Mitandao ya kijamii inavyoweza kuwa fursa au kikwazo cha kupata ajira
- Wataalam wanasema mtu anaweza kukosa nafasi ya ajira kwa sababu ya anachopost kwenye mitandao ya kijamii.
- Wanashauri kuchapisha mambo yatayoonyesha ujuzi ulionao tofauti na taaluma uliyonayo.
Dar es salaam. Miaka ya hivi karibuni mitandao ya kijamii imekuwa sehemu muhimu ya maisha ya waliowengi ikiwemo vijana ambao huitumia kwa ajili ya shughuli mbalimbali.
Ripoti ya takwimu za robo ya nne ya mwaka 2025 za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaonesha watumiaji wa intaneti wameongezeka hadi kufikia milioni 58.1 kutoka milioni 40 iliyorekodiwa mwaka 2024.
Kwa idadi hiyo, ni sawa na kusema watumiaji milioni 18.1 wa intaneti waliongezeka nchini Tanzania wakiitumia kuperuzi katika majukwaa mbalimbali mtandaoni ikiwemo mitandao ya kijami kama Instagram, Facebook na TikTok.
Wapo wanaoitumia kujiburudisha, kujiongezea maarifa, kujenga utambulisho binafsi (personal brand) huku wengine wakiutumia kupiga soga na kufatilia mambo yasiyo ya maadili ambayo wakatii mwingine yanaweza kuwa kiwazo cha kushindwa kupata ajira.
Afisa Vipawa na mtaalamu wa masuala ya uajiri kutoka Niajiri Plattform, Mary Kopwe, ameiambia Nukta Habari kuwa waombaji wengi wa kazi huzingatia sana kuandaa wasifu (CV) na kujiandaa kwa usaili, lakini husahau kuwa taswira yao mtandaoni ni sehemu ya tathmini muhimu kwa baadhi ya waajiri.
“Anaweza kuwa na sifa zote zinazohitajika, lakini akashindwa kupata kazi kwa sababu ya kile alichowahi kuposti,” amesema Kopwe.
Anaongeza kuwa waajiri wengi kwa sasa hufanya uchunguzi wa akaunti za mitandao ya kijamii za waombaji ili kuthibitisha tabia, maadili na mienendo yao kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho.
Hali hii inaendana na mwenendo wa sasa ambapo vijana wengi hutumia mitandao ya kijamii bila mipaka, wakichapisha maudhui bila kuzingatia athari za muda mrefu.
Baadhi hujihusisha na mijadala ya matusi, siasa zenye misimamo mikali au hata kushiriki maudhui yasiyoendana na maadili ya kitaaluma. Wengine huona kama ni sehemu ya uhuru wa kujieleza, bila kutambua kuwa waajiri wanaweza kuona hayo kama dalili ya ukosefu wa nidhamu, busara au uaminifu.
“Namna mbavyo umejiweka na kuji ‘position’ kwenye hiyo mitadao ni kitu cha muhimu sana kwa sababu mwajiri anaweza akakushusha kulingana na ulivyojiweka,” anasisitiza Kopwe.
Upande mwingine wa sarafu
Hata hivyo, Kopwe anabainisha kuwa upande mwingine wa sarafu, mitandao ya kijamii ni mgodi wa dhahabu ambao mtu anaweza kutumia kuvutia waajiri na fursa.
Anaeleza kuwa, vijana wananafasi ya kutumia mitandao ya kijamii kwa kupanua wigo wa fursa hasa katika kujitangaza kitaaluma, kuonesha ujuzi na kujenga mahusiano na watu mbalimbali (networking) jambo linaloweza kufungua milango ya ajira na fursa.
“Unaweza ukachapisha taarifa kama ukihudhuria mafunzo, ukipata cheti cha mafunzo fulani au kushiriki hata kwenye mikutano. Hii pia inasaidia kuonyesha ujuzi wa ziada uliokuwa nao zaidi ya taaaluma uliyonayo,” ameshauri Kopwe.
Pamoja na umuhimu wa mitandaoo hiyo katika uchaguzi wa mwisho wa nafasi za ajira, Shirika la Kazi Duniani (ILO) linabainisha kuwa mitandao hiyo inaweza kuwa nyenzo bora kwa vijana wanaotafuta ajira.
Mitandao ya kijamii inaweza kuwasaidia vijana Kusanya taarifa kuhusu kampuni wanazotaka kufanya nazo kazi na kujenga mtandao na watu wenye ushawishi kabla hata ya kupata uzoefu wa kazi,” imesema ILO.
Latest