Mfumo wa kielektroniki wa taarifa za usafirishaji wazinduliwa Tanzania
- Umezinduliwa na wadau wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF)
- Utasaidia kuwapunguzia wafanyabiashara gharama za usafirishaji wa bidhaa katika nchi za jirani ikiwemo Zambia.
Dar es Salaam. Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imezindua mfumo wa kielektroniki wa habari za manunuzi, uuzaji na usafirishaji (NFLIP) utakaowasaidia wafanyabiashara kupunguza gharama za usafirishaji wa bidhaa katika nchi za jirani ikiwemo Zambia.
Mfumo huo umezinduliwa leo (Desemba 10, 2019) jijini Dar es Salaam na Jukwaa la Wafanyabiashara Tanzania kwa kushirikiana na wadau kutoka TPSF utakaotumika katika nchini na nchi jirani.
Akizindua mfumo huo, Mwenyekiti wa Kampuni ya Simba Group, Azim Dewji amesema kuwa, mfumo huo utawarahisishia wafanyabiashara kwa kupunguza gharama za usafirishaji kutoka eneo moja kwenda jingine.
“Mfumo huu utasaidia sana,badala ya mtu kutoka hapa kwenda Zambia au Congo kununua mzigo, ukifika kule, utatafute hoteli, utatumia usafiri wa ndani ya nchi uliopo, mawasiliano ya ndani hiyo ni gharama, lakini ukitumia mtandao wa NFLIP utaokoa gharama nyingi kwani utafanya hayo yote kwa wakati mmoja,”, amesema Dewji.
Zinazohusiana:
- Sababu zilifanya Tanzania iporomoke viwango vya ufanyaji biashara duniani
- Kiswahili ndiyo mpango mzima kusaka wateja Tanzania: Ripoti
- Sekta binafsi yazungumzia Kairuki kuteuliwa kusimamia uwekezaji
Mfumo huo unamuwezesha mfanyabiashara kupata taarifa mbalimbali zinazohusu bidhaa na huduma zinazotolewa nchini na nchi jirani, jambo linaloweza kumsaidia kufanya maamuzi sahihi ya muda na pesa wakati anasafirisha bidhaa hizo
Akizungumza na wanahabari mara baada ya uzinduzi wa mfumo huo, Mkurugenzi wa Miradi ya Uendelezaji wa Biashara kutoka TPSF, Edward Furaha amesema teknolojia hiyo itaongeza ufanisi kwa wafanyabiashara kwa kupunguza gharama na muda unaotumika katika usafirishaji wa bidhaa.
’Mfumo huu unawahusu wafanyabiashara, wasafirishaji na wenye bidhaa, hivyo ni teknolojia itakayowaweka pamoja watu wote hao kwa wakati mmoja na kwa gharama nafuu,” amesema Furaha.
TPSF imekuwa mdau muhimu katika kuboresha mazingira ya sekta binafsi nchini ikiwemo kutumia mifumo ya kidijitali yenye tija kwa wafanyabiashara na Serikali.
Latest