Mfumuko wa bei wapaa kwa asilimia 0.1 Agosti
- Mfumuko wa bei wafikia asilimia 4.3 kwa mwaka ulioishia Agosti 2026 kutoka asilimia 4.2 Julai.
- Bei wa vyakula washuka hadi asilimia 3.7 kutoka asilimia 4.1.
Dar es Salaam. Kasi ya ongezeko la bei za bidhaa na huduma nchini imeongezeka kwa asilimia 0.1 kwa mwaka ulioishia Agosti 2026 ikichangiwa na kupaa kwa gharama za habari na mawasiliano.
Hii inamaanisha kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2026 imeongezeka na kufikia asilimia 4.3 ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi uliopita.
Taarifa ya mwenendo wa mfumuko wa bei nchini iliyotolewa Septemba 8, 2026 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imebainisha kiwango cha mfumuko wa bei Agosti bado kipo ndani ya wastani.
“Kwa ujumla kati ya mwezi Agosti 2025 na Agosti 2026, zikiongezeka kutoka 119.77 hadi 124.93. Katika kipindi hicho kiwango cha Mfumuko wa Bei kiliendelea kuwa katika kiwango cha wastani, kikiwa kati ya asilimia 3.2 na asilimia 4.3,” imesema NBS.
Uchambuzi uliofanywa na Nukta Hababri umebaini kuwa kiwango cha Agosti 2026 ndio cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa ndani ya miaka mitatu iliyopita.
Kiwango cha juu zaidi cha mfumuko wa bei kilichorekodiwa ndani ya kipindi hicho kilikuwa asilimia 4.0 Mei 2023. Katika miezi iliyofuata, kiwango hicho kiliendelea kupanda na kushuka, kikibadilika ndani ya wastani wa kati ya asilimia 3.9 na asilimia 4.2.
Kuanzia Agosti 2023 kurudi nyuma kiwango hicho kilipaa hadi kufikia asilimia 4.9 Oktoba, 2022.