Mjue Mkunga samaki ambaye yupo hatarini kutoweka
Mvuvi Hussein Kawango (mwenye kizibao chekundu) na mvuvi mwenzie katika ufukwe wa Kawe jijini Dar es Salaam. Kawango anasema kwa sasa ni nadra kumpata samaki aina ya Mkunga Chui baharini. Picha| Nuzulack Dausen.
- Baadhi ya aina ya Mkunga wakiwemo wanaoitwa “American Eel, Japanese Eel na European Eel’ wapo hatarini kutoweka duniani.
- Habari njema ni kuwa Mkunga Chui si moja ya aina zilizopo hatarini.
Dar es Salaam/Pangani. Baada ya kuzunguka kwa zaidi ya saa nne hivi baharini, Hussein Kawango anatoka na moja ya kiumbe adimu cha majini, Mkunga.
Kwa wageni wa viumbe bahari, wakimuona Mkunga huenda wakaanza kuchanja mbuga wakihisi ni nyoka, la hasha! Ni samaki kama wengine.
Baada ya kumuona samaki huyu baadhi ya watu waliokuwa wamekuja kununua samaki katika soko la samaki la Kawe jijini Dar es Salaam walianza kumsogelea na kushangaa umbo lake na madoa madogo madogo ya njano yaliyomfanya aonekane kama mwenye ngozi ya chui.
Kwa kuwa ni mrefu kidogo kama zaidi ya mita moja hivi, mvuvi Hussein Kawango alimviringisha samaki huyo aitwaye Mkunga Chui mkononi mwake kabla ya kumbwaga mezani na kuacha “watalii” wamshangae.
“Kichwa chake hakiliwi kwa sababu kinatisha,” anasema Kawango mkazi wa Kawe huku akicheka “ila sisi wavuvi tunakula kila kitu.”
Mkunga ama Eel kwa Kiingereza ni moja ya aina ya samaki mwenye umbo la nyoka ambaye baadhi ya tafiti za viumbe vya majini zinaonyesha kuwa kuna aina ambazo tayari zipo hatarini kutoweka ulimwenguni.
Samaki huyu anapatikana baharini na hata kwenye maji baridi.
Zinazohusiana:
- Umemejua unavyoweza kuzinufaisha hoteli Tanzania
- Kutana na vijana wanaoipa thamani nyumba yako kwa ‘taka
- Biashara ya hewa ukaa inavyoweza kuokoa mazingira Tanzania
Muungano wa Kimataifa wa Kuhifadhi Mali Asili (IUCN) unaonyesha kuwa aina za Mkunga zijulikanazo kama American Eel, European na Japanese Eel zipo hatarini kutoweka, jambo linalofanya wadau wa masuala ya uhifadhi viumbe bahari kuongeza nguvu kuwalinda.
Samaki huyu huwa na matamvua madogo katika sehemu yake ya mwili ambayo humwezesha kuogelea majini na jarida la Iscience linaonyesha kuwa Mkunga hupendelea zaidi kukaa katika matumbawe.
Kwa mujibu wa IUCN, Mkunga Chui ajulikanaye kwa kimombo kama ‘Spotted Snake Moray’ hali ya kiwango chake hakifahamiki kiasi cha kumuweka katika nafasi kuwa hayupo hatarini kutoweka yaani ‘Least concern’. Hadi sasa hakuna takwimu kuhusu aina hii ya mkunga.
Mkunga kama huyo, IUCN inaeleza kuwa hupatikana katika maeneo ya bahari ya Afrika Mashariki katika nchi za Tanzania, Kenya, Msumbiji, Ufilipino, Yemeni, India na mataifa mengine zaidi ya 20.
Pamoja na kuwa hali yake haifahamiki wavuvi wa Tanzania hasa Dar es Salaam na Pangani ambako Nukta Habari (www.nukta.co.tz) imetembelea wanasema ni adimu kidogo.
“Kwa wiki nzima ukiingia baharini kuvua unaweza kuwabahatisha wawili tu. Hawapatikani kirahisi hivi na baadhi wanamtumia kama dawa,” anasema Kawango.
Jarida la Iscience linaeleza kuwa aina hiyo ya Mkunga ipo pia hatarini kutokana na kuwepo kwa shughuli nyingi za kibinadamu katika matumbawe ambayo hukaa samaki hao.
“Shughuli za kibinadamu katika matumbawe huenda vikapunguza aina ya Mkunga Morays ambao wanapatikana katika maeneo karibu na watu,” unasomeka sehemu ya utafiti uliofanywa na watafiti 21 katika visiwa vya Carribean na kuchapishwa na jarida la Iscience.
Samaki huyo havuliwi kirahisi kama wengine mfano Tasi, Damudamu, Kolekole ama Kibua.
Kawango anaeleza kuwa Mkunga huvuliwa “kwa bahati mbaya” pale wanapokuwa wametega mitego yao kwa ajili ya samaki wengine basi naye hujikuta kanasa.
Soko la samaki huyo, Kawango anasema lipo lakini bei hutofautiana kutokana na mahitaji.
“Kwa wastani huwa tunamuuza kwa Sh8,000 hadi Sh9,000 lakini kuna wakati mahitaji yakiwa makubwa huwa anafikia Sh15,000,” anasema.
Samaki huyu huwa na matamvua madogo katika sehemu yake ya mwili ambayo humwezesha kuogelea majini na jarida la Iscience linaonyesha kuwa Mkunga hupendelea zaidi kukaa katika matumbawe. Picha| Nuzulack Dausen.
Kawango anasema Mkunga kwa sasa wapo wengi kidogo katika Mto Ruvuma ambako aliwahi kufanya shughuli za uvuvi miaka ya nyuma.
Licha ya wataalamu wa samaki kushauri samaki avuliwe akiwa amefikia umri stahiki ili kusaidia pia kuchochea kuzaliana lakini huyu aliyevuliwa na Kawango bado mdogo kwa umri jambo linaloweza kupunguza kiwango chao siku zijazo iwapo jitahada za makusudi hazitafanyika kuwalinda.
Mvuvi wa Pangani mkoani Tanga na mvuvi wa muda mrefu Ally Ally anasema kuwa kinachowaokoa Mkunga ni kwamba si moja ya samaki wawindaji (Hunting fish) na kwamba iwapo wangekuwa na tabia hiyo wangeathirika zaidi na taka bahari kama plastiki na wangekuwa wanavuliwa mara kwa mara.
“Ili kuhakikisha samaki hawa tunawalinda na wengine tunahitaji kutunza bahari kwa kuzuia uvuvi wa mabomu na sumu na utupaji wa plastiki baharini,” anasema Ally ambaye pia ni Mwenyekiti wa kikundi cha ulinzi wa fukwe (Beach Management Unit) ya Pangani Mashariki.
Makala hii imefadhiliwa na Shirika la WAN-IFRA-Press Freedom. WAN-IFRA haihusiki kwa namna yeyote na maudhui haya.