Fahamu mitandao ya kijamii iliyotumiwa zaidi Tanzania 2025

December 22, 2025 12:08 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Kufikia Septemba 2025, Watanzania milioni 56.3 wameunganishwa na huduma ya intaneti huku takriban Watanzania milioni 26.9 wakirekodiwa kutumia simu janja.

Dar es Salaam. Mitandao ya kijamii ni miongoni mwa nyenzo za mawasiliano zinazotumiwa zaidi siku za hivi karibuni, ikisaidia kuwaunganisha watu kutoka maeneo mbalimbali, kubadilishana mawazo, taarifa na uzoefu kwa haraka na kwa urahisi.

Pamoja na kuwaungaisha watu, mitandao hiyo imekuwa fursa kwa vijana kujiajiri na kutunisha mifuko yao kiasi cha kufanya baadhi zao kutumia muda mwingi zaidi katika mitandao hiiyo na kusahau kujichanganya na wanajamii.

Ripoti ya takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) za robo ya tatu (Juni -Septemba)  ya mwaka 2025 inabainisha kuwa Watanzania milioni 56.3 wameunganishwa na huduma ya intaneti kufikia Septemba mwaka huu.

Kati ya watumiaji hao, milioni 26.9 waliunganishwa kupitia simu janja (Simu a rununu 58,850,493), (Modemu 743,376), (vishkwambi 544,888) pamoja na magari (8,539).

Nukta Habari imekuandalia orodha ya mitandao mitano iiyotumika zaidi kwa mwaka 2025 kwa mujibu wa DataReportal

Facebook kinara wa matumizi

Kwa vijana wa zamani watakumbuka kuwa facebook ilikuwa mtandao wa kwanza maarufu kutumiwa zaidi nchini Tanzania ukijizolea umaarufu hata kwa watu ambao taratibu wanaanza kukaribia ‘kula chumvi nyingi’.

Hata hivyo, bado Facebook imeendelea kushika kinara ikiwa na watumiaji milioni 6.79 ikiwaacha nyuma washindani wake ambao wanaaminika kupendwa zaidi na kizazi kipya yaani Gen Z.

Idadi hiyo ya watumiaji wa Facebook ni sawa na kusema asilimia 9.7 ya Watanzania wote waliopo nchini kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Watumiaji hao wa Facebook waliongezeka kwa asilimia 19.5 kati ya mwaka 2024 na mwanzoni mwa mwaka 2025. 

Instagram 

Instagram ni mtandao wa kijamii unaolenga zaidi matumizi ya picha na video, na umekuwa chaguo maarufu sana miongoni mwa Watanzania. Watumiaji wengi huutumia kuonyesha maisha yao ya kila siku, kushirikisha matukio muhimu.

Takwimu za DataReportal zinabainisha kuwa mtandao huo kwa mwaka 2025 uliuwa na watumiaji milioni 3.7 wakiongezeka kwa asilimia 5.7 kutoka idadi ya watumiaji iliyorekodiwa mwaka uliopita.

Mbali na mtandao huo kutumiwa kwa ajili ya mawasiliano, umekuwa ukitumiwa pia kukuza biashara kama anavyobainisha Cletus Mboya (20) anayejihusisha na uuzaji wa simu kariakoo, Dar es Salaam. 

“Kwa siku, wateja ninaopata (kupitia mtandao wa instagram)  ni wengi zaidi kuliko wale wanaoniona kwa macho wakipita dukani,” anaeleza Mboya.

Linkedin

Kwa wamiliki wa kampuni, wajasiriamali na wanaotafuta ajira huenda wakawa wameutumia zaidi mtandao wa Linkedin na kuufanya kuwa miongoni mwa mitandao yenye idadi kubwa ya watumiaji mwaka 2025.

Meta inabainisha kuwa watu milioni 1.5 sawa na asilimia 2.2 ya Watanzania walitumia Linkedin mwanzoni mwa mwaka 2025, idadi inayodhihirisha ongezeko la uelewa wa matumizi ya mitandao huo kitaaluma. 

Messenger

Messenger, jukwaa hili linaendelea kutumika zaidi kama chombo cha mawasiliano ya haraka kati ya watu binafsi, familia na wafanyabiashara.

Takwimu zinaonyesha kuwa Messenger ilikuwa na watumiaji takribani milioni 1.3 nchini. Kati ya watumiaji hao, wanawake walikuwa asilimia 37.1 na wanaume asilimia 62.9.

Watumiaji wengi hutumia Messenger kubadilishana ujumbe wa maandishi, sauti na picha kwa wakati halisi, kurahisisha mawasiliano ya kila siku bila hitaji la kupiga simu. 

X jukwaa la mijadala 

Licha ya kuwa na idadi ndogo ya watumiaji ikilinganishwa na mitandao mingine, mtandao wa X (zamani Twitter) umeendelea kuwa jukwaa lenye ushawishi mkubwa Tanzania katika uundaji wa hoja na mjadala wa umma, hasa miongoni mwa wanahabari, wanasiasa, wachambuzi na watumiaji wanaopenda maudhui ya habari na hoja.

Mpaka kufikia mwanzoni mwa mwaka 2025, X ilikuwa na watumiaji 666,000, ikiongezeka kwa 7.2, wanaume wakiwa ni  asilimia 87.7 ya na wanawake asilimia 12.3.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks