Dhana tano potofu kuhusu matumizi ya friji nyumbani
- Dhana hizo ni pamoja na kuweka kila chakula na kutosafisha ndani na nje ya friji.
- Zimekuwa zikiwagharimu watu kwa sababu kifaa hicho kupunguza ufanisi wake.
- Watumiaji wanashauriwa kufuata maelekezo ya matumizi ya friji kila wanunuapo.
Katika nyumba nyingi za mjini, friji ni miongoni mwa vifaa muhimu vya kielektroniki ambavyo huwezi kuvikosa nyumbani au maeneo yanayohusisha shughuli za kibinadamu.
Matumizi yake hutofautiana, licha ya kuwa kazi yake kubwa ni kupoza na kugandisha vyakula na vimiminika ikiwemo maji.
Pamoja na umuhimu wake, kumekuwepo na dhana mbalimbali potofu juu ya matumizi yake, jambo ambalo husababisha madhara kwa friji au hata kwa watumiaji wake.
Leo tunaangazia dhana tano ambazo zimekuwa zikitafsiriwa visivyo na watumiaji wa friji kwa kujua au kutokujua, licha ya kuwa vifaa hivyo huwa na maelekezo ya jinsi ya kutumia kwa ufanisi mara baada ya kununua:
Unaweza kugandisha au kupoza chakula chochote
Baadhi ya watu wamekuwa wakiweka vyakula vya aina zote kwenye friji hata vile vinavyoweza kutumiwa bila kuhifadhiwa kwenye kifaa hicho.
Wengine hawafahamu kuwa baadhi ya mboga za majani, matunda na vitu laini havitakiwi kugandishwa kwenye friji. Mfano vyakula ambavyo vina maji mengi kama matikiti hayatakiwa kukaa kwenye friji kwa muda mrefu.Tovuti ya Love Food inayohusika na mapishi imeanisha vyakula vya aina 20 ambavyo havitakiwi kuwekwa kwenye friji kwa sababu havihitaji hali ya ubaridi. Vyakula hivyo ni pamoja na vitunguu maji na saumu, karanga, asali, mafuta ya kula, viazi, ndizi na mikate.
Muhimu ni kufahamu kuwa unaweza kuweka baadhi ya vyakula kwenye friji kwa muda mfupi kabla ya kuvitumia lakini vingine vikaa muda mrefu ndani ya friji vinaharibika.
Unashauriwa kujifunza zaidi kuhusu vyakula unavyopaswa kuweka kwenye friji lako ili kuliongezea ufanisi na uhai.
Siyo kila chakula unatakiwa kuweka kwenye friji. Weka vile vinavyohitaji ubaridi. Picha|Mtandao.
Kuweka chakula cha moto kwenye friji
Dhana hii pia inaleta utata kwa watumiaji, kuwa kuweka chakula cha moto kwenye friji siyo sahihi. Hilo siyo kweli. Ukishapika chakula na hukitumii kwa wakati huo weka kwenye friji. Kinapokaa muda mrefu nje, uwezekano wa kuharibika ni mkubwa.
Hata hivyo, unashauriwa usiweke chakula cha moto sana kwenye friji kwa sababu kinaweza kuleta madhara na kupunguza ufanisi wake.
Kila friji linatakiwa kuwekwa juu ya kibebeo
Siyo lazima kutumia kibeba friji (stand). Matumizi ya kibebeo hicho yanategemea ni wapi unatumia friji hiyo ukiwa nyumbani. Mfano kama eneo unalohifadhi friji lina maji au sakafu siyo nzuri unaweza kutumia kibebeo ili kulikinga na uharibifu.
Lakini friji nyingi zinazoingia sokoni kwa sasa zina vibebeo kwa chini ambavyo vimefungwa tayari pamoja na friji. Ukinunua ni kutumia tu.
Zinazohusiana
- Makosa unayotakiwa kuepuka wakati unatumia simu yako
- Mbinu tano za kudhibiti matumizi makubwa ya intaneti kwenye ‘smartphones’
Kusafisha koili za nje
Baadhi ya watumiaji wamekuwa wakisafisha ndani ya friji na kuacha maeneo mengine hasa upande wa nyuma ambako kuna vifaa vinavyoendesha kifaa hicho ikiwemo koili (Fridge Cooling Coil) zinazosaidia chakula kiwe cha baridi.
Kazi ya koili hizo ni kuondoa joto toka kwenye friji.
Ukaaji wa koili hizo hutegemea muundo wa friji. Zipo koili zilizo nyuma au chini ya friji. Wakati mwingine vumbi na chembe chembe za uchafu hujishika kwenye koili hizo.
Uchafu huu unaweza kusababisha jokofu kuongeza msukomo wa kazi yake, kulichosha na kusababisha matengenezo ya gharama kubwa.
Kusafisha koili za nje ya friji ni rahisi sana. Zima friji, livute na futa vumbi kwenye koili kwa kitambaa au brashi laini lisilo na maji.
Wataalam wa mtandao wa Realtor wanashauri kuwa koili za friji zisafishwe kila baada ya miezi sita ili zifanye kazi kama inavyotakiwa.
Koili za nyumba ya friji ni muhimu, zingatia usafi wake ili zifanya kazi kama inavyohitajika. Picha|Mtandao.
Kuyeyusha barafu ya friji
Wapo wanaamini kuwa hutakiwi kuyeyusha barafu na kulisafisha friji kwa ndani. Hii siyo kweli. Wakati unanunua friji linakuwa halina barafu, bali hujitengeneza baada ya kuanza kulitumia.
Wakati mwingine barafu hujikusanya kiasi cha kuzuia mlango wa friji kufunga vizuri. Unahitaji kuyeyusha barafu ndani ya friji ili kupata nafasi ya kuweka vyakula vyako.
Njia rahisi ni kuzima friji uli kuruhusu barafu iyeyuke. Kabla haijayeyuka hadi kuwa maji, unaweza kutoa vipande vya barafu. Baada ya barafu yote kutoka washa tena na weka vitu vyako kwenye friji ili kuendelea kutumia.
Usilazimishe kutoa barafu kwa vitu vyenye ncha kali kama kisu na vinginevyo. Utaishia kuharibu friji lako na hata kulitoboa.
Hata hivyo, kudumu kwa friji lako hutegemea zaidi jinsi unavyolitunza na kuzingatia maelekezo kwa usahihi wa matumizi yake.