Umemejua unavyoweza kuzinufaisha hoteli Tanzania

Daniel Samson 0311Hrs   Januari 21, 2019 Safari
  • Unasaidia kupunguza gharama za nishati inayotumika kwenye mifumo ya machemsho ya maji.
  • Nishati hiyo ni endelevu na inaweza kutumika wakati wote na kupunguza tatizo la kukatika mara kwa mara kwa umeme. 
  • Wadau washauri kufanyika kwa tathmini ya mnyororo wa thamani wa shughuli za uzalishaji zinazoendeshwa na nishati hiyo.

Dar es Salaam. Wamiliki wa hoteli nchini wameshauriwa kugeukia matumizi ya umemejua yatakayowasaidia kupunguza gharama za nishati na kuongeza mapato yatakanayo na vyumba vinavyotumiwa na wageni wanaotembelea hoteli hizo. 

Kwa mujibu wa utafiti ukuaji wa biashara ya hoteli (Hotels outlook: 2018-2022) uliofanywa na taasisi ya PwC unabainisha kuwa mapato ya vyumba vya hoteli yataongezeka zaidi mwaka huu na kufikia Dola za Marekani 252 milioni (zaidi ya Sh5.7 trilioni) ikiwa ni ongezeko la asilimia 4 ukilinganisha na mwaka uliopita. 

Sababu kuu ni kuimarika kwa usafiri wa ndege na hoteli zaidi ya saba zenye hadhi ya kimataifa zinazotarajiwa kufunguliwa chini ya kampuni za Rotana, Anantara, City Lodge, Hyatt Regency, Sarovar Portico na Ritz-Carlton. 

“Kwa sababu hii, PwC tunatarajia vyumba vya ziada 900 mwaka 2019 na 1,200 mwaka 2022 ikijumlisha na vyumba vilivyopo, vitaongezeka kutoka 7,700 hadi 8,900 mwaka 2022,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Hata hivyo, ongezeko la mapato hayo linaweza kufanikiwa ikiwa wamiliki wa hoteli wataweka mikakati ya kupunguza gharama za umeme kwa kuanza kutumia nishati jadidifu ikiwemo umemejua katika maeneo yao. 

Katibu Mtendaji wa Chama cha Wadau wa masuala ya Nishati Jadidifu (TAREA), Mhandisi Mathew Matimbwi amesema gharama kubwa za umeme kwenye hoteli zinatokana na uchemshaji maji yanayotumika kwa shughuli mbalimbali. 

Amesema umemejua unaweza kutengenezewa mfumo wa machemsho ya maji na kuwahakikishia wageni huduma bora wakati wote kuliko kutegemea umeme wa gridi ya Taifa. 

“Mionzi ya juu hutumika kwenye hoteli kuchemsha maji ambayo yanahitajika sana na wageni, hapa unaweza kupunguza gharama za umeme,” amesema Matimbwi wakati wa Mafunzo Maalum ya Wanahabari ya Nishati yanayofanyika jijini Dar es Salaam kwa siku nne.

Ufungaji wa mifumo ya machemsho ya maji inayoendeshwa na umemejua inaweza kupunguza gharama za uendeshaji hoteli nchini. Picha| Construction Review Online.

Akitolea mfano wa hotel ya Rombo Green View iliyopo Sinza jijini Dar es Salaam, amesema wamilikiwa wa hoteli hiyo wamefanikiwa kupunguza gharama za umeme kwa asilimia 60 kwasababu wamefunga mfumo wa machemsho ya maji unaendeshwa na paneli za sola. 

Mhandisi Matimbwi amesema  umemejua ni wa uhakika, endelevu na unaondoa changamoto ya kukatika kwa umeme kwa sababu mionzi ya jua inapatikana wakati wote.

Matumizi ya umemejua yanaweza kusaidia katika utunzaji wa mazingira na kuvutia watalii kukaa katika hoteli zinazopatikana karibu na hifadhi za Taifa. 

Kwa mujibu wa utafiti wa ufanisi wa nishati katika sekta ya hoteli uliochapishwa na kampuni ya Inorma UK Limited mwaka 2018 unaeleza kuwa ikiwa vyanzo vya uhakika vitatumika vitasaidia kuongeza ushindani wa hoteli, kukidhi mahitaji ya wageni, kupunguza gharama za matengenezo na kushindwa kwa mifumo ya umeme.


Zinazohusiana: 


Hata hivyo, Mtaalam wa matumizi endelevu ya nishati (PUE), Fredrick Mushi anasema kabla ya kuchagua aina ya nishati inayofaa kutumika katika maeneo ya uzalishaji zikiwemo  hoteli ni vema tathmini ya matumizi ya aina ya nishati na shughuli za uzalishaji ili kuepuka hasara inayoweza kutokea wakati wa uendeshaji mitambo ya umeme. 

Mwaka 2016, Serikali ilianzisha kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ya asilimia 18 kwa huduma za utalii jambo lililoongeza tozo cha viza kwa safari za kibiashara na gharama za uendeshaji hoteli nchini.

Related Post