Mfumuko wa bei wasalia 4.3%, usafiri bado pasua kichwa
- Usafiri umeendelea kuwa eneo lenye ongezeko kubwa zaidi la bei kwa mwaka, ambapo mfumuko wake ulifikia ongezeko la asilimia 14.0 Septemba 2026, kulinganisha fahirisi ya Septemba 2025.
Dar es Salaam. Mfumuko wa bei nchini kwa mwaka unaoishia mwezi Septemba 2026 umeendelea kusalia asilimia 4.3 kwa mwezi wa pili mfululizo ikichangiwa na kupata kwa gharama za usafiri, nishati na baadhi ya vyakula.
Mfumuko wa bei ni hali ya kupanda kwa bei za huduma na bidhaa katika uchumi kwa kipindi fulani.
Kwa lugha rahisi, ni hali ambayo fedha ile ile ambayo mwananchi aliweza kununua kiasi fulani cha bidhaa, inanunua bidhaa nyingi au chache zaidi baada ya kipindi fulani kulinganisha na awali.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) iliyotolewa Oktoba 8, 2026, inabainisha kuwa kiwango hicho ni cha wastani.
“Ingawa farhisi za bei za Taifa kwa ujumla ziliongezeka katika kipindi hicho, kiwango cha mfumuko wa bei wa mwaka kilibadilika kwa kiwango kidogo kiasi, huku kiwango cha juu zaidi cha asilimia 4.3 kikirekodiwa kati ya Agosti na Septemba 2026,” imesema NBS.
Licha ya kiwango cha mfumuko wa bei kutobadilika ndani ya miezi miwili mfululizo, bado kinasalia kuwa kiwango cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa ndani ya miezi 40 tangu Aprili 2023.
Usafirishaji, mafuta bado pasua kichwa
Kwa upande wa matumizi, usafiri umeendelea kuwa eneo lenye ongezeko kubwa zaidi la bei kwa mwaka, ambapo mfumuko wake ulifikia ongezeko la asilimia 14 Septemba 2026, kulinganisha fahirisi ya Septemba 2025.
Nishati, mafuta na huduma za matumizi ya nyumbani pia ziliendelea kuwa na ongezeko kubwa, huku mfumuko wa kundi hilo ukifikia asilimia 7.8 jambo ambalo ndilo linachagiza kuongezeka kwa gharama za usafirishaji na bidhaa nyingine ikiwemo chakula.
Kwa upande wa chakula, mfumuko wa bei uliongezeka hadi asilimia 3.9 Septemba kutoka asilimia 3.7 Agosti, sawa na ongezeko la asilimia 0.2.
NBS imesema ongezeko hilo lilichangiwa na kupanda kwa bei za baadhi ya vyakula, ikiwemo viazi vitamu, mihogo mibichi, ndizi za kupikia na unga wa mihogo.
Mbali na chakula, bei za baadhi ya bidhaa za matumizi ya nyumbani pia zilipanda, huku saruji, na gesi yakupikia zikitajwa miongoni mwa bidhaa zilizoongezeka bei.