Mambo ya kutupia macho katika maandalizi Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050
- Ni pamoja na kuzingatia mahitaji ya vijana pamoja na uimarishaji wa utawala bora
- Waliotoa maoni wafikia 800,000.
Dar es Salaam. Makamu wa Rais Dk Philip Mpango amebainisha mambo matano muhimu yanayotakiwa kutupiwa macho katika maandalizi ya dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 itakayotoa mwelekeo wa taifa kwa miaka 25 ijayo.
Dk Mpango aliyekuwa akizungumza katika uzinduzi wa kongamano la kwanza la kitaifa la kuhusu maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 uliofanyika leo Juni 8, 2024 jijini Dar es Salaam ameyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na kuzingatia mahitaji ya sasa na ya baadae ya vijana.
“Dira ya 2050 inapaswa iwe ya vijana zaidi na kwa ajili ya vijana, sababu yake ni kuwa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 inasema asilimia 77.5 ya watanzania ni vijana na watoto kati ya miaka sifuri hadi 35 huku kundi la vijana kuanzia miaka 15 wakiwa ni asilimia 34.5,” amesema Dk Mpango.
Kutokana na takwimu hizo Dk Mpango amesema kuwa ni vyema dira hiyo ikaweka nguvu kwenye maendeleo ya elimu ya kujenga ujuzi wa stadi za kazi, teknolojia na upanuzi wa shughuli zinazovutia vijana ikiwemo tehama, sanaa, burudani, uwezeshaji wa shughuli zinazochipukia (startups) na kilimo janja.
Utekelezaji wa masuala hayo unatarajiwa kutatua tatizo kubwa la utegemezi lililopo nchini hivi sasa ambapo kwa mujibu wa Dk Mpango umefikia asilimia 87.4 jambo linalodidimiza ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Hii ni mara ya kwanza kwa kongamano la maandalizi ya dira hiyo kufanyika nchini tangu yalipozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Disemba 9, 2024.
Kongamano hilo lililowakutanisha wananchi, wanazuoni, viongozi wa Serikali na wadau wa maendeleo ni mwanzo wa safari ya kukamilika kwa dira hiyo inayotarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi kwenye maeneo ya uzalishaji yanayowagusa wananchi.
Soma zaidi:Rais Samia adokeza vipaumbele Dira ya Maendeleo 2050
Dira ya Taifa 2050 izingatie utawala bora
Suala lingine linalotakiwa kupewa kipaumbele katika maandalizi ya dira hiyo ni utawala bora na uwajibikaji ambapo kwa mujibu wa Dk Mpango ni miongoni mwa maeneo yenye changamoto zinazokwamisha maendeleo ya nchi.
Masuala hayo pia yalijitokeza katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2023, na ripoti ya Tume ya Haki jinai iliyowasilishwa kwa Rais Julai, 2023.
Dk Mpango amebainisha kuwa pamoja na hatua ambazo Serikali inazichukua kuboresha upatikanaji wa utawala bora dira hiyo inatakiwa kuweka mikakati bora ili kuimarisha suala hilo.
Aidha, dira hiyo pia inatazamiwa kuweka mkakati matumizi sahihi ya rasilimali zinazolitambulisha Taifa letu ikiwemo madini ya kimkakati na ujenzi wa viwanda vitakavyowezesha uzalishaji wa bidhaa zenye ubora kwa ajili ya masoko ya kimataifa.
Awali Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema kuwa tangu kuzinduliwa kwa mchakato wa kukusanya maoni kuhusu dira hiyo wamepokea maoni kwa watanzania zaidi ya 800,000 kupitia njia ya simu za mkononi, tovuti na nyinginenzo.
“Watu wengi wamejitokeza na waliotoa maoni wengi ni vijana kati ya miaka 15 hadi 35 ambao ni asilimia 80 ya wote waliotoa maoni na maoni ni mazuri sana,” amesema Prof Mkumbo.
Mbali na jitihada hizo wizara hiyo itaendelea na mchakato wa kukusanya maoni ili kuwawezesha wananchi wa Tanzania hususani vijana kushiriki kikamilifu katika maandazi ya dira hiyo itakayotoa mwelekeo wa Taifa kwa miaka 25 ijayo.
Latest
