Serikali yaingilia kati sakata la mjane kutupiwa vitu nje Dar
- Yataka haki itendeke bila kujali hali za walalamikaji.
Arusha. Siku moja tangu kuripotiwa tukio la mjane aliyefukuzwa kwenye nyumba anayodai ni ya mume wake, Serikali imeunda tume ya wataalamu kuchunguza madai hayo ili haki itendeke.
Mchana wa Septemba 23, 2025 mwanamke mjane aliyejitambulisha kwa jina la Alice Haule alidai kuvamiwa nyumbani kwake na watu waliodai kumdai marehemu mume wake Sh150 milioni.
Watu hao waliodai kuwa na barua ya kibali kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni walimuondoa kwa nguvu Alice na familia yake pamoja na wapangaji waishio katika nyumba hiyo kwa jambo lililotafsiriwa kuwa ni uvunjfu wa sheria.
Baada ya kutokea kwa tukio hilo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila ametembelea eneo hilo leo Septemba 24, 2025 akisitisha shughuli zote katika eneo hilo mpaka pale uchunguzi utakapo kamilika.
“Mahali hapa kisifanyike kitu kingine chochote mpaka vyombo vya usalama kwa uharaka mkubwa vijiridhishe haya machache ambayo yamelalamikiwa, moja ni umadhbuti wa nyaraka na masuala haya yote kwa ujumla wake,” amesema Chalamila.
Kwa mujibu wa maelezo ya Chalamila nyumba hiyo ilikuwa inamilikiwa na Justice Lughaibula pamoja na Alice Haule kuanzia miaka ya 2007/2008 mpaka mwaka 2011 ambapo iliuzwa kwa mtu aliyemtambulisha kwa jina moja la Mohamed Mustapha.
Mwaka mmoja baadae Alice alienda katika Wizara ya Ardhi kwa ajili ya kuzuia uuzwaji wa nyumba huo lakini akakuta tayari zoezi la uuzwaji wa nyumba limekamilika hivyo madai yake yakashindwa kufika mahakamani.
Kutokana na maelezo hayo Chalamila ameunda kamati maalum itakayohusisha maafisa kutoka Wizara ya Ardhi, Tume ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Jeshi la Polisi watakaofuatilia madai hayo kwa kina ili kugundua ukweli.
Aidha, Chalamila amewataka wataalamu hao pamoja na walalamikaji watakutana ofisini siku ya Ijumaa Septemba 26, 2025 ili kufanya mazungumzo na kufikia muafaka asikisistiza kuwa haki itapatikana bila kujali hali ya walalamikaji.
“Ujane isiwe sababu ya kukanyaga haki kama mama huyu itabainika kweli hana haki, haki itafuata utaratibu wake bila kigezo cha ujane, kama bwana Mustapha ana haki, haki itafuata mkondo wake bila kujali ni maskini au ni tajiri…
…Ninachotaka kuhitimisha ni kwamba ujane, ulemavu,ufui, unene, kutkuona sio vigezo vninavyokupelekea kuvunjasheria au kujichukulia sheria mkononi.
Latest



