Tanzania kufanya mapitio sheria, kanuni zinazosimamia uvutaji sigara

June 1, 2021 11:50 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Mapitio hayo yanatarajiwa kufanywa Julai mwaka huu.
  • Hiyo itasaidia kuongeza nguvu ya utekelezaji wa sheria zinazosimamia uvutaji wa sigara mwenye maeneo ya umma.
  • Pia itasaidia kupunguza madhara wanayopata watu wanaovuta sigara bila hiari.

Dar es Salaam. Ili kudhibiti madhara ya uvutaji wa sigara usio wa hiari, Serikali imesema itaanza kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kufanya mapitio ya sheria na kanuni zinazosimamia zao la tumbaku na uvutaji wa sigara katika maeneo ya umma ili kuwalinda watu wasiotumia bidhaa hizo.

Hivi karibuni, Nukta Habari (www.nukta.co.tz) ilichapisha ripoti maalumu ya kuonyesha hatari inayowakumba watu wanaovuta sigara bila hiari ikiwemo kupata magonjwa ya moyo kwa kuvuta moshi wa sigara kwa kukaa karibu na watu wanaovuta sigara.

Ripoti ya Utafiti wa Tumbaku kwa Watu Wazima Duniani kwa upande wa Tanzania (GATS) ya mwaka 2018 imeeleza kuwa watu huvuta sigara bila hiari katika maeneo mbalimbali ikiwemo vyuoni, kumbi za starehe na nyumbani.

Kati ya maeneo yaliyotajwa, watu wengi zaidi (watu wazima milioni 3.8) wanaripotiwa kuvuta sigara bila hiari wakiwa katika kumbi za starehe za usiku na baa.

Sheria zitakazoangaliwa ni pamoja na Sheria ya Usajili wa Bidhaa za tumbaku ya mwaka 2003. Picha| Mtandao.

Mkurugenzi Msaidizi Magonjwa yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk James Kiologwe ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz)  amesema ifikapo mwezi Julai mwaka huu, Serikali inalenga kufanya mapitio kuona changamoto zilizopo katika sheria na kanuni mbalimbali zinazosimamia matumizi ya bidhaa za tumbaku ili zirekebishwe.

“Serikali tunapanga kufanya mapitio mwezi Julai mwaka huu kuona maeneo yenye changamoto tuyafanyie marekebisho,” amesema Dk Kiologwe.

Sheria zitakazoangaliwa ni pamoja na Sheria ya Usajili wa Bidhaa za tumbaku ya mwaka 2003 (Tobacco product registration act 2003).

Katika sheria hiyo, zimeainishwa adhabu zinazotakiwa kumfikia mtu atakayevuta sigara hadharani ikiwa ni pamoja na faini isiyozidi Sh500,000 na kifungo kisichozidi miaka mitatu jela.


Soma zaidi:


Licha ya hayo yote kuwa wazi, matumizi ya tumbaku na bidhaa zake hadharani bado yamekuwa yakiendelea na kuwa chanzo cha kuongezeka kwa vifo vinavyotokana na uvutaji wa sigara usiokuwa na hiari.

Amesema wakati Serikali ikijipanga kurekebisha sheria na kununi, inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya uvutaji wa sigara kwenye maeneo ya umma na namna ya kuwakinga wale wasiovuta. 

Dk Kiologwe amesema viongozi wa serikali za mitaa wana wajibu wa kulinda afya za wananchi wao ikiwa ni pamoja na kuwaepusha na usumbufu wa moshi wa sigara kutoka kwa wavutaji.

“Moshi wa sigara siyo jambo ambalo kuna mtu hahusiki. Wajibu wa Serikali ni kutoa elimu ikianzia kwa wananchi na wasimamizi au wamiliki wa kumbi za starehe kuhakikisha usalama wa mtu dhidi ya bidhaa za tumbaku popote anapokuwa,” amesema Dk kiologwe.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inakadiriwa kuwa  ifikapo mwaka 2030, vifo vinavyotokana na matumizi ya tumbaku na bidhaa zake vitaongezeka kufikia milioni 8 kwa mwaka duniani kote. 

“Kila mwaka watu 600,000 hufariki kutokana na kuvuta moshi wa wavutaji kwa kuwa karibu na wavutaji ambapo kati yao asilimia 28 ni watoto,” ameeleza Waziri wa wizara hiyo, Dk Dorothy Gwajima katika tamko la Serikali kuhusu Siku ya Kutotumia Tumbaku Duniani Mei 31, 2021.

Enable Notifications OK No thanks