Sheikh wa mkoa Mwanza: Serikali idhibiti muda watoto kurudi nyumbani

April 3, 2023 2:43 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Ashauri ni vema watoto wakawa wamesharudi kutoka shule Saa 12 jioni kuwaepusha na ukatili wa kijinsia.
  • Aeleza vitendo vya ulawiti na ushoga hutokea kwa sababu ya mmomonyoko wa maadili na huwakumba watoto kutokana na kuchelewa kurudi nyumbani. 

Mwanza. Katika jitihada za kuwaokoa watoto na ukatili wa kijinsia, Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke ameiomba Serikali kuweka utaratibu utakaowasaidia wanafunzi kurudi mapema shuleni au kwenye masomo ya ziada. 

Kabeke amewaeleza wanahabari Jijini Mwanza leo (Aprili 3, 2023) kuwa licha ya Serikali kuchukua uamuzi mzuri wa kuzuia shule za bweni kwa watoto wadogo bado wanaosoma kutwa wanachelewa kurudi nyumbani jambo linalofanya wawe hatarini kufanyiwa ukatili wa kijinsia ikiwemo kulawitiwa. 

Uamuzi wa hivi karibuni wa Serikali kuwaondoa wanafunzi kwenye madarasa kuanzia darasa nne kushuka chini, amesema utasaidia kwa kiasi fulani kulinda na kutunza maadili.

Katika ombi lake, Sheikh Kabeke amesema wanafunzi wanaporudi mapema shule au kwenye masomo ya jioni watapata muda mzuri wa kupumzika na kurejea kufanya mambo mengine ya nyumbani.

Amesema suala hilo la maadili pia liende sambamba na malezi ya kiroho kwa kuwa hakuna maadili kama mtoto hatalelewa kiroho, hawatoenda madrasa au shule ya Jumapili (Sunday school)

 “Nitumie fursa hii kuwaomba Waislamu na Wasio waislamu kurudi kwenye utamaduni wa kulea watoto. Habari ya kumwacha mtoto awe namna anavyokuwa sio jambo la sawa sawa, lazima tusimame imara turudi kukagua watoto wetu tujue wanasoma wapi, mwalimu wake ni nani na akitoka shule anapita wapi,” amesema Sheikh Kabeke. 

Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke akizungumza kwenye hafla fupi ya kupokea futari kutoka wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wiki iliyopita. Picha|Mariam John/ Nukta.

Serikali ina kigugumizi gani? 

Shekh huyo amehoji Serikali inapata kigugumizi gani cha kutengeneza mazingira ya kumfanya mtoto arudi nyumbani mapema ili apate elimu ya dini ambayo inaweza kutengeneza madili.

Kwa ushauri wake, anasema ni vema inapofika Saa 12 jioni watoto wote wawe majumbani mwao kwa ajili ya usalama zaidi.

Hii ni mara ya pili ndani ya wiki moja kwa kiongozi wa juu ndani ya mkoa wa Mwanza kusisitiza kuboresha malezi na kulinda watoto dhidi ya maadili hatarishi.  

Juma lililopita Waziri wa Ardhi nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabula amekiri kuwa suala la maadili kwa sehemu kubwa limemomonyoka na kutaja sababu ni wazazi kusahau wajibu wao wa kuwafundisha watoto maadili mema.

Waziri Mabula alisema zamani mtoto alikuwa anakanywa na yeyote kwenye jamii lakini kwa sasa hali ni tofauti ambapo mzazi hakubali mtoto wake kukanywa na mtu mwingine.

Mabula ataka kila mmoja kuwa mlinzi wa watoto

“Ombi langu ni kuwataka wazazi kurejea kwenye malezi ya zamani na turejee kwa mwenyezi Mungu na kila mzazi atimize wajibu wake wa malezi, kila jukumu ambalo mzazi alipaswa kulifanya alifanye yeye wengine wabaki kama sehemu ya kumsaidia,” amesema Waziri Mabula. 

Waziri Mabula amesema suala lililopo la ushoga linaenda kupoteza taifa na maadili ya Mtanzania kwa sababu mwanaaume kwa mwanaume au mwanamke kwa mwanaamke hawawezi kuwa na uzao wowote.

“Mwisho wa siku kizazi kilichopo kitapita na vijana waliopo wanaoingia kwenye huo mchezo maana yake hawatakuwa na watoto hivyo taifa litakuwa linaangamia lakini pia mwishoni tutapata adhabu ya mwenyezi Mungu kama ilivyokuwa kwa Sodoma na Gomola walivyofanya walikiuka maadili Mungu alichukuizwa akaona aiangamize,” amesema Mabul. 

Baadhi ya wazazi jijini Mwanza wamesema ipo haja ya kila mzazi kukaa chini na mtoto wake kumpa elimu ya kujikinga na vitendo hatarishi vinavyoweza kuchangia kujiingiza kwenye makundi yasiyofaa.

Grace Marco mkazi wa Mbugani jijini Mwanza amesema suala la utandawazi linachangia kwa kiasi kikubwa mmomonyoko wa maadili ambapo mtoto anaiga vitu vya nje na kuvifanyia majaribio nyumbani au kwa watoto wa Jirani yake.

Enable Notifications OK No thanks