Mikakati ya Tanzania kuwakinga watu na uvutaji wa sigara usio wa hiari
- Utatenga maeneo maalum ya kuvutia sigara na kuweka vibao.
- Watu kupewa elimu kuhusu madhara ya uvutaji wa sigara.
Mwanza. Uvutaji sigara ni moja ya sababu zinazochangia watu kupata saratani za koo, kinywa na moyo na kuibebesha Serikali na familia mzigo mzito wa matibabu kwa watu waliopata magonjwa hayo.
Kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO) zinabainisha kuwa zaidi ya watu milioni 7 hufariki duani kutokana na matumizi ya tumbaku na asilimia 80 ya watumiaji hao wanaishi kwenye nchi zenye kipato cha chini.
Kutokana na changamoto hiyo, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imeanzisha mpango kazi wa miaka mitatu kuanzia mwaka 2021 hadi 2024 wa kupambana na matumizi ya sigara kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali zikiwemo taasisi za elimu.
Kupitia mango huo, TMDA itaweza kufanya tafiti zitokanazo na athari za matumizi ya tumbaku na bidhaa zake ili kujua hali halisi iliyopo nchini kuliko kutegemea za WHO pekee.
Kaimu Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa, Mtani Njegere akizungumza na waandishi wa habari, leo Marchi 4, 2022 amesema kupitia mpango kazi huo, watatoa elimu kwa wananchi kuacha kuvuta sigara ya aina yoyote kwenye mkusanyiko wa watu ili kupunguza athari zinazosababishwa na moshi.
“Mpango kazi ni wa miaka mitatu tayari zoezi limeshaanza na hadi leo tumefikia maeneo tofauti 58 kuwakumbusha kuweka vibao vinavyozua uvutaji sigara maeneo hayo na kuhamasisha kujenga chemba ya kuvutia ili kupunguza madhara ambayo kwa sasa ni makubwa,” amesema Njegere.
Taasisi zilizofikiwa ni pamoja na vyuo, stendi za mabasi, mialo, viwanda na vyombo vya habari, lengo likiwa ni kutoa uhamasishaji kwa wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya uvutaji sigara.
Mamlaka hiyo inahamasisha kuweka ving’ora kwenye maeneo ya kuvutia ili mvutaji anapowasha sigara king’ora kitoe ishara kwa watu waliopo kuondoka ili madhara yasiwakumbe.
“Tafiti za WHO zinaonyesha kuwa matumizi ya tumbaku ni kisababishi cha kifo namba mbili ukiacha Ukimwi hivyo tunaweka kampeni kwenye maeneo maalum ya kuvutia sigara kupunguza madhara hayo,” amesema Njegere.
Baadhi ya wafanyaazi wa Mamlaka ya dawa na vifaa tiba (TMDA) wakionyesha alama za vibao vinavyotakiwa kubandikwa kwenye maeneo ya wazi na umma ili kuzuia uvutaji sigara hadharani unaoweza kusababisha madhara kwa watu wengine wasiokuwa watumiaji wa tumbaku. Picha|Mariam John.
Kwa mujibu wa Njegere amesema zipo tafiti zingine zlifanywa miaka ya nyuma katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Dar es Salam ambazo zinaonyesha athari za moshi wa sigara haziishii kwa watumiaji pekee lakini zinaathiri hata wasiotumia ikiwa watakaa karibu na mazingira ya wavutaji.
Baadhi ya wananchi ambao walizungumza na Nukta habari walikiri kuwa kwa sasa hakuna maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kuvutia sigara na kuwa wavutaji huvuta popote.
Elia Jackson, mkazi wa jiji Mwanza amesema elimu inayotolewa na TMDA itapunguza kwa kiasi fulani uvutaji usiozingatia kanuni za afya hivyo suala la kuweka vibao vya kuzuia uvutaji kwenye maeneo na kujenga chemba maalum utasaidia.
Happy Masala amepongeza juhudi hizo na kueleza kuwa zitasaidia kuwakumbusha wavutaji kutowabugudhi wengine.
“Kwa Kweli moshi wa sigara ni kero na ni hatari hivyo wavutaji watajua maeneo yapi sahihi kwao kuvutia na watapunguza madhara kwa wengine,” amesema Happy.
Soma zaidi:
Sheria ya Usajili wa Bidhaa za tumbaku ya mwaka 2003 (Tobacco product registration act 2003) inakataza watu kuvuta sigara katia maeneo ya umm na imeainishwa adhabu zinazotakiwa kumfikia mtu atakayevuta sigara hadharani ikiwa ni pamoja na faini isiyozidi Sh500,000 na kifungo kisichozidi miaka mitatu jela.
Licha ya hayo yote kuwa wazi, matumizi ya tumbaku na bidhaa zake hadharani bado yamekuwa yakiendelea na kuwa chanzo cha kuongezeka kwa vifo vinavyotokana na uvutaji wa sigara usiokuwa na hiari.
Ripoti ya Utafiti wa Tumbaku kwa Watu Wazima Duniani (GATS) wa mwaka 2018 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Shirika la Afya Duniani (WHO) na Ofisi Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS) imeeleza kuwa watu huvuta sigara bila hiari katika maeneo mbalimbali ikiwemo vyuoni, kumbi za starehe na nyumbani.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu wengi zaidi (watu wazima milioni 3.8) wanaripotiwa kuvuta sigara bila hiari wakiwa katika kumbi za starehe za usiku na baa.
Latest