Utupaji sigara hovyo unavyoathiri binadamu, viumbe wa baharini

Mwandishi Wetu 0224Hrs   Februari 05, 2022 Chati & Data
  • Kampeni maalum yazinduliwa kukabiliana na vitendo vya utupaji sigara hovyo.

Dar es Salaam. Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira UNEP limezindua kampeni ya kujenga uelewa na kuchukua hatua za kutunza mazingira na afya za wananchi kutokana na vipande vidogo vidogo vya plastiki katika machujio ya sigara.

UNEP inashirikiana na Sekretarieti ya Mkataba wa Mfumo wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani juu ya Udhibiti wa Tumbaku (WHO FCTC) katika kampeni hiyo itakayofanyika mtandaoni na inayohusisha kutumia watu maarufu na vijana wachechemuzi wa masuala ya mazingira mitandaoni na mabalozi wa hiyari.

Ushirikiano huo unawezeshwa kupitia kampeni ya UNEP ya “Bahari Safi”, muungano wa kimataifa unaojumuisha nchi 63 zinazojitolea kukomesha uchafuzi wa plastiki baharini.

Mkuu wa Uhamasishaji wa Umma wa UNEP Atif Butt amesema, “Sekretarieti ya WHO FCTC ina utaalamu wa kiufundi wa athari za bidhaa za tumbaku siyo tu kwa afya ya binadamu bali pia kwa mazingira, kwa kujiunga nasi  katika uanzishaji wa Bahari Safi bila vipande vya plastiki, tunalenga kuangazia jinsi afya yetu inavyohusishwa na ile ya sayari yetu."

Kila mwaka, tasnia ya tumbaku huzalisha sigara trilioni 6 zinazotumiwa na wavutaji sigara bilioni 1 duniani kote. 

Sigara hizi zina vichujio vinavyojumuisha hasa plastiki ndogo zinazojulikana kama nyuzi za acetate za selulosi. Sigara zinayotupwa hovyo vitako yake ( Vichungi)  huvunjika kutokana na sababu mbalimbali kama mwanga wa jua na unyevunyevu na hapo ndiyo hutoa plastiki ndogo pamoja na kemikali nyingine nyingi, hivyo kuathiri afya na huduma za mifumo ikolojia.

Mkuu wa Sekretarieti ya WHO FCTC, Adriana Blanco Marquizo amesema, “Nawaomba nyote kujiunga na kampeni hii. Hebu sote tufanye sehemu yetu kuhakikisha bahari yetu pamoja na wakazi wake wote  wanalindwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.”

Ushirikiano huu unaashiria hatua muhimu ya kwanza kuelekea kupata  suluhisho la athari za kiafya na kimazingira za plastiki ndogo kwenye vichungi vya sigara.

Related Post