Mahakama Kuu kutoa uamuzi mdogo kesi ya mgawanyo wa mali Chadema Septemba 29, 2025
- Ni baada ya kusikiliza hoja na mapingamizi ya pande zote mbili.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam inatarajiwa kutoa uamuzi mdogo kuhusiana na maombi ya nyaraka katika kesi ya mgawanyo wa mali ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia bodi ya wadhamini na katibu mkuu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wakili wa Bodi ya Wadhamini ya Chadema, Wakili Hekima Mwasipu, hatua hiyo inakuja baada ya Mahakama hiyo chini ya Jaji Hamidu Mwanga kumaliza kusikiliza mapingamizi yaliyowekwa na wadau.
Wakili Mwasipu ameeleza kuwa upande wa madai ukiongozwa na aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Said Issa Mohamed na wenzake wawili wamewasilisha maombo mahakamani hapo wakitaka wadaiwa wawapatie nyaraka kadhaa muhimu za kiofisi ikiwemo muhtasari na ajenda za vikao vya Bodi ya Wadhamini, ajenda za Kamati Kuu, Sekretarieti, Kamati Maalum ya Kamati Kuu Zanzibar na Sekretarieti ya Kamati Maalum Zanzibar.
Nyaraka nyingine ni pamoja na taarifa za fedha, taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), nyaraka zote hizo ni za kuanzia mwaka 2019 hadi 2024, jambo ambalo Chadema inalipinga vikali.
“Tumeiambia Mahakama kwamba tunapinga na tumewasilisha maombi, wasipewe nyaraka hizo kisheria” amesema Wakili Mwasipu.
Aidha, itakumbukwa kuwa katika kesi ya msingi inayoendelea mahakamani hapo, Said Issa Mohamed na wenzake wanadai kuwa chama hicho kimekuwa kikiitenga Zanzibar katika shughuli zake na hakizingatii usawa wa mgawanyo wa mali na rasilimali fedha.
Sambamba na hilo wanadai kuwa chama hicho kupitia viongozi wake kimekuwa kikitoa kauli zinazoashiria udini, ukosefu wa usawa wa kijinsia na viashiria vya kuvuruga muungano, jambo ambalo ni kinyume na Katiba ya Chadema, Katiba ya Nchi na Sheria ya Vyama vya Siasa Nchini.
Hata hivyo, madai hayo yamekanushwa na Chadema wakidai kuwa kesi hiyo inatumika kupotosha nia yake ya kusaka mageuzi ya uchaguzi na kudhoofisha demokrasia nchini.