Mjane aomba zuio la kutoondolewa kwenye nyumba
- Mahakama yataka umma kutambua kuwa mashauri yanayomhusu mjane huyo yako katika hatua tofauti za usikilizwaji.
Dar es Salaam. Mjane aliyefukuzwa kwenye nyumba anayodai kuwa ni mali ya mumewe amewasilisha maombi katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, akiomba zuio la muda la kutoondolewa kwenye nyumba hiyo iliyoko Kiwanja Na.819, Hati Na.49298, Msasani beach Dar es Salaam.
Maombi hayo madogo Na.24541/2025 yaliwasilishwa Septemba 25, 2025 na Alice Paschal Haule, ambaye pia ni msimamizi wa mirathi ya marehemu mumewe Justice Adeodatus Rugaibula aliyefariki Septemba 25, 2022.
Taarifa ya Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano wa Mahakama ya Tanzania Gerard Julius Chami iliyotolewa Septemba 25, 2025, imeeleza kuwa mashauri yanayomhusu mjane huyo yako katika hatua tofauti za usikilizwaji.
“Kwa mujibu wa taarifa ya Msajili Mkuu wa Mahakama, ni vyema umma ukatambua kuwa mashauri yote mawili yanayomhusu Alice yako katika hatua mbalimbali Mahakamani,” inaeleza taarifa ya Chami.
Kulingana na taarifa hiyo, shauri la awali lilifunguliwa Februari 11, 2025 na Alice kupitia Wakili wake Mwesigwa Muhingo dhidi ya Mohamedi Mustafa Yusufali, Kamishna wa Ardhi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali shauri hilo Na.3143/2025 lilidai nyumba hiyo ni mali ya marehemu.
Hata hivyo, wakati wa Kongamano la Mwisho (Final Pre-trial Conference) Septemba 19, 2025, Wakili Muhingo aliomba kuliondoa shauri kwa ruhusa ya kulifungua upya ili kumuongeza Msajili wa Hati kama mdaiwa na mahakama iliridhia ombi hilo.
“Baada ya shauri la awali kuondolewa kwa ruhusa, Wakili wa Alice aliwasilisha upya maombi. Lakini hati ya madai aliyowasilisha ilibainika kuwa na mapungufu ya kisheria, hivyo hakusajiliwa hadi alipofanya marekebisho na hatimaye shauri jipya kusajiliwa Septemba 24, 2025 kwa Na.24396/2025,” amesisitiza Chami katika taarifa yake.
Siku moja baadaye, Septemba 25, 2025, Alice aliwasilisha pia maombi madogo ya zuio (Na.24541/2025) akitaka kutoondolewa kwenye nyumba inayodaiwa kuwa ya marehemu mumewe huku shauri jingine likiendelea kupitia hatua zake za kisheria.
Kwa mujibu wa Msajili Mkuu wa Mahakama mashauri yote mawili yako katika hatua mbalimbali na yataendelea kusikilizwa kwa mujibu wa taratibu za kisheria.
Taarifa hii ya mahakama inakuja siku tatu baada ya vyombo mbalimbali vya habari kuripoti tukio la mwanamke kutolewa kwenye nyumba kwa nguvu ambalo lilitokea mchana wa Septemba 23, 2025.
Baada ya kutokea kwa tukio hilo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila alitembelea eneo hilo Septemba 24, 2025 na kusitisha shughuli zote katika eneo hilo mpaka pale uchunguzi utakapo kamilika.
Latest