Biashara ya hewa ukaa inavyoweza kuokoa mazingira Tanzania

Daniel Samson 0601Hrs   Mei 29, 2021 Biashara
  • Inahusisha udhibiti wa uzalishaji wa gesi joto duniani.
  • Gesi hizo huchangia kuongeza joto la dunia na hewa ukaa.
  • Biashara hiyo inahusisha upandaji wa miti na kudhibiti shughuli za uzalishaji hewa ukaa.

Morogoro. Wataalam wa mazingira wameshauri watu binafsi, taasisi, mashirika na kampuni binafsi nchini Tanzania kufanya biashara ya hewa ukaa (carbon trading) ili kupunguza uchafuzi wa hewa na ongezeko la joto duniani jambo litakalosaidia kutunza mazingira.

Biashara ya hewa ukaa ni mfumo katika soko la dunia ambao unakusudia kupunguza gesi joto ambazo zinachangia kuongezeka kwa joto la dunia hasa ikiwemo hewa ukaa (carbondioxide) ambayo inatokana na shughuli za viwanda na uchomaji wa uoto na ukataji wa miti.

Mkurugenzi wa Kituo cha Kitaifa cha Kufuatilia Kaboni (NCMC) Prof Eliakimu Zahabu amesema kwa sasa dunia ikiwemo Tanzania inakabiliwa na athari nyingi za mabadiliko ya tabianchi ambayo yamesababishwa na kuongezeka kwa viwango vya hewa ukaa. 

Athari hizo ni pamoja na ongezeko la joto la dunia, ukame, mafuriko, ukosefu wa malisho kwa wafugaji na kuteteleka kwa shughuli za kilimo na uvuvi ambazo ni vyanzo vya mapato kwa wakulima. 

Prof Zahabu amesema njia mojawapo ya kukabiliana na ongezeko la hewa ukaa ni kuanzisha miradi ya biashara ya hewa hiyo katika maeneo mbalimbali Tanzania. Biashara hiyo inahusisha upandaji na utunzaji wa miti na kuweka mifumo inayodhibiti uzalishaji wa hewa ukaa katika shughuli mbalimbali katika sekta za kilimo, nishati, viwanda, miundombinu.

“Biashara ya hewa ukaa inasisitizwa duniani na Umoja wa Mataifa kwa sababu kiwango cha hewa ukaa kimeongezeka sana na kinatishia maisha ya binadamu na viumbe wengine wanaotegemea mazingira kuishi,” alisema Prof Zahabu katika warsha ya wanahabari kuhusu hewa ukaa iliyofanyika Mei 28, 2021 mkoani Morogoro.


Zinazohusiana: 


Baadhi ya miradi inayoanza kufanya biashara hiyo Tanzania ni pamoja na mradi wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam (DART) na Carbon Tanzania uliopo mkoani Arusha ambao unawahamasisha wananchi kutunza na kupanda miti katika maeneo yao ili kufyoza hewa akaa isisambae angani.

Hata hivyo, Prof Zahabu ambaye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) amesema biashara hiyo ili ifanikiwe inahitaji kutimiza vigezo vya kimataifa na kupata kibali cha nchi husika. 

“Miradi hii inahitaji rasilimali za kutosha zikiwemo fedha na kufanya utafiti wa kina ili ukidhi viwango vya kimataifa vinavyosimamia biashara hiyo,” amesema mtaalam huyo wa mazingira.

Biashara hiyo inasimamiwa na Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya Mkataba wa Kudhibiti Mabadiliko ya Hali ya Hewa (UNFCCC), ambapo kigezo kimojawapo kinachohitajika ni kuandika andiko litakalohusisha makundi yote yaliyopo katika mradi na kisha wahusika wakubaliwe na nchi husika kufanya mradi huo.

Related Post