Viashiria Muhimu vya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto (THDS-MIS) ya mwaka 2022 kuwa watoto milioni 2.8 waliopo nchini wana udumavu unaosababishwa na lishe duni. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo mikoa ya  Njombe, Iringa na Ruvuma inaongoza kwa idadi kubwa ya watoto wenye udumavu licha ya kuwa miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa chakula.

Katika hotuba yake leo, Dk Mpango amesema changamoto nyingine zinazokwamisha Serikali kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025 ni rushwa, ufujaji wa mapato ya Serikali, wizi, matumizi yasiyo na tija na mapungufu kwenye eneo la haki jinai.

Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025 ilikuwa na malengo makuu matano ambayo ni kuboresha hali ya maisha ya Watanzania, kujenga uchumi imara,utawala bora, usalama na umoja katika nchi pamoja na jamii iliyoelimika vyema.


Soma zaidi


Mchakato utashirikisha wananchi wote

Akihutubia kwenye uzinduzi huo Makamu wa Rais amesema mchakato wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050 utakuwa shirikishi ukihusisha watu wa makundi yote ndani na nje ya nchi.

“Watanzania waliopo ughaibuni na washirika wa maendeleo watapewa muda wa kutosha wa kushiriki kwenye mchakato huu muhimu,” amesema Dk Mpango.

Sambamba na hayo amesisitiza Wizara, Taasisi za Umma, Idara zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Sekta binafsi  pamoja na wadau wote wa maendeleo kutoa ushirikiano kwa timu ya maandalizi ya dira hiyo.

“Niwaombe watanzania kutenga muda wa kutosha kushiriki kikamilifu katika zoezi hili muhimu kwa ajili ya mustakabali wa nchi yetu,” ameongeza Dk Mpango.

Miongoni mwa mambo yanayotakiwa kuzingatiwa kwenye mchakato wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050 ni pamoja na kuimarisha uwezo wa uchumi, kuongeza matumizi ya Sayansi na teknolojia pamoja na kuimarisha mifumo ya elimu  ya sayansi, ufundi, utafiti na ubunifu.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW